Buzwagi Kusitisha Uchimbaji wa Dhahabu
Kampuni ya Acacia inayomiliki mgodi wa dhahabu wa Buzwagi mkoani Shinyanga, imesema ndani ya miaka miwili, itasitisha shughuli za uchimbaji na uzalishaji madini hayo, kutokana na soko kuzidi kushuka.
Meneja
Mkuu wa mgodi huo, Filbert Rweyemamu alisema hayo juzi katika kikao
cha pamoja baina ya mgodi na wajumbe wa Kamati ya Kijiji cha Mwime,
iliyoundwa na uongozi wa mtaa wa Mwime kwa ajili ya kusainiana mkataba
wa shughuli za maendeleo.
Rweyemamu
alisema shughuli za uzalishaji na uendeshaji ni tofauti na mauzo, hivyo
kampuni inazidi kutumia gharama kubwa za uendeshaji.
“Kutokana
na mgodi kusitisha shughuli za uzalishaji ndani ya miaka miwili ijayo;
siyo kwamba dhahabu zimeisha dhahabu ni nyingi mno, isipokuwa
tunashindwa kumudu gharama za uzalishaji wilaya ya Kahama ina dhahabu
tangu hatujaingia, makampuni mengi yalichimba na kuondoka na sisi
tunaondoka”, alisema meneja huyo.
Bei
ya dhahabu kwa mwaka 2014, imekuwa chini ya dola 1,300 kwa ounce moja
kwa muda mrefu. Kufikia Novemba, bei ilikuwa 1,129 kwa ounce moja, hali
ambayo imeleta mtikisiko wa uendeshaji wa kampuni za uchimbaji wa
dhahabu.
Katika
kikao hicho ambacho madhumuni yake ilikuwa ni usainishwaji wa rasimu
ya mkataba wa shughuli za maendeleo baina ya Kampuni ya Acacia na
Serikali ya Kijiji cha Mwime, kilicho jirani na mgodi, shughuli hiyo
ilishindikana kufanyika.
Baada
ya kujadili upya, walibaini baadhi ya miradi ya vyoo vitano
vinavyogharimu Sh milioni 51 na visima vitano vinavyogharimu Sh milioni
140, havikuwemo katika rasimu hiyo, hali iliyopingwa na Meneja wa mgodi.
Katika
mkutano huo Meneja Mkuu wa mgodi huo , Rweyemamu aliwaeleza wajumbe wa
Kamati kwamba hawawezi kuanza kuijadili rasimu hiyo kwa kuwa wao kama
mgodi, rasimu hiyo waliipeleka kwa Mwanasheria wa Halmashauri ya Mji wa
Kahama na kuidhinishwa na Mkurugenzi wa Mji huo, Felix Kimaryo.
Alisema
ni muda mrefu tangu wairudishe rasimu hiyo kwa Ofisa Mtendaji ili
Kamati ijadili, kama kuna upungufu wawasiliane na uongozi wa mgodi.
“Ndugu
wajumbe wa Kamati hii ni kwamba mkutano huu ulikuwa ni wa kusaini
rasimu hii ya mkataba, sasa naona mnasema rasimu hii vyoo na visima
havimo, sisi kama mgodi tumekuja kusaini siyo kujadili tena, kazi hiyo
tuliwaachia nyie maana sisi rasimu hiyo tuliipeleka kwa Mwanasheria wa
Halmashauri na ikapitishwa na Mkurugenzi wa Mji,” alisema Meneja Mkuu huyo.
Alisema, “Mnataka
visima gani? Maana tayari tumechimba visima vitano kwa kata nzima ya
Mwendakulima vyenye thamani ya Shilingi milioni 140 , tumejenga vyoo
katika shule za msingi Mwime thamani vya Sh milioni 51, tumeweza
kujenga zahanati kijiji cha Mwime ikiwa lengo la mgodi ni kuweka
mahusiano mazuri kwa wananchi wanaozunguka mgodi,” alisema.
Rweyemamu
alisema kuwa Kampuni ya Acacia kupitia Mgodi wake wa Buzwagi, iliweka
vipaumbele katika mambo mbalimbali ya maendeleo kwenye mtaa huo, lakini
viongozi ndiyo wanakwamisha.
Aliwataka viongozi kujipanga upya huku wakiwa wameweka upungufu wote na wao kama mgodi, watakubali kusaini makubaliano hayo.
Mmoja
wa wajumbe wa rasimu ya mkataba huo, Mayala Makoye alieleza kwamba
wananchi wa mtaa wa Mwime, wanashindwa kufaidika na matunda ya mgodi
huo, kutokana na uongozi wa kijiji hicho kufanya mambo kwa maslahi yao
binafsi, hali inayosababisha wauchukie mgodi na kutamani ufungwe haraka.
No comments:
Post a Comment