TRA MBARONI KWA MENO YA TEMBO ZANZIBAR

Na Mohammed Mhina wa Jeshi la Polisi-Zanzibar
Jeshi la Polisi Zanzibar limewakamata 
watuhumiwa wemhine watatu wakiwemo Maafisa wawili wa Mamlaka ya Mapato 
nchini TRA kituo cha Bandari Zanzibar kwa kuhusika na kashfa ya 
kupatikana kwa meno ya tembo yenye thamani ya Mabilioni ya shilingi.
Kamishna wa Polisi Zanzibar CP Mussa 
Ali Mussa, amewataja Maafisa hao wa TRA waliokamatwa kuwa ni Omari Hamad
 Ali(50) na Mohammed Hija(48) ambao wote wanafanyia kazi katika Bandari 
ya Zanzibar. Mtuhumiwa mwingine ni kibarua wa Mamlaka ya bandari 
Zanzibar Haidar Ahmad Abdallah(54).(P.T)
Kukamatwa kwa watuhumiwa hao kunaifanya idadi ya watuhumiwa waliokamatwa hadi sasa kwa kuhusika na sakata hilo kufikia watano.
Kamishna Mussa amesema Watuhumiwa 
wengine wawili ambao ni wafanyakazi wa Kampuni ya Uwakala wa Mizigo ya 
Island Sea Food Limited, Mohammed Suleiman Mussa(45) na Juma Ali 
Makame(34) wao walikamatwa siku ya tukio la kukamatwa kwa meno hayo ya 
tembo kwenye Bandari ya Zanzibar.
Tayari watuhumiwa hao wamesafirishwa 
kwenda Makao Makuu ya Polisi Dar es Salaam kwa ajili ya mahojiano 
zaidi.Pamoja na mambo mengine, kusafirishwa kwa watuhumiwa hao kwenda 
Jijini Dar es Salaam, kunatokana na Zanzibar kutokuwa na Sheria maalumu 
inayohusu wanyamapori.
Maafisa wa Idara ya Wanyamapori 
nchini, leo wamekamilisha kazi ya kuhesabu na kulinganisha vipande 1,023
 vya meno ya tembo vilivyokamatwa jana kwenye Bandari ya Zanzibar na 
kubaini idadi ya tembo waliouawa kuwa ni 305.
Meno hao yenye uzito wa kilo 2,915 
yenye thamani ya Dolla 4,775,000 sawa na shilingi 7,480,125,000 za 
Tanzania (Bil.7.4), yalikamatwa juzi yakiwa yamehifadhiwa katika magunia
 98 na kuwekwa kwenye konteina moja la futi 40 lenye namba PCIU 857619/0
 lillilokuwa tayari kupakiwa kwenye meli ya MV Kota Henning kupelekwa 
nchini Ufilipino kwa magendo.
Hadi sasa bado Makachero wa Polisi wa 
Kimataifa Interpol hapa nchini kwa kushirikiana na Makachero wa Polisi 
Zanzibar, idara ya wanyamapori makao makuu wanaendelea na upelelezi wa 
kuwabaini wale tote waliohusika na kashfa hiyo.
Jana Kamishna wa Polisi Zanzibar CP 
Mussa Ali Mussa, alisema kuwa kazi kubwa iliyobaki ni kuhakikisha kuwa 
upelelezi wa kina unafanyika ili kuwakamata wale wote wanaohusika na 
mtandao huo.
Alisema hadi sasa Jeshi la Polisi bado
 linamsaka tajiri aliyewezesha mipango ya kukusanywa na kusafirisha 
shehena hiyo kutoka Tanzania Bara hadi Zanzibar ili kusafirishwa nje ya 
nchi.
No comments:
Post a Comment