TIFFAN ENT

TIFFAN ENT

TUKO WANGAPI

TUKO WANGAPI

GLORY FREIGHT

GLORY FREIGHT

Thursday, February 5, 2015

BUNGE LARIDHIKA NA HALI YA ULINZI NA USALAMA WA RAIA 

hussein
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Hussein Mwinyi akijibu swali la mbunge Bungeni Dodoma.
BUNGE limeridhishwa na hali ya ulinzi wa nchi, usalama wa raia na mali zao kwa kipindi cha mwezi Februari mwaka 2014 hadi Januari mwaka huu kutokana na hali ya ulinzi wa nchi na usalama wa raia kuwa shwari.

Hayo yamesemwa na Kamati ya Bunge ya Ulinzi na Usalama kupitia Mjumbe wa kamati hiyo Capt. Mstaafu John Chiligati wakati akiwasilisha taarifa ya kamati hiyo kwa kipindi cha mwezi Februari 2014 hadi Januari 2015, bungeni mjini Dodoma.

Alisema pamoja na hali kuwa shwari kulikuwepo na changamoto chache za uvunjifu wa amani, vitendo vya uporaji mali na matukio ya mauaji ya vikongwe na watu wenye ualbino yaliyotokea katika baadhi ya mikoa.

"Katika ziara ya kamati pamoja na taarifa kutoka kwenye wizara husika, Kamati ilibaini kuwa kwa ujumla hali ya ulinzi wa nchi na usalama wa raia katika kipindi hiki ilikuwa shwari" alisema Capt. Mstaafu Chiligati na kuongeza:

"Ijapokuwa zipo changamoto chache za uvunjifu wa amani na vitendo vya uporaji mali na matukio ya mauaji ya vikongwe na watu wenye ualbino yaliyotokea katika baadhi ya mikoa"
Capt. Mstaafu Chiligati alilipongeza Jeshi la Ulinzi la Wananchi kwa kazi kubwa na nzuri inayofanya ya kulinda mipaka ya nchi kwani katika kipindi hiki hali ya mipaka ya nchi imekuwa shwari.

Alibainisha kuwa ili kudumisha hali iliyopo, aliishauri Serikali itenge fedha za kutosha ili kuviwezesha vyombo vya ulinzi na usalama kufanya kazi nzuri zaidi na kuifanya hali ya nchi kendelea kutulia na kuwa na amani na utulivu.

Kwa upande wa masuala ya Ulinzina Usalama wa Mipaka, Capt. Mstaafu Chiligati alisema katika kipindi hicho hali katika mipaka yote ya Tanzania imekuwa shwari licha ya kuwepo kwa changamoto ya uingiaji wa wahamiaji haramu.

Kutokana na hali hiyo Kamati hiyo ililipongeza pia Jeshi la Polisi nchini kwa jitihada za kudhibiti uhalifu kote nchini na kupunguza matukio ya uhalifu katika baadhi ya maeneo yaliyokubwa na matukio hayo hivi karibuni.

"Aidha Kamati ilipotembelea mkoa wa Arusha iliridhika na hali ya kupungua kwa matukio ya uhalifu na pia ilikuta hali ya utulivu na amani imerejea katika jiji la Arusha" alisema Capt. Mstaafu Chiligati.

Alieleza kuridhishwa kwa kamati na taarifa za kukamtwa na kufunguliwa kesi mahakamani kwa baadhi ya watuhumiwa wa matukio ya kigaidi yaliyotokea katika mkoa wa Arusha.

Hata hivyo kamati alishauri kwamba kesi hiyo isikilizwe haraka na kutolewa hukumu ili ikidhi matarajio ya wananchi.

Kwa upande wa Mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa mujibu wa Sheria, kamati iliishauri Serikali kuongeza muda wa mafunzo hayo kutoka miezi 3 hadi miezi 6 huku ikiitaka Serikali kuwachukulia hatua za kisheria wanafunzi wanaokwepa kuhudhuria mafunzo bila ya sababu za msingi.

Aliishauri Serikali kupitia Wizara ya Ulinzi na JKT na ile ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kukaa pamoja ili kutafuta njia ya kuoanisha mihula ya vyuo ili isigongane na muda wa mafunzo ya JKT kwa mujibu wa sheria

No comments:

Post a Comment