SERIKALI YAPATA SH. BILIONI 15 ZA KULIPA MADENI YA MAHINDI
SERIKALI
Serikali imepata mkopo wa sh. bilioni 15 ambazo zitatumika kulipa kiasi
cha madeni ya mazao ya nafaka ambayo wakulima wanaidai kupitia Wakala wa
Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA).
Hayo
yamesemwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda kwa nyakati tofauti wakati
akizungumza na wananchi wa Mkoa wa Iringa akiwa kwenye ziara ya kikazi
ya kukagua maendeleo katika mkoa huo.
Akizungumza
na wananchi mara baada ya kukagua Chama cha Ushirika cha Akiba na
Mikopo (SACCOS) cha Mazombe kilichopo Ilula wilayani Kilolo, mwishoni
mwa wiki, Waziri Mkuu alisema katika kipindi cha mwezi huu, Serikali
imepata mkopo huo kutoka benki ya CRDB ambazo zimesambazwa kwenye mikoa
mbalimbali ili kuwalipa wakulima hao.
Alisema
hadi kufikia Machi mwaka huu, Serikali itahakikisha inamaliza kulipa
madeni kwa wakulima ambao waliuza mazao yao kwa Wakala wa Taifa wa
Hifadhi ya Chakula (NFRA).
Akifafanua
kuhusu mgao wa fedha hizo, Waziri Mkuu alisema kanda ya Arusha wamepata
sh. bilioni 1.72/-; kanda ya Dodoma sh. bilioni 2.02/-; kanda ya Kipawa
sh. milioni 632.3/-; kanda ya Makambako sh. bilioni 4.58/-; kanda ya
Shinyanga sh. milioni 238.85/-; kanda ya Songea sh. bilioni 1.97/- na
kanda ya Sumbawanga sh. bilioni 3.82/-.
Alisema
fedha hizo zimegawanywa kwenye vituo, vikundi na mawakala na kuongeza
kuwa Serikali kupitia Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika itatoa sh.
bilioni 15 nyingine ili zigawanywe katika kanda na kumaliza kabisa
madeni ya wakulima.
Alitoa
ufafanuzi huo baada kutolewa malalamiko kuwa ucheleweshwaji wa malipo
hayo kwa wakulima umewafanya baadhi yao washindwe kurejesha mikopo
kwenye taasisi za fedha kwa wakati.
Alisema
ucheleweshwaji wa malipo hayo ulitokana na ziada ya chakula kwenye msimu
wa kilimo wa mwaka 2014 kuongezeka kwa kufikia zaidi ya tani milioni
1.3, ukilinganisha na ziada ya tani 300,000 za msimu uliopita. "Serikali
ililazimika kununua mazao ya wakulima zaidi ya malengo yake... matokeo
hayo mazuri ya kilimo, yalitokana na msisitizo wa Serikali kuwekeza
kwenye pembejeo, mbegu bora pamoja na kuingiza nchini matrekta zaidi ya
1600.
Mapema,
akisoma taarifa ya chama hicho mbele ya Waziri Mkuu, Mwenyekiti wa
Mazombe SACCOS, Bw. Yohanes Mwemtsi, alisema kucheleweshwa kwa marejesho
ya mikopo iliyochukuliwa na wakulima kunazorotesha maendeleo ya SACCOS
hiyo kwa kushindwa kujiimarisha kimtaji.
Alisema
licha ya changamoto hiyo, chama hicho kimeshatoa mikopo yenye thamani ya
sh. bilioni 4.3 kwa wanachama wake zaidi ya 1,300 huku kukiwa na
ongezeko la wanachama wapya kwa wastani wa asilimia 10 kila mwaka.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATATU, FEBRUARI 23, 2015
No comments:
Post a Comment