BEI YA MAFUTA YAZIDI KUPOROMOKA
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), imetangaza kushuka zaidi kwa bei za bidhaa za mafuta hapa nchini kuanzia leo, kutokana na bei katika soko la dunia kuendelea kuporomoka.
Mwezi
uliopita, kwa mara ya kwanza baada ya muda mrefu, bei ya petroli,
dizeli na mafuta ya taa ilishuka kwa kiasi kikubwa, mathalani bei
ikifikia chini ya Sh 2,000. Na jana, bei ya juu kabisa ya petroli
ilitangazwa kushuka kwa Sh 187 zaidi.
Nafuu
hiyo ya bei ilitangazwa na Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Felix Ngamlagosi,
akisema bei hizo za kikomo za bidhaa ya mafuta zitaanza kutumika leo
nchi nzima na kwamba mabadiliko hayo ya bei yanatokana na kushuka kwa
bidhaa hiyo katika soko la dunia.
Alisema
bei za jumla na rejareja kwa aina zote za mafuta yakiwemo petroli,
dizeli na mafuta ya taa zimeshuka, ikilinganishwa na bei katika toleo
lililopita la Januari 7, mwaka huu.
“Katika
toleo hili bei za rejareja kwa petroli zimepungua kwa Sh 187 kwa lita
sawa na asilimia 9.56, dizeli imepungua kwa Sh 139 kwa lita sawa na
asilimia 7.53 na mafuta ya taa yamepungua kwa Sh 177 kwa lita sawa na
asilimia 9.64,” alisema.
Aidha,
alisema kwa kulinganisha matoleo hayo mawili bei za jumla zimepungua
ambapo petroli imepungua kwa Sh 186.89 kwa lita sawa na asilimia 10.08,
dizeli Sh 138.97 kwa lita sawa na asilimia 7.97 na mafuta ya taa kwa Sh
176.64 kwa lita sawa na asilimia 10.20.
“Bei
za mafuta masafi katika soko la dunia kwa petroli, dizeli na mafuta ya
taa zimepungua kati ya mwezi Julai na Desemba 2014 kwa takribani dola
440 kwa tani, dola 304 kwa tani na dola 324 kwa tani sawia sawa na
punguzo la asilimia 44,35 na 35 sawia,” alisema.
Alisema
kati ya mwezi Septemba 2014 na Februari 2015, bei za petroli, dizeli na
mafuta ya taa katika soko la ndani zimepungua kwa Sh 499 kwa lita, Sh
384 kwa lita na Sh 384 kwa lita sawia, ambayo ni sawa na punguzo la
asilimia 22, 18 na 19 sawia.
"Katika
kipindi husika, thamani ya shilingi ya Tanzania ikilinganishwa na dola
ya Marekani imeshuka kwa asilimia 6. Bei ya mafuta kwenye soko la ndani
ingeweza kupungua zaidi kama thamani ya shilingi isingeendelea
kudhoofu," alisema.
Pia,
Ngamlagosi alisema ni muhimu kuzingatia kwamba kwa wastani bei za
mafuta katika soko la dunia na gharama za uagizaji (CIF) huchangia
asilimia 60 ya bei ya mafuta katika soko la ndani, hivyo kiwango cha
ushukaji bei katika soko la ndani hakiwezi kuwa sambamba na asilimia ya
ushukaji katika soko la dunia.
"Kampuni
za mafuta zipo huru kuuza bidhaa za mafuta ya petroli kwa bei ya
ushindani ilimradi bei hizo ziko chini ya bei ya kikomo kama
ilivyokokotolewa na fomula iliyopitishwa na EWURA na ambayo ilichapwa
kwenye gazeti la serikali namba 354 la Septemba 26, 2014," alisema.
Alisema
vituo vyote vya mafuta vinatakiwa kuchapisha bei za bidhaa za mafuta
katika mabango yanayoonekana bayana na yakionesha bei ya mafuta,
punguzo, vivutio vya biashara au promosheni zinazotolewa na kituo
husika.
"Pale
ambapo inawezekana kuchagua wateja wanashauriwa kununua bidhaa za
mafuta kutoka kwenye vituo vinavyouza mafuta kwa bei ndogo zaidi ili
kuimarisha ushindani. Ni kosa kuuza mafuta bila kuweka mabango ya bei
inayoonekana vizuri kwa wateja na adhabu itatolewa kwa kituo husika," alisema.
Aidha
aliwataka wanunuzi kuhakikisha wanapata stakabadhi ya malipo
inayoonesha jina la kituo, tarehe, aina ya mafuta yaliyonunuliwa na bei
kwa lita.
Alisema
stakabadhi hiyo ya malipo itatumika kama kidhibiti cha mnunuzi wa
mafuta endapo kutajitokeza malalamiko ya ama kuuziwa mafuta kwa bei ya
juu kuliko bei kikomo au endapo mnunuzi atakuwa ameuziwa mafuta yenye
kiwango cha ubora kisichofaa.
Alisema
bei za kikomo kwa Dar es Salaam bei za rejareja kwa lita moja ya
petroli ni Sh 1,768, dizeli Sh 1,708 kwa lita na mafuta ya taa ni Sh
1,657 kwa lita huku bei za jumla ikiwa ni Sh 1,666.43 kwa lita ya
petroli, Sh 1,605.52 kwa lita ya dizeli na Sh 1,554.59 kwa lita ya
mafuta ya taa.
Hata
hivyo, alizitaka mamlaka mbalimbali kuhakikisha zinawawezesha wananchi
kuona manufaa ya kupungua kwa bei ya bidhaa hiyo hasa katika sekta ya
usafirishaji na nishati ya umeme.
Pamoja
na nafuu hiyo ya bei, wataalamu mbalimbali wa masuala ya uchumi,
wakiwemo wanasiasa waliohoji kwa muda mrefu sababu za kutoshuka kwa bei
ya mafuta nchini, hawakuwa tayari kuzungumzia mapema juu ya punguzo hilo
la bei.
Zitto
Kabwe, Mchumi na Mbunge wa Kigoma Kaskazini anayeiongoza Kamati ya
Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), alipotafutwa kuzungumzia hilo,
alisema hajapata taarifa rasmi, hivyo hatakuwa tayari kusema lolote.
No comments:
Post a Comment