TIFFAN ENT

TIFFAN ENT

TUKO WANGAPI

TUKO WANGAPI

GLORY FREIGHT

GLORY FREIGHT

Friday, November 15, 2013

UGONJWA WA KISUKARI WAENDELEA KULETA MADHARA

AFYA_-_1_39429.jpg

Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Hussein Mwinyi (kushoto) akitoa tamko la Serikali kuhusu Siku ya Ugonjwa wa Kisukari Duniani inayoadhimishwa kila mwaka Novemba 14. Kulia ni Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt.Seif Rashid.
AFYA_-2_ef5f9.jpg
Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Donan Mmbando akitoa ufafanuzi wa namna ya kujikinga na ugonjwa wa kisukari leo jijini Dar es salaam wakati mkutano na waandishi wa habari.
Picha na Aron Msigwa - MAELEZO.(P.T)
UGONJWA WA WAENDELEA KULETA MADHARA , WATANZANIA WATAKIWA KUJENGA TABIA YA KUPIMA AFYA NA KUFANYA MAZOEZI.
Na. Aron Msigwa –MAELEZO.
14/11/2013 – Dar es salaam.
Watanzania wametakiwa kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi mara kwa mara, kupima afya na kuepuka tabia hatarishi zinazochangia uwezekano wa kupata ugonjwa wa kisukari.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es salaam na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Hussein Mwinyi wakati akitoa tamko la Serikali kuhusu Siku ya Ugonjwa wa Kisukari Duniani inayoadhimishwa kila mwaka Novemba 14.
Amesema Tanzania kama zilivyo nchi nyingine inaadhimisha siku hiyo kwa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa kushirikiana na Chama cha Ugonjwa wa kisukari Tanzania kutoa elimu ya umuhimu wa kuzuia na kujikinga na madhra mbalimbali yatokanayo na ugonjwa huo.
Amesema maadhimisho ya Siku ya Kisukari Duniani 2013 yataongozwa na kauli mbiu isemayo "Linda Maisha yajayo dhidi ya Ugonjwa kisukari" inayolenga kuhamasisha jamii juu ya matatizo mbalimbali yanayotokana na ugonjwa wa kisukari katika jamii.
Ameeleza kuwa athari za ugonjwa wa kisukari katika mwili wa binadamu hutokea wakati sukari katika damu inapokuwa nyingi kupita kiwango cha kawaida kwa muda mrefu na kuongeza kuwa tafiti zinaonyesha kuwa mwaka 2007 kulikua na wagonjwa milioni 246 duniani huku mwaka 2012 kukiwa na wagonjwa milioni 371 ambapo nusu ya idadi ya wagonjwa hao walikua hawajaanza kupata matibabu.
Kuhusu dalili za ugonjwa huo Dkt. Mwinyi amesema kuwa ni rahisi kuzitambua na huambatana na mgonjwa kuwa na kiu isiyoisha, kukojoa mara kwa mara, kupungua uzito, kusikia njaa kila wakati na mwili kukosa nguvu na kuongeza kuwa athari za ugonjwa huo ni kubwa kutokana na ugonjwa huo kuharibu mishipa ya damu na fahamu, macho, figo, kusababisha upofu, moyo na figo kushindwa kufanya kazi na miguu kufa nganzi na kuwa na vidonda.
Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa asilimia 80 ya wagonjwa wote duniani wanaishi katika nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania na kuongeza kuwa utafiti uliofanyika mwaka 2012 nchini Tanzania kwa kuzihusisha wilaya 50 unaonyesha kuwa asilimia 9.1 ya watanzania wenye umri wa miaka 25 na kuendelea wana ugonjwa wa kisukari.
"Ni jambo lililo wazi kuwa lazima tubadili tabia hasa tabia hatarishi zinazochangia ugonjwa wa kisukari zikiwemo unywaji wa pombe kupita kiasi, ulaji usiofaa, ulaji usiofaa na tabia ya kupuuza kufanya mazoezi", sasa Tanzania katika nchi 10 za Afrika zinazoongoza kwa kisukari barani Afrika inashika nafasi ya 8" Amesema Dkt. Mwinyi.
Kuhusu sababu zinazochangia ugonjwa huo Dkt. Mwinyi amesema kuwa ni pamoja na tabia ya ulaji usiofaa hasa matumizi ya chumvi kwa wingi , mafuta na sukari, uzito uliozidi, unene uliokithiri, kutofanya mazoezi , uvutaji wa sigara na bidhaa zitokanazo na tumbaku pamoja, kula vyakula vyenye mafuta mengi hasa yatokanayo na wanyama, sukari nyingi,kula chakula kupita kiasi, kukoboa nafaka, kutokula mbogamboga na matunda na unywaji wa pombe kupita kiasi.
Ameeleza kuwa jamii inapaswa kuepuka mambo yanayochangia chakula kilicholiwa kutotumika vizuri ikiwemo tabia ya kukaa muda mrefu bila kufanya mazoezi huku akisisitiza kuwa unywaji wa pombe kupita kiasi huharibu maini na kusababisha utapiamlo kwa wale wanaoishia kunywa pombe Zaidi bila kula chakula.
" Natoa ushauri hasa kwa watumishi kuepuka kuketi ofisini, darasani au kuangalia runinga kwa muda mrefu na hata kutumia lifti kwenda ghorofani badala ya ngazi na matumizi ya magari katika umbali mfupi unaoweza kufikika kwa kutembea tu"
Dkt. Mwinyi ameleza kuwa serikali imejipanga kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazotokana na ugonjwa huo na kusisitiza kuwa utekelezaji wa Sera ya Afya ya mwaka 2007 unaendelea kwa kuhakikisha kuwa utoaji wa hudunma za magonjwa yasiyo ya kuambukiza ikiwemo kisukari unafanyika kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Ameeleza kuwa serikali kwa kutambua gharama za kutibu ugonjwa wa kisukari kuanzia mwaka 1983 ilitoa msamaha wa matibabu kwa wagonjwa wote wa kisukari kutochangia gharama za matibabu pia kuhakikisha kuwa dawa muhimu zinapatikana katika kliniki mbalimbali zilizopo nchini.
Kwa upande wake Mganga mkuu wa Serikali Dkt. Donan Mmbando amewataka vijana kote nchini ambao ni kundi kubwa kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi mara kwa mara na kuepuka maisha ya anasa ambayo huwaweka katika hatari kubwa ya kupata ugonjwa wa kisukari.
Amesema mapambano ya ugonjwa wa kisukari yanahitaji ushiriki wa kila mwananchi hasa kuzingatia kanuni za Afya na kujenga mazoea ya kufanya mazoezi mara mara.
MWISHO.

No comments:

Post a Comment