Ujerumani haioni matumaini katika mzozo wa Ukraine
Frank Walter Steinmeier (kushoto) na Sergei Lavrov mjini Moscow
Waziri wa
mashauri ya kigeni wa Ujerumani Frank Walter Steinmeier alisema Jumanne
(18.11.2014) haoni sababu za kuwa na matumaini kuhusu mzozo unaoendelea
Ukraine kutokana na machafuko kuongezeka mashariki mwa nchi hiyo.
Katika
mkutano na waandishi wa habari pamoja na waziri wa mambo ya kigeni wa
Urusi Sergei Lavrov hapo jana, Steinmeir alionya kuhusu hali ya kutisha
inayoendelea nchini Ukraine. Alizitolea mwito pande zote zinazohusika
katika mzozo wa Ukraine kuuheshimu mkataba wa makubaliano uliofikiwa
katika mkutano wa mjini Minsk nchini Belarus uliofanyika Septemba 5
mwaka huu ambao kwa kiwango kikubwa unaonekana kusuasua.(P.T)
Steinmeier
alisema itakuwa hasara kubwa kuachana na mkataba huo ambao umefaulu
kusitisha mapigano mengi, lakini umeshindwa kuepusha kuzuka machafuko ya
hapa na pale katika maeneo muhimu. "Hata kama tuna shaka kama mkataba
unafanya kazi katika kila kipengele, hata kama tutaripoti vipengele
muhimu vimekiukwa katika wiki zilizopita, itakuwa hasara kubwa kuukataa
mkataba huu. Lazima tufanye juhudi kujaribu kutafuta kilichokwenda kombo
baada ya mkataba kusainiwa ili tuendeleze kazi ya kuvitekeleza
vipengele hivyo."
Steinmeier
alikwenda Moscow akitokea Kiev ambako alikutana na waziri mkuu wa
Ukraine Arseniy Yatsenyuk. Mwanadiplomasia huyo wa Ujerumani alitaka kwa
haraka kuwekwe eneo lisiloruhusiwa mapigano kati ya majeshi ya serikali
ya Ukraine na waasi wanaoegemea Urusi mashariki mwa Ukraine kuuokoa
mkataba wa makubaliano ya kusitisha mapigano.
Waziri wa
mambo ya kigeni wa Urusi Sergei Lavrov aliunga mkono mwito wa
Steinmeier na kusisitiza umuhimu wa kuutekeleza kikamilifu mkataba wa
Minsk. "Lengo kuu ni kuzuia mzozo wa kijeshi kusini mashariki mwa
Ukraine, kuweka eneo la kuzitenganisha pande mbili na kuondoa silaha
nzito. Lakini tutatafakari njia za kuleta uthabiti wa muda mrefu Ukraine
bila kusahau umoja wa taifa, maelewano na maridhiano. Na hatupaswi
kuyasahau mageuzi ya katiba yaliyosainiwa na Ukraine mjini Geneva Aprili
17."
Misimamo tofauti yajitokeza
Tofauti
zilijitokeza kati ya Steinmeier na Lavrov katika mkutano na waandishi wa
habari huku wote wakionekana kutotulia mara kadhaa. Ingawa viongozi
wote walisisitiza umuhimu wa mkataba wa Minsk, Lavrov alisema mdahalo
kati ya pande zinazohasimiana Ukraine unapaswa kuzingatia uchaguzi wa
Novemba 2 ulioandaliwa na waasi katika maeneo wanayoyadhibiti katika
hatua ya kukaidi uchaguzi wa bunge uliofanyika siku chache kabla.
Lavrov
alisema hakuna mbadala wa ushirikiano kati ya Urusi na Umoja wa Ulaya
akiongeza kuwa Urusi haipaswi kulaumiwa kwa mahusiano mabovu na umoja
huo kwa sababu ya mzozo wa Ukraine.
Steinmeier
alikutana pia na rais wa Urusi, Vladimir Putin, lakini ikulu ya Kremlin
haikutoa maelezo yoyote kuhusu mazungumzo kati ya viongozi hao. Waziri
Steinmeier ni kiongozi wa kwanza wa ngazi ya juu kutoka Ulaya kuzuru
Moscow tangu mwezi Julai mwaka huu, katika ishara inayoonyesha namna
gani uhusiano kati ya mataifa ya magharibi na Urusi ulivyovurugika tangu
kumalizika kwa vita baridi kutokana na mzozo mashariki mwa Ukraine.
Mwandishi:Josephat Charo/AFPE/RTRE
Mhariri:Daniel Gakuba
Chanzo:DW
No comments:
Post a Comment