MAREKANI YAIWEKA PABAYA TANZANIA YAIITA KITOVU CHA ‘BIASHARA’ YA BINADAMU
Marekani
imetoa ripoti inayozungumzia usafirishaji wa binadamu ya mwaka 2013,
huku ikiitaja Tanzania kuwa kinara wa kunyanyasa wasichana,
kuwatumikisha katika ngono na usafirishaji wa binadamu.
Ripoti
hiyo iliyotolewa na idara ya nchi hiyo inayohusika na diplomasia (US
Department of State, Diplomacy in Action), pia inaitaja Tanzania kuwa ni
kitovu cha njia ya kusafirisha wanawake, watoto na wanaume ambao
hutumikishwa kwenye kazi za mashambani na biashara ya ngono.(HD)
Ripoti
hiyo iliyozinduliwa Julai mwaka huu na Waziri wa Mambo ya Nje wa
Marekani, Seneta John Kerry inaweka bayana kwamba biashara ya
usafirishaji wa binadamu hufanywa na baadhi ya ndugu na marafiki ambao
hutoa ahadi kwa wahusika kwamba wanakwenda kuwasomesha au kuwatafutia
ajira nzuri mijini.
"Unyonyaji
wa wasichana wadogo na utumikishaji majumbani ndilo tatizo
linaloongoza, ingawa kesi za watoto kusafirishwa kwa ajili ya biashara
ya ngono katika mpaka wa Tanzania na Kenya zinaongezeka. Pia, wasichana
wananyonywa kwenye maeneo ya utalii," inasema sehemu ya ripoti hiyo.
Kwa
mujibu wa ripoti hiyo, watoto kutoka Burundi na Kenya, watu wazima
kutoka Bangladesh, Nepal, Yemen na India wanatumikishwa kufanya kazi
kwenye sekta za kilimo, madini na majumbani nchini Tanzania.
"Baadhi
ya raia kutoka nchi jirani huingia Tanzania kwa hiari yao, lakini
hulazimishwa kufanya kazi majumbani kabla ya kupelekwa kutumikishwa
kwenye biashara ya ngono Afrika Kusini, Ulaya na Mashariki ya Kati,"
inaeleza.
Naibu
Waziri wa Katiba na Sheria, Angela Kairuki alimtaka mwandishi kumtumia
ripoti hiyo kwa njia ya baruapepe ili aweze kuisoma na kuitolea maelezo.
Alipotafutwa
siku ya pili, alisema kuwa ameipokea na kuikabidhi ofisi ya Mkurugenzi
Mkuu wa Mashtaka (DPP) ili ifanyiwe kazi na baadaye kutoa majibu.
"Ripoti
niliipata nikaikabidhi ofisi ya DPP kwa kuwa wao ndio wanaoweza kuitolea
maelezo baada ya kuisoma. Maoni yangu lazima yawe ya kitaalamu siwezi
kusema bila kupata taarifa kutoka kwao," alisema.
Lawama kwa Serikali
Ripoti
hiyo inaitupia lawama Tanzania kwa kutokuwa na sheria thabiti za
kupambana na biashara haramu ya kusafirisha binadamu, huku ikitolea
mfano namna ilivyoshindwa kuwasaidia raia wake waliokuwa wakinyanyaswa
nje ya nchi.
"Kamati
ya Serikali ya kupambana na usafirishaji binadamu, haijachukua hatua za
kutosha katika kutekeleza mpango mkakati wa kupambana na vitendo hivyo,"
inaeleza na kuongeza:Serikali imeshindwa kutenga fedha kwa ajili ya
kuwasaidia waathirika wa usafirishaji wa binadamu kama ambavyo
inaelekezwa kwenye sheria ya kudhibiti biashara hiyo ya 2008."
Taarifa
hiyo inaitaka Tanzania kuongeza nguvu katika kutekeleza sheria ya
kudhibiti biashara ya kusafirisha binadamu ya 2008 kwa kuwakamata na
kuwashtaki wahusika wote, lakini ikaikosoa kwa kusema inatoa adhabu
ndogo kwa mtu anayebainika kufanya makosa, ikiwa ni pamoja na kumhukumu
kwenda jela miaka 10, kulipa faini au vyote viwili kwa pamoja.
"Sheria
hiyo haifanani na nyingine kama za mtu anayepatikana na kosa la kubaka
au kufanya kosa jingine la jinai. Mamlaka imesema ina kesi nne
inazozichunguza, saba zipo mahakamani toka mwaka jana, zikiwepo mbili
mpya," inasema ripoti.
Pia,
Serikali ya Tanzania imelaumiwa kwa kushindwa kuripoti maendeleo ya
uchunguzi wa maofisa wake waliotuhumiwa kujihusisha na biashara ya
usafirishaji binadamu.
LHRC na TGNP
Mkurugenzi
wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo-Bisimba
alisema tatizo la usafirishaji wa binadamu pia linachangiwa na wasichana
kuwa na tamaa ya maisha mazuri, hivyo kukubali ahadi ambazo hupewa
kwamba wanapelekwa kusoma, wasifahamu wanarubuniwa.
"Wengi
wanatamani kwenda 'majuu' wakidhani watapata elimu, lakini baadaye
wanaingizwa kwenye vitendo vinavyowafedhehesha na kuwafanya wakate tamaa
kabisa," alisema.
Naye
Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Usu Mallya
alisema katika siku za karibuni kumekuwa na ongezeko kubwa la vitendo
vya unyanyasaji dhidi ya wasichana waliochukuliwa vijijini kwenda mijini
kufanya kazi.
Alisema
pamoja na tatizo hilo kuongezeka hapa nchini, hakuna tafiti za kutosha
ambazo zimefanywa na wadau mbalimbali kuonyesha madhara yaliyopatikana
hadi sasa.
"Katika
siku za usoni kumekuwa na ongezeko kubwa la vitendo vya kunyimwa
chakula, kupigwa na kufukuzwa kazi huku wasichana wengine wakitumika
kwenye biashara ya ngono," alisema na kuongeza:
"Ripoti hii isiishie kwenye makabrasha bali ifanyiwe kazi ili jamii yote ijue kuwa hili ni tatizo."
Ripoti
hiyo inabainisha kuwa watu 47,000 pekee ndio walioweza kuokolewa mwaka
jana kutoka kwenye mazingira ya utumikishwaji kati ya milioni 27 waliopo
katika hali hiyo duniani.Tanzania imetajwa kuwa ni miongoni mwa nchi 44
ambazo zinajaribu kupambana na biashara hiyo, lakini hali inazidi kuwa
mbaya zaidi.:CHANZO MWANANCHI
No comments:
Post a Comment