WAZIRI MEMBE ALIPONGEZA KANISA LA SDA
Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Benard Membe akifanya
mazungumzo na Rais wa Baraza Kuu la Makanisa ya Sabato Duniani Askofu
Ted Wilson wakati wa siku ya ufungaji wa Kongamano hilo lililofanyika
Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Benard Membe ambaye
alikuwa mgeni rasmi akiwahutubia wananchi pamoja na wageni wengine
waalikwa (hawapo pichani) wakati wa siku ya ufungaji wa Kongamano hilo
lililofanyika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Watoto
wakitoa burudani mbele ya mgeni rasmi (hayupo pichani) wakati wa siku ya
ufungaji wa Kongamano hilo lililofanyika Uwanja wa Taifa jijini Dar es
Salaam.
Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Benard Membe
(aliyesimama katikati) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya
viongozi wa Makanisa ya Wasabato (SDA) wakati wa siku ya ufungaji wa
Kongamano hilo lililofanyika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam siku
ya tarehe 7 Februari, 2015.
(PICHA ZOTE NA BENEDICT LIWENGA-MAELEZO-DSM)
Na Benedict Liwenga, Maelezo-Dar es Salaam.
WAZIRI wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard Membe
amelipongeza Kanisa la Wasabato (SDA) kwa kuwa mfano mzuri wa
ustahimilivu, uvumilivu wa kidini na imani katika Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.
Mhe.
Membe ameyasema hayo leo wakati alipokuwa akifunga rasmi Kongamano la
siku 4 (4-7 Februari, 2015) Kimataifa la Utume kwa Kanisa la Sabato
lililofanyika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam ambalo lilishirikisha
Mataifa zaidi ya 20 Duniani.
Alisema
kuwa, katika kipindi chote cha uongozi wake kama Waziri hajawahi kusikia
mgogoro wala matatizo yakioongozwa na SDA dhidi ya madhehebu mengine ya
dini hapa nchini na hata dhidi ya wananchi.
"Mpo
mnafanya kazi zenu, mnachapa shughuli zenu kwa amani na utulivu,
hamjachokoza mtu na hiyo ni sifa ya dini mojawapo yenye amani duniani",
alisema Mhe. Membe.
Alisisitiza
kwa kuwataka wananchi wa dini zote nchini kuiga mfano wa wana SDA ili
Tanzania iendelee kuwa nchi yenye amani na utulivu.
Aidha,
alieleza kuwa, Dini na Diplomasia vina husiana pale masuala ya amani,
ulinzi na usalama yanapoguswa huku akiwataka wananchi wa dini zote
nchini kushiriki katika kutengeneza viongozi bora katika jamii kwa
misingi ya uadilifu ambao watasimamia amani na kujiepusha na vitendo
viovu ikiwemo rushwa.
Aliongeza
kuwa dhamira ya Serikali ya kuendelea kushirikiana nalo kwa ajili ya
ustawi wa nchi huku akieleza kuwa, Serikali itaendelea kulinda uhuru wa
kuabudu kwa dini zote kama inavyoelezwa kwenye Katiba ya Jamhuriu ya
Muungano wa Tanzania.
Naye Rais
wa Baraza Kuu la Makanisa ya Sabato Duniani, Askofu Ted Wilson alisema
kuwa anawaombea Viongozi wa Tanzania waendelee na maono kwa lengo la
kuwatumikia wananchi na kwamba wakimtumaini Mungu atawawezesha kupata
maono mapya kwa ajili ya kulitumikia Taifa zima.
Kongamano
hilo lilishirikisha Mataifa zaidi ya 20 ambapo Kanisa hilo la Wasabato
ni Kanisa linalokua duniani likiwa na Waumini milioni 307 huku Waumini
milioni 30 wakiwa Afrika na takriban milioni 5 wakiwa Tanzania.
No comments:
Post a Comment