TIFFAN ENT

TIFFAN ENT

TUKO WANGAPI

TUKO WANGAPI

GLORY FREIGHT

GLORY FREIGHT

Friday, November 15, 2013

MATOKEO YA UTAFITI WA UWEZO WA MAPATO NA MATUMIZI YA KAYA BINAFSI NCHINI TANZANIA YATOLEWA 

TAKWIMU-_1_4722e.jpg
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha Dkt. Servacius Likwelile (katikati) akitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu matokeo ya utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi leo jijini Dar es salaam. Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa.
Takwimu_-_2_2_4214b.jpg
Afisa Mwandamizi wa Benki ya Dunia Bw. Richard Martini (katikati) akitoa salaam za Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia kwa nchi za Tanzania, Uganda na Burundi Bw. Phillipe Dongier, ameipongeza Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa kuzingatia vigezo vya tafiti vya kimataifa katika kutoa matokeo ya Mapato na Matumizi ya Kaya nchini.
TAKWIMU_-_3_57228.jpg
Sehemu ya waandishi wa habari wakati wa mkutano huo.(P.T)
MATOKEO YA UTAFITI WA UWEZO WA MAPATO NA MATUMIZI YA KAYA BINAFSI NCHINI TANZANIA YATOLEWA, LICHA YA CHANGAMOTO ZA UMASKINI KAYA NYINGI ZAONYESHA MAFANIKIO.
Na. Aron Msigwa – MAELEZO.
14/11/2013, Dar es salaam.
Uwezo wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi nchini kwa mwaka 2011/2012 unaonyesha kuongezeka kutokana na maboresho mbalimbali yaliyofanyika katika sekta ya elimu, afya, umiliki wa biashara, shughuli za kilimo, umiliki wa Vifaa na Rasilimali , makazi bora, ongezeko la shughuli za kiuchumi na ajira.
Akitoa taarifa ya Utafiti ulioendeshwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa kuangalia tathmini ya kiwango cha umasikini wa kaya kwa kutumia kipato na masuala mengine yasiyo ya umasikini wa kipato leo jijini Dar es salaam , Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha Dkt. Servacius Likwelile amesema kuwa kukua kwa kiwango cha elimu, matumizi ya nishati ya umeme, hali ya makazi na umiliki wa rasilimali ni miongoni mwa sababu za kuongezeka kwa uwezo wa mapato na matumizi ya kaya.
Amesema kuwa utafiti huo ulifanyika kuanzia mwezi Oktoba 2011 hadi Oktoba 2012 ambapo jumla ya kaya 10,186 kati ya 10,400 zilizokuwa zimelengwa zilihojiwa katika maeneo ya Dar es salaam na maeneo mengine ya mijini na vijijini kwa Tanzania Bara.
Amesema uchumi wa Tanzania kwa sasa umekua kutokana na kuimarika kwa sekta za ujenzi, usafirishaji, Elimu, shughuli za mawasiliano, huduma za afya na huduma za kifedha.
" Serikali imefanya mambo makubwa na sasa uchumi wa Tanzania umekua kutokana na juhudi kubwa zilizofanywa katika kuboresha miundombinu ,kuwekeza katika sekta ya elimu, usafirishaji, mawasiliano pamoja na ongezeko la huduma za kifedha" amesema.
Amesema kumekuwa na jitihada mbalimbali zilizofanywa na serikali zikiwemo kuongeza ujenzi wa shule Zaidi hasa zile za sekondari ambazo zimewezesha kupanda kwa kiwango cha wanafunzi wanaojiunga katika elimu ya sekondari kutoka 15% mwaka 2007 hadi asilimia 29% 2011/12.
Amefafanua kuwa idadi ya kaya zinazoishi katika nyumba zilizojengwa kwa vifaa vya ujenzi vya kisasa, paa za kisasa, vigae na matumizi ya zege na kuta imara tangu mwaka 2007 imeongezeka kwa 66%.
Ameongeza kuwa matokeo ya utafiti yanaonyesha kuwa asilimia 4% ya kaya zinamiliki pikipiki, 55% zinamiliki radio na 57% ya kaya zote angalau mwanakaya mmoja anamiliki simu ya mkononi na kufafanua kuwa kiasi cha asilimia 78 ya kaya za maeneo ya mengine ya mjini na asilimi 88 ya kaya za Dar es salaam zinamiliki angalau simu moja ya mkononi.
Katika hatua nyingine Dkt. Servacius ameeleza wastani wa kiwango cha umasikini wa chakula kitaifa ni asilimia 9.7 na kuongeza kuwa kiwango hicho kinafikia asilimia 11.3 kwa maeneo ya vijijini huku Dar es salaam ikiwa na kiwango cha chini kabisa cha umasikini wa chakula kwa asilimia 1.0 na maeneo mengine ya mjini yakiwa na umasikini wa chakula kwa asilimia 8.7.
Amesema miji mikubwa ina kiwango cha chini cha umasikini wa chakula kwa asilimia 1.0 ambapo wananchi wanaoishi maeneo mengine ya mjini wana umasikini wa chakula wa asilimia 8.7.
Ameongeza kuwa umasikini wa mahitaji ya msingi kwa Tanzania bara ni asilimia 28.2 ikilinganishwa na asilimia 33.3 kwa maeneo ya vijini na asilimia 21.7 kwa maeneo mengine ya mjini na kubainisha kuwa Dar es salaam ina kiwango cha chini cha umasikini wa mahitaji ya msingi cha asilimia 4.1.
Kwa upande wake Afisa Mwandamizi wa Benki ya Dunia Bw. Richard Martini akitoa salaam za Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia kwa nchi za Tanzania, Uganda na Burundi Bw. Phillipe Dongier, ameipongeza Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa kuzingatia vigezo vya tafiti vya kimataifa katika kufuatilia hali ya umasikini na kipato nchini.
Amesema twakimu za utafiti huo zilizotolewa zinaonyesha hali halisi ya maisha wanayoishi wanachi na kuongeza kuwa zitaisaidia serikali, wananchi na wadau mbalimbali wa maendeleo kuelewa na kushiriki kikamilifu katika kuleta maendeleo na kukabiliana na changamoto za umasikini zilizopo nchini.
MWISHO.

No comments:

Post a Comment