Yanga SC yanasa straika aliyewaumbua Zamalek
YANGA iko
kwenye harakati za karibu sana za kumshawishi straika wa Uganda na AS
Vital ya DR Congo, Yunus Sentamu atue Jangwani na wakimpata wana imani
kwamba watakuwa wamemaliza kazi na tatizo sugu kwenye fowadi yao.
Mchezaji
huyo mwenye miaka 20 ndiye mchezaji aliyefunga bao pekee la AS Vital
lililoing'oa Zamalek ya Misri jijini Alexandria kwenye mechi ya kufuzu
nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kuwaacha Waarabu wengi midomo
wazi.
Sentamu
pia alifunga moja kati ya mabao mawili walipocheza na CS Sfaxien na
kufuzu fainali ya Ligi ya mabingwa Afrika hivikaribuni. Ni miongoni mwa
wachezaji wanaothaminiwa sana kwa sasa nchini Uganda kiasi cha kufanya
kocha wa nchi hiyo, Sredejovic Milutin 'Micho' awasahau Hamis Kiiza wa
Yanga na Emmanuel Okwi wa Simba.
Yanga
imeanza kupambana kimyakimya kumpata straika huyo hata kabla ya Kocha
Marcio Maximo kusitisha mkataba wa Mbrazil Geilson Santos 'Jaja' na
kutangaza kumleta kiungo mkabaji Emerson Rouqe wa Brazil.(P.T)
Straika
huyo wa AS Vita yupo katika orodha ya CAF ya wachezaji wanaowania tuzo
ya uchezaji bora Afrika kwa upande wa wachezaji wanaocheza ndani.
Habari za
ndani ya kamati ya Usajili ya Yanga, zinasema Sentamu ni kati ya
washambuliaji wanaotakiwa sana ili kuwa na straika mmoja mkali wa Afrika
ambaye ni mtu wa kazi na mwenye uzoefu kuliko kujaribujaribu na kuingia
hasara kila mara.
"Viongozi
wanafanya kazi ya kutafuta straika wa maana mwenye uwezo wa kufunga ili
kuonyesha kwamba bado Afrika ina wachezaji wazuri tofauti na fikra za
kocha (Marcio Maximo)," alidokeza kiongozi huyo na kuongeza kwamba
endapo huyo akitua huenda safari ikamkumba Hamis Kiiza au wakaachana na
Emerson anayekuja nchini kesho Jumanne na Maximo.
Si Yanga
pekee wanamtaka mchezaji huyo kwani CS Sfaxien ya Tunisia nao wameingia
kwenye kinyang'anyiro lakini Yanga wamegundua kwamba mchezaji huyo
ameambiwa kwamba Tanzania kuna fedha na anataka kucheza karibu na
nyumbani.
Awali
wakati ishu ya Sentamu inaanza, Yanga kulikuwa na malumbano kwenye
kamati ya usajili kwani baadhi ya viongozi wanataka kusajili mchezaji
kutoka nje ya ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kutokana na usumbufu
wanaoupata kutoka kwao mara kwa mara na kwamba wengi wao wana viwango
vinavyofanana na wachezaji wa Tanzania.
Bado
Yanga ipo katika kuhakikisha pia inamnasa kiungo mshambuliaji wa Mbeya
City, Deus Kaseke ambaye amerudi Mbeya baada ya kutokamilika kwa
mazungumzo ya kwanza jijini Dar es Salaam wiki iliyopita.
Ili
Sentamu asajiliwe katika kikosi cha Yanga, ni wazi klabu hiyo itabidi
iachane na mmoja wa wachezaji wake wa kigeni kati ya Hamis Kiiza
(Uganda), Haruna Niyonzima au Mbuyu Twite wote wa Rwanda lakini Kiiza
ndiye yupo katika wakati mgumu kwani tayari Maximo anaonekana hamhitaji
kikosini mwake.
Chanzo:Mwanaspoti
No comments:
Post a Comment