Utafiti wawabeba vijana Urais 2015 Mwigulu
SHIRIKA
la Utafiti wa Maendeleo ya Elimu (TEDRO), limesema katika utafiti
walioufanya kuhusu ushiriki wa vijana katika siasa na matarajio kuelekea
uchaguzi mkuu 2015, umeonesha kwamba endapo mgombea urais kijana
atapendekezwa atakubalika kwa asilimia 82.
Akizungumza
na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa shirika
hilo, Jacob Kateri alisema katika wananchi hao waliohojiwa pia asilimia
11 walisema vijana hawatakubalika na asilimia saba walisema hawajui.
Alisema
utafiti huo umeandaliwa na kufanyika Tanzania Bara na maeneo
yaliyohusishwa ni kanda za kijiografia ili kuwezesha uhusishwaji mpana
wa Watanzania na katika kila wilaya wamehojiwa wananchi wa vijiji vitatu
kwa kuzingatia siasa za eneo husika.
Aidha
alisema utafiti huo umeonesha sababu mbalimbali zinazoweza kuwa
kichocheo cha vijana kuingia katika siasa ambapo zilizochukua uzito ni
uzalendo kwa asilimia 67 ambapo wananchi walisema vijana wengi wameingia
katika siasa kwa sababu ya uzalendo.
“Sababu
nyingine ni kimbilio baada ya kukosa ajira kwa asilimia 57, uwezo mdogo
wa watangulizi wao katika nafasi husika kwa asilimia 60, mafanikio ya
wanasiasa vijana walio mahiri asilimia 72, vyama vya siasa kuwapa nafasi
vijana katika vyama vyao kwa asilimia 59 na kukubalika kwa vijana kwa
asilimia 63,” alisema.
Aidha
alisema wanasiasa vijana waliopendekezwa kupitia chama tawala
aliyeoonekana kuongoza kwa kukubalika ni Mwigulu Nchemba kwa asilimia
38, Dk Emmanuel Nchimbi kwa asilimia 26, January Makamba kwa asilimia
24, William Ngeleja kwa asilimia 11 na Lazaro Nyalandu kwa asilimia 10.
Wengine
ni Hamisi Kigwangala kwa asilimia saba, Deo Filikunjombe kwa asilimia
tano, Esther Bulaya kwa asilimia 2 na waliosema hakuna anayefaa walikuwa
asilimia 9 na asilimia 13 walipendekeza wengine wasio vijana.
Utafiti
huo pia unaonesha kwamba kijana anayepewa nafasi kubwa endapo
atasimamishwa kupitia upinzani anayeongoza ni Zitto Kabwe kwa asilimia
18, James Mbatia kwa asilimia 16, Tundu Lissu kwa asilimia 14, Halima
Mdee kwa asilimia nne na David Kafulila kwa asilimia sita.
Wengine
ni Julius Mtatiro kwa asilimia nne, John Mnyika kwa asilimia saba,
Joshua Nassari kwa asilimia mbili, Moses Machali kwa asilimia nne na
asilimia 11 ya wananchi walisema hawajui na asilimia 16 walisema hawaoni
anayefaa.
Hata
hivyo, utafiti huo ulionesha kwamba endapo wakishindanishwa vijana wote
bila kujali itikadi zao anayeongoza kwa kukubalika ni Mwigulu Nchemba
kwa asilimia 27, Zitto Kabwe kwa asilimia 19, January Makamba kwa
asilimia 14, James Mbatia kwa asilimia 11 na Emmanuel Nchimbi kwa
asilimia nane.
Wengine
ni Lazaro Nyalandu kwa asilimia saba, Tundu Lissu kwa asilimia tano,
Hamis Kigwangala kwa asilimia nne, wengine waliotajwa wasio vijana ni
asilimia nne na wasiofaa walikuwa ni asilimia mbili.
Mapema
Mkurugenzi wa Mafunzo wa Utafiti wa TEDRO, Jackson Coy alisema utafiti
huo wameufanya bila shinikizo kutoka kwa mtu yeyote na waliufanya kuhusu
siasa kutokana na kwamba mwaka huu utafanyika uchaguzi mkuu.
Alisema
lengo la utafiti huo limechambua ushiriki wa vijana katika siasa kama
wagombea, mchango wa wanasiasa vijana katika kufuatia misingi ya utawala
bora na uwajibikaji, utekelezaji wa ahadi za wagombea kwa wapiga kura
na matarajio ya wananchi kwa vijana katika kuelekea uchaguzi mkuu.
“Utafiti
tunaoendesha ni mwendelezo wa uchambuzi wa changamoto za elimu, ndani ya
dira ya TEDRO na programu ya mchango wa elimu katika kufungua fursa za
ajira, siasa ikiwa ni mojawapo ya fursa zenye kimbilio la vijana,”
alisema.
Hadi sasa
TEDRO inaendesha utafiti wa Mitandao ya Kijamii inavyoathiri wanafunzi
wa sekondari na kutazama njia rafiki katika kutumia mitandao hiyo kama
njia ya kujifunzia na kuendeleza sekta nzima ya elimu.
Utafiti
huu uliotarajiwa kuhusisha wilaya 24 Tanzania Bara, umeendeshwa katika
wilaya 18, kila wilaya ikiwa imewakilishwa na wahojiwa 45 waliochaguliwa
15 kutoka kila kijiji; hivyo utafiti huu kuhusisha vijiji 54 kwa
ujumla.
Wilaya
ambapo utafiti umefanyika ni Njombe Mjini, Ludewa, Mbeya Mjini, Kilwa,
Lindi Mjini, Mtwara Mjini, Morogoro Mjini, Kisarawe, Kinondoni, Tanga
Mjini, Vunjo, Arumeru, Singida, Kasulu, Kigoma Mjini, Bukoba Vijijini,
Biharamulo na Mwanza Mjini (Nyamagana).
Katika
utafiti huu uliohusisha watu 910, taarifa binafsi za wahojiwa
zilizokusanywa ni pamoja na zile zinazohusu umri wa wahojiwa, jinsia,
hali ya ndoa, kazi, kiwango cha elimu na vyama vya siasa vinavyoongoza
majimbo sehemu uchaguzi ulipofanyika.
Lakini
wakati matokeo hayo ya utafiti yakianikwa, kwa upande wa CCM, Rais
Jakaya Kikwete hivi karibuni akiwa mjini Songea, Ruvuma alikokuwa mgeni
rasmi katika maadhimisho ya miaka 38 ya chama hicho, alisema chama chake
bado hakina mgombea mpaka sasa.
Aidha,
alitumia fursa hiyo kuwataka Watanzania kuwashawishi wanaoonekana kuwa
na uwezo wa kuongoza huku wakiwa hawana ‘madoa’ waweze kujitosa katika
uchaguzi mkuu wa baadaye mwaka huu.CHANZO:HABARI LEO
No comments:
Post a Comment