Taarifa rasmi ya Zitto Kabwe kuhusu kinachoitwa “Taarifa ya siri ya CHADEMA”

Tamko rasmi la Ndugu Zitto Z. KABWE (MB) kuhusiana na kinachoitwa "Taarifa ya Siri ya CHADEMA"
Ndugu Wanahabari,
NILIPOKUWA katika ziara ya bara la 
Ulaya kati ya Oktoba 21 mpaka Novemba 2 mwaka huu (2013), nilipokea kwa 
njia ya barua pepe ripoti inayoitwa "Taarifa ya Siri ya Chadema" ambayo 
pia ilikuwa imesambazwa katika mitandao mbalimbali ya kijamii.
"Taarifa ya Chadema inasema kwamba chama hicho (chama changu) kilikuwa kimechunguza mwenendo wangu tangu
mwaka 2008 hadi 2010 na kubaini kuwa mimi napokea fedha kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili kuivuruga Chadema.
Ripoti hiyo ilinihusisha pia na 
mwananchi raia wa Ujerumani, Andrea Cordes ambaye, kwa mujibu wa ripoti 
hiyo, alinisaidia kupokea na kuhifadhi kiasi cha dola 250,000 za 
Marekani kupitia kwenye akaunti yake binafsi.(P.T)
Taarifa hii ya kutunga na iliyojaa uongo wa kiwango cha kutisha, imenifadhaisha, kunisikitisha na kunikasirisha.
Taarifa hii iliibuliwa katika kipindi 
ambacho nilikuwa safarini kutetea haki za Watanzania na Waafrika ambao 
utajiri wao wa rasilimali unafaidiwa na watu wachache waliohifadhi mali 
katika nje za nje na pia kupigania makampuni ya mataifa tajiri yalipe 
kodi stahiki katika nchi zetu.
Pengine lengo la ripoti hiyo lilikuwa 
ni kutaka kunipoteza kutoka katika nia na dhamira yangu ya dhati ya 
kutaka Watanzania wafaidike na utajiri wao. Muda ambao watunzi wa ripoti
 hiyo waliamua kutoa taarifa yao unazua maswali mengi kuliko majibu.
Nafahamu kwamba mimi ni mwanasiasa 
ambaye nimekuwa mlengwa (target) wa mashambulizi kutoka kwa makundi 
mbalimbali ya wanasiasa na vikundi vyao. Kama mwanasiasa, niko tayari 
kupokea changamoto zozote zinazokuja na uanasiasa wangu.
Hata hivyo, ambacho sitakubali ni kwa watu kutumia jina langu na uanasiasa wangu kunichafua mimi binafsi na watu wengine wasiohusika kwa sababu ya kutaka kutimiza malengo yao ya kidhalimu.
Hata hivyo, ambacho sitakubali ni kwa watu kutumia jina langu na uanasiasa wangu kunichafua mimi binafsi na watu wengine wasiohusika kwa sababu ya kutaka kutimiza malengo yao ya kidhalimu.
Raia huyo wa Kijerumani tayari amekana
 kuhifadhi fedha zangu. Kwa maelezo yake kwa baadhi ya viongozi wa 
Chadema amekana kuwa na akaunti inayotajwa na amekana pia kuwepo nchini 
Ujerumani katika siku na wakati uliotajwa kwenye ripoti hiyo.
Ripoti hiyo imemtaja pia mtu kama Dk. 
Charles Kimei, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB ikidai kwamba 
nilikutana naye na alishiriki kwenye igizo hilo la kunipa fedha.
Niseme mapema kwamba tangu kuzaliwa 
kwangu sijawahi hata mara moja kukutana na Dk. Kimei popote pale ndani 
au nje ya nchi. Kumuingiza mtu ambaye amejenga jina lake kwenye taaluma 
ya kibenki kwa sababu tu ya lengo ovu la kumchafua Zitto Zuberi Kabwe si
 uungwana bali ni unyama.
Kutokana na uchafuzi huu wa wazi dhidi
 ya taswira yangu binafsi na watu wengine walioingizwa kwenye mkumbo 
huu, nimeandika rasmi kwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk.Wilbrod Slaa 
kumwomba athibitishe kwamba kinachoitwa Taarifa ya Siri ya Chadema ni 
kweli ni taarifa ya chama au kiikanushe ili niweze kuchukua hatua za 
kisheria dhidi ya waandishi wa hekaya hiyo.
Cha ajabu, nimepokea ujumbe wa 
kutishiwa maisha kutoka kwa mtu anayejiita Theo Mutahaba na kuahidiwa 
KUPOTEZWA endapo nitaendelea na jitihada zangu za kupambana na ufisadi 
na kutafuta haki kwa Watanzania wote pasipo kujali tofauti zao za 
kiitikadi, kikanda, kikabila na kidini.
Natarajia kuchukua hatua kali za 
kisheria dhidi ya wote ambao wamehusika na utungaji na uenezi wa taarifa
 hii. Nitahakikisha kwamba wahusika wanatafutwa na kufunguliwa mashitaka
 stahiki ya upotoshaji na kuchafuana.
Ni matarajio yangu kwamba wale wenye 
mapenzi mema na Tanzania, mimi binafsi na utawala wa sheria, wataelewa 
nia yangu ya kutafuta haki katika suala hili.
Nimeamua kujitolea maisha yangu kwa 
ajili ya Watanzania na kama alivyopata kusema Rais Mstaafu wa Afrika 
Kusini, Nelson Mandela; "Struggle Is My Life."
Forward Ever, Backward Never- Kwame Nkrumah
Zitto Kabwe (Mb)
10/11/2013
10/11/2013
No comments:
Post a Comment