'Magaidi wa Tanga' Watiwa Mbaroni.....Mwili wa Mwanajeshi wa JWTZ Aliyeuawa katika Mapigano hayo Waagwa
Serikali imetoa taarifa rasmi kuhusu uhalifu uliotikisa mkoani Tanga, ikisema hali ni shwari na umma wa Watanzania upuuze taarifa zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zikitia hofu.
Aidha, imesema watu kadhaa wanashikiliwa wakihusishwa na uhalifu huo.
“Tunawashikilia
ila mpaka sasa siwezi kukueleza idadi yao na kwamba ni wa kikundi cha
ugaidi au la. Hao watu tunafanya nao mahojiano ili kuweza kuelewa kama
wanahusika kwenye tukio hilo,” alisema Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Juma Ndaki.
Akitoa
taarifa kwa waandishi wa habari, Ndaki alisema hali katika kitongoji
cha Majimoto, Amboni na mkoa wa Tanga kwa ujumla iko shwari. “Tunaendelea kufanya uchunguzi kubaini hao wahalifu pamoja na silaha zilizoibwa,” alisema.
“Tunaomba
wananchi waendelee kutoa ushirikiano wao hasa wanapoona watu wenye
majeraha au wanaowahisi kwamba ni wahalifu ili nasi tuweze kuwachunguza
kama wanahusika kwenye tukio hili”, alisema.
Ingawa
Kamanda hakuelezea mazingira ya kukamatwa kwa watuhumiwa, waandishi wa
habari waliozuru eneo la Amboni yalikotokea mapigano, waliarifiwa
kwamba baadhi ya wavuvi kwenye Mto Zigi, walimkamata mtu wakimtuhumu
kukutwa akifua nguo zenye damu.
Katika
mapigano hayo baina ya askari na wahalifu, yalisababisha kifo cha
askari wa JWTZ, Sajenti Said Kajembe na wengine kujeruhiwa.
“Asubuhi
wavuvi kadhaa walikuwa hapo mtoni ghafla walikutana na mtu pembeni ya
mto akiwa anafua kanzu pamoja na vifaa fulani kama nguo za kufunika uso
..’maski’ ikabidi wawapigie haraka polisi simu lakini hawakuweza
kupatikana na ndipo wakawapigia askari wa JWTZ ambao walifika haraka
eneo la tukio na kumkamata mhusika”, alisema mkazi mmojawapo.
Kwa
upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Magalula Said Magalula aliwataka
wakazi wa Tanga na vitongoji vyake, kuondoa hofu kwa kuhakikisha
wanaendelea na shughuli zao za uzalishaji kwa sababu ulinzi umeimarishwa
na hali ya usalama ni shwari.
Pia,
aliwataka wananchi na wageni wenye mpango wa kutembelea eneo la
kihistoria la Mapango ya Amboni, kuendelea na ratiba zao kwa sababu eneo
hilo liko salama na tangu awali halikuhusika kwenye vurugu hizo.
Magalula ambaye pia alikutana na waandishi wa habari, alisema “Hali
ni nzuri ulinzi na usalama uko imara… naomba wananchi waondoe hofu,
wawe na amani na waendelee na shughuli zao za uzalishaji… hakuna tatizo
kabisa usalama umedhibitiwa vizuri.”
Mkuu huyo wa mkoa ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, alisisitiza “Naomba
Watanzania wenzangu muelewe kwamba eneo lilipofanyika tukio la mapigano
na wahalifu si pale yalipo mapango ya Amboni ... maeneo hayo yapo mbali
na nitoe mwito kwa wageni wenye mpango wa kutembelea hapo wawe huru
kufanya hivyo mahali hapo ni salama.”
“Naomba
Watanzania nchini kote kwa ujumla wawe na amani kwa sababu Tanga iko
shwari hakuna tena hizo vurugu za wahalifu… naomba wasiamini sana
taarifa zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii… sisi tuko shwari na
shughuli za kijamii zinaendelea kama kawaida ikiwemo Amboni,” alisema.
Akizungumzia
mapigano hayo yaliyotokea Februari 14, alisema licha ya majibizano ya
kurushiana risasi yaliyofanywa na askari wa Polisi kwa kushirikiana na
wa JWTZ , uchunguzi unaendelea kuwapata wahusika.
