Watanzania waonywa urais wa fedha, udini
WAZIRI wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe amewataka
Watanzania kuwapuuza wanasiasa wenye kutaka kutumia fedha, dini, ukabila
na aina yoyote ya ubaguzi kujijengea uhalali na kuombea kura katika
uchaguzi mkuu ujao.
Akifunga
Mkutano wa Kimataifa wa Utume wa Kanisa la Waadventista Wasabato, Dar es
Salaam juzi, Membe ameliomba kanisa hilo kuzungumza na vijana wao na
kuwakumbusha wajibu wao wa kulinda amani na kufanya uchaguzi sahihi na
kutokubali kutumika.
“Nawasihi
muwapuuze wanasiasa wenye mwelekeo huo... hawa ni hatari kwa umoja na
upendo wetu. Tuwachague wale wenye ulimi wa upendo, unyenyekevu, utu na
amani. Tumwepuke shetani na kazi zake za ufisadi, rushwa na maovu
mengine,” alisema Membe.
Mkutano
huo wa kimataifa wa utume maarufu kama ‘Mission Extravaganza’ ulianza
Jumatano wiki iliyopita katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na
uliwahusisha waumini wa kanisa hilo kutoka nchi 11 zilizoko katika
ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, lengo lake likiwa ni kuwaandaa watu
kiakili, kijamii na kiroho ili waweze kuishi maisha yenye uadilifu.
Zaidi ya
watu 2,400 walibatizwa katika mkutano huo. Membe alisema mwaka huu,
licha ya nchi kufanya uchaguzi mkuu lakini pia ina tukio lingine la kura
ya maoni ya katiba, hivyo akasisitiza waumini wa kanisa hilo kuliweka
taifa kwenye maombi.
“Nasisitiza hilo kwa kutambua kuwa kipindi kama hiki huja na migongano na mivutano katika nchi zenye demokrasia changa.”
Membe pia
alitoa rai kwa waumini wa Kanisa hilo la Waadventista Wasabato
kushiriki kikamilifu katika kutengeneza viongozi bora wa Serikali
wanaozingatia misingi ya uadilifu, upendo na unyenyekevu.
Membe
alisema kuwa dini na madhehebu yanayo nafasi kubwa katika kujenga jamii
yenye maadili na hofu ya Mungu, wakiwemo viongozi na hivyo kusababisha
taifa kuwa na amani, upendo na mshikamano.
Alieleza
kuwa kama Waziri wa Mambo ya Nje, amejifunza kuwa diplomasia na hofu ya
Mungu vikifanya kazi pamoja hakuna changamoto yoyote isiyoweza
kukabiliwa.
“Dini na
Diplomasia vinahusiana pale masuala ya amani, ulinzi na usalama
yanapoguswa. Hivyo nawaomba mshiriki katika kutengeneza viongozi bora
katika jamii zetu kwa misingi ya uadilifu ambao watasimamia amani na
kujiepusha na vitendo viovu ikiwemo rushwa,” alisema Membe.
Aidha,
alilipongeza kanisa hilo kwa kuwa mfano mzuri wa ustahimilivu na
uvumilivu wa kidini hapa nchini. Alieleza kwamba kamwe hajawahi kusikia
Kanisa la Waadiventista Wasabato limeingia katika mgogoro na Serikali,
dhehebu au dini nyingine.
Alisema
hilo ni funzo kubwa kwa Watanzania, kwamba kutofautiana kiitikadi,
kidini, kikabila au rangi si sababu tosha ya kuwagombanisha na kuvuruga
amani ya nchi.
“Nalipongeza
kanisa lenu kwa kuwa mfano mzuri wa uvumilivu wa kidini na imani,
mnaendesha mambo yenu kwa uvumilivu mkubwa na kushirikiana na dini zote
na hili linatufundisha kuwa kutofautiana kwetu sio sababu tosha ya
kugombana,” alisisitiza Membe.
Membe
alilihakikishia kanisa hilo dhamira ya Serikali ya kuendelea
kushirikiana nalo kwa ajili ya ustawi wa nchi na kufafanua kuwa Serikali
itaendelea kulinda uhuru wa kuabudu kwa dini zote kama inavyoelezwa
kwenye Katiba ya nchi.
“Serikali
inao wajibu wa kusaidia dini na madhehebu kufanya kazi kwa uhuru.
Bahati nzuri Katiba inayopendekezwa imezingatia kulinda uhuru huo hivyo
tuiunge mkono,” alifafanua Waziri Membe.
Aidha,
amelisifu kanisa hilo kwa kuanzisha miradi ya huduma zikiwemo Shule 15
za Sekondari na Msingi, Chuo Kikuu na Hospitali mbili ambavyo vinatoa
mchango mkubwa kwa serikali na wananchi kwa ujumla.
Awali
akimkaribisha Waziri Membe kufunga kongamano hilo, Kiongozi Mkuu wa
Kanisa hilo duniani, Askofu Dk Ted Wilson alisema kuwa anawaombea
viongozi wa Tanzania waendelee kuwa na maono kwa ajili ya kuwatumikia
wananchi na kwamba wakimtumaini Mungu atawawezesha kupata maono mapya
kwa ajili ya kulitumikia Taifa hili.
Kwa
upande wake, Kiongozi wa Kanisa hilo Kanda ya Afrika Mashariki na Kati,
Askofu Blasius Luguri aliipongeza Tanzania kwa kudumisha amani ambayo
imechangia kuichagua Tanzania kuwa mwenyeji wa Kongamano hilo
lililoshirikisha Mataifa zaidi ya 20.
Aidha,
alimwomba Waziri Membe kufikisha ujumbe kwa Rais Jakaya Kikwete kuwa
wana imani na Tanzania kuwa ni nchi ya amani, usalama na utulivu.
Kanisa la
Sabato ni kanisa linalokua duniani likiwa na waumini milioni 307 huku
waumini milioni 30 wakiwa Afrika na takriban milioni 5 wakiwa Tanzania.CHANZO:HABARI LEO
No comments:
Post a Comment