TIFFAN ENT

TIFFAN ENT

TUKO WANGAPI

TUKO WANGAPI

GLORY FREIGHT

GLORY FREIGHT

Wednesday, November 6, 2013

JK KULIHUTUBIA BUNGE KESHO

 jk_d71ab.jpg

Rais Jakaya Kikwete, kesho anatarajiwa kulihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Habari zilizopatikana Mjini Dodoma jana na kuthibitishwa na uongozi wa Bunge pamoja na Ikulu, Dar es Salaam zinasema atahutubia mchana.
Kutokana na ujio huo, Serikali imewaelekeza Mawaziri na Manaibu Waziri kutotoka nje ya Dodoma hadi hapo Rais atakapokuwa amehutubia Bunge. Kadhalika safari zote za Kamati za Bunge ambazo zilikuwa katika mchakato wa kutekelezwa zimeahirishwa hadi baada ya kesho, ili kutoa fursa kwa wabunge wote kuwapo wakati wa hotuba hiyo.
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alisema jana kuwa hata yeye amesikia taarifa kuwa Rais atazungumza bungeni lakini hajui atazungumza kitu gani... "Hata mimi nimesikia kuwa atazungumza lakini sijui atazungumza jambo gani kwa kuwa siyo miongoni mwa watu wanaomwandalia hotuba," alisema Balozi Sefue.(P.T)
Kadhalika, Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu alithibitisha kuwa Rais Kikwete atalihutubia Bunge, Alhamisi... "Nathibitisha ni kweli, ila kwa taarifa nyingine watafuteni watendaji wa Bunge, kama Katibu wa Bunge nadhani wana taarifa zaidi."
Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah alithibitisha jana katika Viwanja vya Bunge Dodoma kuwapo kwa ratiba ya Rais Kikwete kulihutubia Bunge na kwamba taarifa rasmi ingetolewa jana jioni kwa wabunge.
"Ni kweli Rais anatarajiwa kuja kulihutubia Bunge na leo (jana) jioni, tutatoa taarifa rasmi bungeni," alisema Dk Kashililah.
Mara ya mwisho Rais Kikwete alilihutubia Bunge wakati akifungua rasmi Bunge la Kumi, Novemba 18, 2010 alipoeleza vipaumbele vya Serikali yake katika awamu ya pili ya uongozi wake. Rais Kikwete analihutubia Bunge wakati likisubiri kujadili mapendekezo ya marekebisho katika Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya 2013 ambayo ilipitishwa katika mkutano uliopita.
Tayari Muswada wa Marekebisho unaopendekezwa umewasilishwa katika Ofisi ya Katibu wa Bunge chini ya hati ya dharura na leo utajadiliwa katika Kikao cha Kamati ya Uongozi ili kupata kibali cha kuingizwa ndani ya Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala na baadaye Bungeni.
Dk Kashililah alisema amepokea muswada huo na kwamba uamuzi wa lini utafikishwa bungeni utafanywa na Kamati ya Uongozi ya Bunge ambayo itakutana na leo.
Kamati hiyo ndiyo yenye mamlaka ya kuifanyia marekebisho ratiba ya vikao vya Bunge na kuruhusu mambo yanayopaswa kuingizwa bungeni kujadiliwa.
Muswada huo ni matokeo ya majadiliano baina ya Serikali kwa upande mmoja na vyama vya siasa vyenye wabunge chini ya uratibu wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) kwa upande mwingine, baada ya vyama vya siasa kutoridhishwa na muswada ulipitishwa katika mkutano wa Bunge uliopita.
Itakumbukwa kwamba wabunge wa vyama vya upinzani vya Chadema, NCCR Mageuzi na CUF walisusia shughuli za mchakato wa kupitishwa kwa marekebisho ya sheria hiyo bungeni, hivyo kutoa fursa kwa wabunge wa CCM kufanya watakavyo kisha kupitisha sheria hiyo.
Baada ya kupitishwa huko, vyama hivyo viliendesha kampeni ya kuitisha maandamano nchi nzima, lakini kabla hayajafanyika Rais Kikwete aliwaalika viongozi wake katika meza ya majadiliano, mchakato ambao umezaa mabadiliko yanayokusudiwa kuingizwa bungeni wiki hii.
Katika mazingira hayo kumekuwa na hofu kwamba huenda wabunge hasa wa CCM wakatumia wingi wao kukwamisha mabadiliko yanayopendekezwa kutokana na kukasirishwa kwao na kile kilichoonekana kuwa ni Rais Kikwete kuwasikiliza wapinzani.
Hiyo inaweza kuwa ndiyo sababu kubwa ya Rais Kikwete kuamua kulihutubia Bunge kwa lengo la kujenga msingi wa maridhiano katika mchakato wa kuandikwa kwa Katiba Mpya kama ambavyo amekuwa akisisitiza mara kwa mara.

No comments:

Post a Comment