MPANGO WA TAIFA WA DAMU SALAMA TANZANIA WAVUKA MALENGO WA UKUSANYAJI DAMU


MPANGO wa Taifa wa Damu Salama
 Tanzania (NBTS) umevuka malengo ya ukusanyaji damu kwa asilimia 110 
katika kipindi cha miezi mitatu ya Julai hadi Septemba 2013 ambapo jumla
 ya chupa 38,552 zilikusanywa na kuvuka malengo ya chupa 35,000 
zilizokuwa zikusanywe.
Ofisa Uhusiano na Masoko wa Mpango wa 
Damu Salama Tanzania Bw. Rajab Mwenda alisema Kanda iliyongoza kwa 
makusanyo ya damu ni Kanda ya Mashariki inayojumuisha mikoa ya Dar es 
Salaam,Morogoro,Dodoma na Pwani ambako jumla ya chupa 13,669 
zilikusanywa, Kanda inayofuatia kwa ukusanyaji damu ni Kanda ya 
Kaskazini (Kilimanjaro,Arusha, Manyara, Tanga) iliyokusanya chupa 6,159.
Alisema katika kipindi cha mwezi 
oktoba 2012 hadi Septemba 2013 takwimu zinaonyesha chupa za damu 139,676
 ambayo ni sawa na asilimia 99.8 ya lengo la kukusanya chupa 140,000 
ilifikiwa hata hivyo Mpango wa Taifa wa damu salama unakusanya asilimia 
26 ya mahitaji ya damu kwa mwaka. Mahitaji ya damu kwa mwaka ni wastani 
wa chupa 400,000- 450,000.
Alisema tofauti iliyoko ya upatikanaji
 wa damu kwenye hospitali nchini imekuwa inafidiwa na ndugu wa wagonjwa 
katika kuchangia damu ili kuokoa maisha ya mgonjwa.
Bw. Mwenda alisema mbalimbali ambazo 
zinasababisha mpango kushindwa kukusanya damu kwa 100% toka kwa 
wachangiaji damu wa hiari kunatoakana na uelewa mdogo katika jamii 
kuhusu uchangiaji damu kwa hiari kwani mfumo uliozoeleka ni ndugu wa 
mgonjwa ndiyo wanatoa.
Alisema nyingine ni uhamasishaji 
usiotosheleza toka kwa viongozi mbalimbali wa jamii, wanasiasa, viongozi
 wa dini, uuzwaji wa damu usio halali hospitalini jambo ambalo 
linawakatisha tamaa wachangia damu wa hiari, matumizi yasiyo sahihi ya 
damu katika hospitali na miundombinu hafifu hususan barabara duni wakati
 wa kukusanya na kusambaza damu.
Bw. Mwenda alisema Mpango wa Taifa wa 
Damu salama una wadau mbalimbali ambao hujitokeza kuchangia damu kwa 
hiari kama taasisi za kidini, majeshi, sehemu za kazi, mikusanyiko ya 
watu na wanafunzi ambao huchangia asilimia 80 ya damu hapa nchini
Alisema katika kipindi cha Novemba 
hadi Januari kila mwaka ni kigumu katika ukusanyaji damu kwani wadau 
wakuu ambao ni wanafunzi wanakuwa likizo ya mwaka hivyo Mpango wa Taifa 
wa Damu Salama umeweka mikakati mbalimbali ili kukabiliana na changamoto
 hiyo.
Alisema katika mikakati hiyo ni 
kufanya kampeni ya kuhamasisha uchangiaji damu kwa hiari katika jamii na
 sehemu za makanisani, minadani, stendi za mabasi, misikitini, kwenye 
masoko na sehemu za kazi.
Alisema wameanza kuhamasisha kambi za 
jeshi, makundi ya dini na ma wasiliano yamefanyika kwa jumuiya 
mbalimbali hapa nchini zichangie damu mfano jumuiya ya Khoja shia, 
Sabato na Jaula.
Pia alisema watatumia vyombo vya 
habari ili kuikumbusha na kuielimisha jamii juu ya umuhimu wa kuchangia 
damu na visaidie kutoa elimu na kutangaza ratiba ya ukusanyaji damu 
katika vituo vidogo na vikuu.
Alitoa rai kwa Watanzania kujitokeza 
kuchangia damu kwa hiari katika vituo vya damu salama kwa mtu yoyote 
mwenye afya mwanamke au mwanaume na mwenye umri kuanzia miaka 18 
ajitokeze kuchangie damu.
Alisema uchangiaji wa damu kwa hiari 
una faida kwa mtoaji kwa vile napunguza hatari ya magonjwa ya moyo, 
kuwepo kwa madini chuma mengi kupita kiasi katika damu kunakodhoofisha 
utendaji kazi na kuchangia damu mara kwa mara hurekebisha madini chuma 
ya ziada katika mfumo wa damu.
Alisema faida nyingine ni upimaji wa 
afya pasipo gharama kwa sababu wakati unapochangia damu mtaalamu wa tiba
 daktari au muuguzi atapima shinikizo la damu yako, mapigo ya moyo na 
kukufanyia vipimo vya afya bure.
Alisema kutoa damu kunaongeza utambuzi
 wa kiwango cha chembe hai nyekundu na chembe na huchochea uzalishaji wa
 seli damu mpya na kuwaomba wanahabari kuendelea kuhamasisha na 
kuielimisha jamii kuhusu umuhimu wa kuchangia damu kwa hiari mara kwa 
mara kwani ni damu ya mwanadamu pekee inayotumika kumuongezea mgonjwa 
anayehitaji damu.
No comments:
Post a Comment