“Vikosi
vya usalama vinaendelea na juhudi za kuwasaka pamoja na kutafuta silaha
zetu lakini hakuna mtu yeyote anayeshikiliwa … zipo simulizi mbalimbali
zinazoendelezwa kwenye mitandao ya kijamii ila sisi serikali ya mkoa
bado hatujathibitisha kwamba watu hao ni wa kikundi gani ila
ninachokifahamu hao watu ni wahalifu”, alisisitiza.
Kuhusu
kuongezeka kwa matukio katika maeneo mbalimbali mkoani humo, alisema
kila tukio linachukuliwa kwa uzito mkubwa na linashughulikiwa kwa namna
linavyotokea.
Aidha,
amewataka wakazi wa Tanga hususan wanaoishi eneo la Amboni na vitongoji
vyake kuhakikisha wanaendelea kutoa habari sahihi kuhusu watu
mbalimbali wanaowatilia shaka . Alisema taarifa hizo zina umuhimu wa
kipekee kwa askari katika kufanikisha kukamatwa kwa wahalifu hao.
Kutokana
na maswali mengi ya wanahabari na wananchi, kudai kutoridhishwa na
mwenendo wa utoaji taarifa kuhusu tukio hilo, Mkuu wa Mkoa aliruhusu
watembelee eneo la tukio kuthibitisha kama hali ni shwari katika eneo
husika.
Timu
ya wanahabri takribani 10 kutoka vyombo mbalimbali vya habari, wakiwa
chini ya ulinzi wa askari walipelekwa eneo la tukio, ambalo liko umbali
wa takribani kilometa tano kutoka yaliko Mapango ya kihistoria ya
Amboni.
Eneo
hilo limetawaliwa na miamba ya mawe makubwa yenye mapango, ambayo
hayatumiki kwa shughuli za kihistoria, kama ilivyo katika kitongoji cha
Kiomoni yalipo mapango ya kihistoria ya Amboni.
Shughuli
zinazoonekana kufanyika jirani na eneo hilo, ni ulipuaji wa miamba kwa
kutumia baruti ambao hufanywa na wachimbaji wadogo kisha kuvunja kokoto
kwa ajili ya viwanda vya kutengeneza chokaa pamoja na mawe kwa shughuli
za ujenzi mjini hapa.
Eneo
wanakodaiwa kuishi wahalifu hao, liko umbali wa meta 300 kutoka upande
wa pili zinapofanyika shughuli za upasuaji kokoto zinazoendeshwa na
wakazi wa kitongoji cha Majimoto na Mafuriko huko Amboni.
Katika
eneo hilo, kulikuwa na ukimya kutokana na kutokuwapo shughuli yoyote
hususani uvunjaji kokoto iliyozoeleka kutokana na wananchi kusimamishwa
kutokana na tukio hilo.
Waandishi
wa habari walilazimika kufuata maelekezo yaliyokuwa yakitolewa na
wanausalama waliokuwa wakiwaongoza kufika ndani ya pango husika.
Mwonekano
wa eneo hilo, ulidhihirisha ni la hatari kutokana na mapango kufunikwa
na vichaka. Ndani ya pango hilo, upo uwazi mkubwa unaoashiria uwepo wa
shughuli za kibinadamu zilizokuwa zikiendelea.
Ndani
ya pango hilo, zilikutwa nguo; hususan suruali, madumu ya kuhifadhia
maji, vikombe kadhaa vya plastiki, chupa za maji ya kunywa zilizotumika
hatua ambayo imedhihirisha kuwapo binadamu waliokuwa wakikaa humo licha
ya kwamba, kufika kwake ni kwa shida.
Wakazi wazungumza
Wakizungumza
na waandishi, baadhi ya wakazi wa maeneo jirani na eneo hilo, walisema
hawajaruhusiwa kufika eneo hilo kwa kuwa linaendelea kulindwa na askari
wa Polisi wa kikosi cha kutuliza ghasia (FFU) kwa kushirikiana na
JWTZ.
“Muda
mfupi tu kabla ya ninyi kwenda huko, askari wa FFU walitoka huko ,
ninyi mnaelezwa kwamba pako shwari lakini sisi bado hatujaruhusiwa
kufika kule kwa sababu panalindwa muda wote na askari… ,” alisema mkazi aliyejitambulisha kwa jina moja la Mrisho.
No comments:
Post a Comment