TIFFAN ENT

TIFFAN ENT

TUKO WANGAPI

TUKO WANGAPI

GLORY FREIGHT

GLORY FREIGHT

Wednesday, November 6, 2013

MWAPACHU:NIMECHOSHWA NA MIGOGORO EAC

mwapachu20juma1 4b5ca
KATIBU Mkuu mstaafu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Balozi Juma Mwapachu, amesema migogoro inayoendelea ndani ya jumuiya hiyo imemchosha. Balozi Mwapachu alisema hayo jana, alipotakiwa na RAI kutoa ufafanuzi wake juu ya mgogoro unaofukuta ndani ya jumuiya hiyo, uliosababishwa na viongozi wa nchi za Rwanda, Kenya na Uganda. (HM)

Viongozi wa nchi hizo, akiwamo Yoweri Museveni (Uganda), Paul Kagame (Rwanda) na Uhuru Kenyetta wa Kenya, wanadaiwa kuanzisha umoja wa hiari, huku wakifanya vikao vya siri na kuitenga Tanzania.
Akizungumzia hali hiyo, Balozi Mwapachu alisema amewahi kuandika mambo mbalimbali juu ya EAC na dalili za kutokea migogoro inayotokea sasa, lakini hakuna hatua zilizochukuliwa za kudhibiti.
Hata hivyo, Mwapachu hakuweza kueleza ni mahali gani alitoa ushauri upi kuhusu jumuiya hiyo, zaidi ya kusisitiza kuwa amechoshwa na migogoro ya chombo hicho.
"Niseme nini mimi, sina la kuzungumza, nimeshaandika sana, nimeshauri sana, na sasa nimechoka, siwezi tena kusema lolote," alisema Balozi Mwapachu, bila kufafanua zaidi na baadaye kukata simu.
Wakati Mwapachu akionekana kuchoshwa na kinachotokea ndani ya EAC, dalili za wazi za kuvunjika kwa jumuiya hiyo zimeanza kuonekana.
Kwa muda sasa marais hao wanakutana kuweka mikakati ya siri bila kuzishirikisha nchi za Tanzania na Burundi, ambapo mapema wiki hii, walimwalika Rais wa Sudan Kusini, Silva Kiir, kwenye mkutano wao.
Hali hiyo imeonekana kuwakera wabunge wa Bunge la Tanzania wanaoendelea na kikao chao mjini Dodoma na kushinikiza wapewe ufafanuzi wa kinachoendelea.
Akitoa hoja ndani ya Bunge, Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango, alisema jumuiya hiyo ipo hatarini kuvunjika na kutaka Tanzania isiendelee na shughuli nyingine yoyote inayoihusu jumuiya hiyo, hadi pale hatima yake itakapojulikana.
Mbunge wa Viti Maalumu (CUF), Rukia Ahmed, naye aliitaka serikali kupeleka bungeni pendekezo la kujitoa katika jumuiya hiyo, ili wabunge walipitishe.
Akijibu hoja hizo, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, alisema Tanzania imeanza mazungumzo na nchi za Burundi na Congo DR, kuangalia namna ya kuwa na ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi hizo.
Hata hivyo, Sitta alisema Tanzania haiwezi kuamua lolote kwa sasa, hadi itakapopata taarifa ya kina kuhusu mikutano ya mara kwa mara inayofanywa na viongozi wa nchi tatu za jumuiya hiyo.
Mkutano wa kwanza wa viongozi hao ambao hawakuishirikisha Tanzania, ulifanyika ghafla Entebbe (Uganda), Juni, mwaka huu, ukafuatiwa na mkutano wa Mombasa (Kenya) Agosti 28 na juzi wakuu hao walikutana Kigali, Rwanda.
Akielezea msimamo wa Tanzania kwa wabunge juzi, Waziri Sitta alisema Tanzania haiwezi kupewa talaka katika jumuiya hiyo, kwa kuwa ina eneo la zaidi ya asilimia 52 ya eneo zima la EAC na asilimia 48 iliyobaki nchi nyingine zinagawana.
Hata hivyo, alisema ingawa Kenya, Uganda na Rwanda hawajaanzisha rasmi jumuiya yao, dalili zinaonesha kuwa wapo katika harakati ambazo hatima yake haijulikani.
Kwa muda mrefu sasa, mgogoro unaofukuta ndani ya jumuiya hiyo umewalazimisha wadau mbalimbali wa uchumi na siasa nchini kuitaka serikali kuachana na EAC na kuelekeza nguvu zake zaidi katika Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).Chanzo: mtanzania

No comments:

Post a Comment