HAWA NDIO MABILIONEA WANNE VINARA TANZANIA
Mfanyabiashara maarufu nchini, Rostam Aziz (49), ametajwa kuwa ndiye tajiri namba moja Tanzania kwa sasa.
Kwa
mujibu wa utafiti uliofanywa na Jarida la Marekani la Forbes na kutoa
taarifa yake juzi, Rostam amekamata nafasi hiyo na ya 27 katika Afrika
akiwa na utajiri wa Dola za Marekani bilioni moja Sh1.6 trilioni.(HD)
Mbunge
huyo wa zamani wa Igunga, ameingia kwa mara ya kwanza katika orodha ya
matajiri 50 wa Afrika ya jarida hilo, pamoja na wafanyabiashara wengine
wa Tanzania, Reginald Mengi na Mbunge wa Singida Mjini (CCM), Mohamed
Dewji 'Mo'. Katika orodha hiyo pia yumo Said Bakhresa ambaye aliwahi
kutajwa siku za nyuma.
Rostam,
ambaye aliachana na siasa mwaka 2011, amempiku Bakhresa, ambaye mwaka
jana Jarida la Ventures Africa la Nigeria lilimtaja kuwa ndiye aliyekuwa
tajiri namba moja wa Tanzania. Bakhressa katika kipindi hicho
alikadiriwa kuwa na utajiri wa Dola 620 milioni (Sh971 bilioni).
Katika orodha hiyo ya Ventures Africa, Bakhresa alifuatiwa na Rostam, Mengi na mfanyabiashara mwingine maarufu, Ali Mufuruki.
Mengi anashika nafasi ya pili kwa Tanzania na ya 34 Afrika akiwa na utajiri wa Dola 550 milioni (Sh861 bilioni).
Forbes
linaonyesha kuwa Bakhresa amefungana na Mo katika nafasi ya tatu ya
orodha ya matajiri wa Tanzania na ya 38 kwa Afrika, wote wakiwa na
utajiri wa Dola 500 milioni (Sh783 bilioni).
Rostam,
Mengi na Bakhresa hawakupatikana jana kuzungumzia suala hilo huku Mo
akisema kwamba asingeweza kuzungumzia suala hilo kwa kuwa jana alikuwa
katika mapumziko ya Sikukuu ya Ashura.
Tajiri wa
Nigeria, Aliko Dangote, ambaye anajenga Kiwanda cha Saruji huko Mtwara
ndiye anayeshika nafasi ya kwanza katika orodha ya Afrika, akiwa na
utajiri wa Dola20 bilioni (Sh31.7 trilioni), akifuatiwa na familia ya
Johanny Rupert ya Afrika Kusini yenye utajiri wa Dola7 bilioni (Sh10.7
trilioni) na Nick Oppenheimer, pia wa Afrika Kusini mwenye utajiri wa
Dola 6.6 bilioni (Sh10.3 trilioni).
1)Rostam Aziz
Jarida la
Forbes limeripoti kuwa utajiri wa Rostam unachangiwa zaidi na biashara
ya mawasiliano ya simu za mkononi, ujenzi na uchimbaji wa madini.Pia
anamiliki Kampuni ya Caspian, ambayo inafanya kazi za kuchimba madini
katika migodi inayomilikiwa na Kampuni za BHP Billiton na Barrick Gold.
Pia ana
hisa katika Kampuni ya Hutchison Wampoa inayofanya kazi za kupakua
mizigo bandarini na anamiliki majumba nchini na katika nchi za Mashariki
ya Kati.
2) Mengi
Ni Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni za IPP.
Utajiri wake unatokana na kumiliki vyombo vya habari, kiwanda cha vinywaji baridi na madini.
Mengi anamiliki magazeti kumi na moja, vituo vitatu vya televisheni na takriban vituo 10 vya redio.
Pia ana mgodi wa madini ya dhahabu na viwanda vya CocaCola.
Kwa mujibu jarida hilo, Mengi alizaliwa katika familia maskini na baadaye kusomea uhasibu huko Uingereza na kufanya kazi huko.
Alijiunga
na Chama cha Wahasibu cha Uingereza kabla ya kurejea Tanzania mwaka
1971 na kuajiriwa na Kampuni ya Ukaguzi ya Coopers & Lybrand
Tanzania (sasa Price Water House Coopers) hadi mwaka 1989, alipoacha
kazi na kujikita zaidi katika biashara.
3) Bakhresa
Said
Salim Bakhresa ni mwasisi na Mwenyekiti wa Kampuni ya Bakhresa Group na
ana utajiri wa Dola500 milioni (Sh783 bilioni).Bakhresa aliacha shule
akiwa na umri wa miaka 14 na kuanza biashara ya kuuza viazi mbatata.
Baada ya hapo alifungua mgahawa na baadaye kuingia katika biashara ya
kusaga nafaka.
4) Mo
Mafanikio
yake yamechangiwa zaidi baada ya kuendeleza mali ya wazazi wake.
Anafanya biashara ya nyumba, kuuza mazao na viwanda vya mafuta.
Mo
alirejea Tanzania baada ya kumaliza masomo yake katika Chuo Kikuu cha
Georgetown, Marekani na kuendeleza biashara ya maduka ambayo
yalianzishwa na baba yake.
Alinufaika baada ya kununua viwanda vilivyobinafsishwa na Serikali.
Alivifanya
viwanda hivyo kutengeneza faida na kuinyanyua Kampuni ya Mohamed
Enterprises (MeTL) kuwa miongoni mwa kampuni zenye mafanikio makubwa
Tanzania.
Mo pia anajihusisha na biashara ya usambazaji bidhaa, viwanda vya nguo na kilimo.
Jarida
hilo lilipiga hesabu za utajiri wa wafanyabiashara hao kwa kuangalia
thamani ya bidhaa zinazouzwa na kampuni zao, mikataba yao na hasa wale
walio kwenye sekta ya mafuta na ukubwa wa kampuni zao.CHANZO MWANANCHI
No comments:
Post a Comment