Mabilioni escrow mali ya umma
Mwenyekiti wa Kamati ya PAC, Zitto Kabwe
Ripoti ya
sakata la uchotaji wa Dola za Marekani 200 milioni katika akaunti ya
Tegeta Escrow iliyotua bungeni wiki iliyopita, imeibua mambo mazito
baada ya Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)
kugundua kuwa fedha zilizochotwa kwenye akaunti hiyo zilikuwa mali ya
Tanesco.
Taarifa
kutoka vyanzo mbalimbali zinaeleza kuwa fedha zilizokuwa kwenye akaunti
hiyo ni Sh306 bilioni wakati madai ya Tanesco kwa IPTL ni Sh321 bilioni,
hivyo fedha zote za Escrow zilipaswa kwenda Tanesco na bado ingekuwa
inadai.
Ukaguzi
wa akaunti hiyo uliamuliwa na Serikali baada ya Mbunge wa Kigoma Kusini
(NCCR-Mageuzi), David Kafulila kudai kuna ufisadi katika uchotaji wa
fedha hizo katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Akaunti
hiyo ilifunguliwa baada ya kutokea mgogoro wa kibiashara baina ya
Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na Kampuni ya kufua umeme ya IPTL.
Katika
mgogoro huo, Tanesco ilikuwa inabishia kiwango cha fedha ilichokuwa
inalipa kwa gharama za uwekezaji kwa IPTL, ndipo ikaamuliwa na mahakama
ifunguliwe akaunti hiyo ili fedha ilizokuwa inalipa ziendelee kuwekwa
huko hadi mgogoro utakapokwisha.
Kesi hiyo iliamuliwa katika mazingira yanayoelezwa kuwa na utata na fedha hizo kuchukuliwa haraka na IPTL.(P.T)
Baada ya
ripoti ya uchunguzi huo kukabidhiwa bungeni wiki iliyopita chanzo chetu
kimeeleza kuwa kwa mujibu wa ripoti hiyo fedha ni za umma na zilipaswa
kwenda Tanesco na shirika hilo kuendelea kuidai IPTL Sh15 bilioni.
Taarifa
zaidi zinaeleza kuwa Kampuni ya PAP haikununua kihalali asilimia 70 ya
hisa za Kampuni ya Mechmar katika IPTL kwani zilizuiliwa na mahakama,
hivyo hawana hati halisi ya hisa na kwamba ilifanya udanganyifu katika
malipo ya kodi kwa kutoa nyaraka za uongo kuwa walinunua hisa kwa Sh6
milioni badala ya Dola za Marekani 20 milioni, hivyo kuikosesha Serikali
Sh8.7 bilioni.
Pia
imeeleza kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali alivunja sheria kwa kuelekeza
kuwa kodi ya ongezeko la thamani kwenye gharama za uwekezaji isilipwe
na hivyo kusababisha Serikali kupoteza mapato ya Sh21 bilioni.
"Wizara
ya Nishati na Madini haikufanya uchunguzi wa awali (due diligence)
kuhusu uhalali wa umiliki wa Kampuni ya IPTL na ilisaini kutoa fedha
bila ya kuhakikisha fedha za Tanesco zinarudi na hivyo kusababisha
kulipotezea Shirika zaidi ya Sh321 bilioni," chanzo chetu kilieleza.
Hata
hivyo, Naibu Spika, Job Ndugai alipoulizwa juzi baada ya kutoka kwenye
Kamati ya Uongozi, bila kufafanua alisema ripoti itawasilishwa bungeni
Novemba 26, mwaka huu kama ilivyopangwa na kuwa angetoa taarifa ya
kilichojiri kwenye Kamati ya Uongozi bungeni leo.
Baadhi ya
wajumbe wa Kamati ya Uongozi wameeleza kuwa, wamekubaliana ripoti hiyo
iwasilishwe kama ilivyopangwa na kwamba muda huu ofisi ya Katibu wa
Bunge na Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) waipitie kwa ajili ya
uwasilishwaji.
Mwenyekiti
wa Kamati ya PAC, Zitto Kabwe ambaye ameshakabidhiwa ripoti hiyo
alipoulizwa alisema bado anaipitia ripoti hiyo kwa kuwa ina kurasa zaidi
ya 300.
"Namshukuru
sana CAG kwa kumaliza kazi hii na kujibu hadidu za rejea zote. Ni
taarifa kubwa yenye zaidi ya kurasa 300," alisema Zitto.
Hadidu za rejea
Katika
uchunguzi huo, CAG alipewa hadidu za rejea za kuchunguza uendeshaji wa
mkataba wa kuzalisha umeme kati ya Kampuni ya IPTL na Tanesco, pia
kuchunguza kama wakati escrow inafunguliwa Kampuni ya Mechmar ilikuwa
inamiliki IPTL, kama ilikuwa imefilisiwa au iwapo ilikuwa imehamisha
umiliki wake kwa Kampuni ya PAP.
Vilevile
kuchunguza na kuthibitisha ushahidi wa Kampuni ya PAP kununua Kampuni ya
Mechmar na kumiliki IPTL na chanzo cha mgogoro kuhusu tozo kati ya
Tanesco na IPTL na kuthibitisha ushahidi wowote kuwa mgogoro uliamuliwa
kwa faida ya IPTL.
Lingine
ilikuwa ni kuchunguza iwapo ilikuwa sahihi kwa Mwanasheria Mkuu wa
Serikali kusamehe kodi ya VAT ya jumla ya Sh26 bilioni kutokana na tozo
ya capacity charges na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), wachukue hatua
gani kuhakikisha kodi hiyo inakusanywa.
Pia
kuchunguza kiwango cha fedha kilichopaswa kuwamo katika akaunti ya
escrow, kiwango gani kilikuwapo wakati IPTL wanalipwa na kiwango gani
kitapaswa kulipwa zaidi kutoka Tanesco.
Vilevile
kuchunguza madai ya Benki ya Standard Chartered kwa Tanesco na madai
mengine yoyote yanayohusiana na mkataba wa kuzalisha Umeme wa IPTL na
iwapo Serikali imejihadhari na uwezekano wa madai yanayoweza
kufunguliwa, nafasi na heshima ya nchi katika kuheshimu mikataba ya
kimataifa na ya uwekezaji.
Pia
alitakiwa kuchunguza iwapo Wizara ya Nishati na Madini ambayo ni mhusika
mkuu wa akaunti ya escrow ilifanya 'due diligence' ya kutosha kabla ya
kuingia makubaliano ya kutoa fedha zilizopo kwenye akaunti.
Kutoa
mapendekezo ya njia bora za kisheria kulinda Taifa kutoingia hasara
zaidi katika mkataba wa IPTL chini ya wamiliki wapya na kutoa ushauri
kwa kamati ya PAC juu ya mapendekezo ya hatua ambazo Bunge linapaswa
kuchukua kuhusu matokeo ya ukaguzi huu maalumu.
Chanzo:Mwananchi
No comments:
Post a Comment