CHADEMA YAJIPANGA KUIMARISHA KITENGO CHA ULINZI NA USALAMA " RED
BRIGADE" ILI KUWAKABILI VIJANA WA CCM WATAKAOLETA FUJO
MUHTASARI
Ili
kukabiliana na vitendo vya fujo vinavyofanywa na vijana wa CCM dhidi ya
wagombea, Wanachama na viongozi wa CHADEMA, Kamati Kuu imeagiza kwamba
kitengo cha ulinzi cha Chama “Red Brigade” kiimarishwe zaidi kwa
kuhakikisha kuwa vijana wote wa Red Brigade Nchi nzima wanapewa mafunzo
maalum ya UKAKAMAVU yatakayoandaliwa katika Makambi maalum katika mikoa
yote.
RIPOTI KAMILI
TAARIFA KWA UMMA KUHUSU MAAMUZI YA KIKAO CHA KAMATI KUU YA CHAMA
KILICHOFANYIKA TAREHE 06-07/07/2013 KATIKA HOTEL YA BLUE PEARL, DAR ES
SALAAM.
Kamati kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo ilikutana katika Kikao
cha dharura kuanzia tarehe 06-07/07/2013 katika Hotel ya Blue Pearl Dar
es salaam kujadili pamoja na mambo mengine Rasimu ya Katiba mpya na
hali ya Siasa nchini.
Kamati kuu imejadili na kuyatolea maamuzi mambo mbalimbali kama ifuatavyo:
1:0. Hali ya Siasa Nchini.
Kamati kuu imepokea taarifa ya hali ya siasa nchini na kuzingatia mambo yafuatayo:
a) Shambulio la Bomu Arusha.
Kamati Kuu imesikitishwa na kulaani kwa nguvu zote tukio la Bomu
Arusha lililosababisha watu wanne kuuwawa na zaidi ya watu 70 wengine
kujeruhiwa vibaya.
Kamati Kuu imeridhika kwamba shambulio hilo lililenga kuwaua viongozi
wakuu wa CHADEMA akiwamo Mwenyekiti wa Taifa Mheshimiwa Freeman A. Mbowe
na Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini na Mjumbe wa Kamati Kuu, Mheshimiwa
Godbless J. Lema na viongozi na wanachama wengine wa CHADEMA
waliohudhuria Mkutano wa kufunga kampeni za udiwani katika Jiji la
Arusha pamoja na kuvuruga Uchaguzi huo na kuinyima CHADEMA ushindi
mkubwa;
Kamati Kuu imeridhika kwamba ushahidi uliopo wa vielelezo na wa
mashuhuda wa shambulio unaonyesha ushiriki wa moja kwa moja wa Jeshi la
Polisi katika shambulio hilo;
Kamati Kuu imefadhaishwa na kauli ya Serikali bungeni iliyolenga
kulikosha Jeshi la Polisi kwa kuhusika kwake na shambulio hilo dhidi ya
CHADEMA na wananchi wa Jiji la Arusha na kuilaumu CHADEMA wakati CHADEMA
ndio mhanga wa shambulio hilo;
Kamati Kuu imeshangazwa na kitendo cha Serikali kupuuza maafa
yaliyowafika wananchi wa Arusha kwa kushindwa kushiriki katika mazishi
ya wahanga wa mauaji ya Soweto na kuwashambulia kwa mabomu ya machozi,
vipigo na maji ya sumu waombolezaji waliokusanyika kuwaaga marehemu
waliouawa kwenye shambulio;
Kamati Kuu imesikitishwa na Rais Kikwete kuendelea kukaa kimya juu ya
shambulio la Arusha na kushindwa kwake kuunda Tume huru ya Kimahakama
kuchunguza kwa uwazi shambulio hilo. Aidha, Kamati Kuu inaamini kwamba
ukimya huu wa Rais Kikwete na kushindwa kwake hata kuwatembelea wafiwa
na wahanga wengine wa shambulio hilo ni ushahidi mwingine wa kuhusika
kwa vyombo vya ulinzi na usalama vya Serikali katika kupanga na
kutekeleza shambulio la Arusha;
Kamati Kuu imefadhaishwa na kitendo cha Bunge la Jamhuri ya Muungano
kuendelea na vikao vya Bunge kama kawaida; kukataa kutoa mchango wowote
kwa wahanga na kushindwa kupeleka ujumbe wa Bunge kuwatembelea na
kuwafariji wahanga na waathirika wa shambulio kinyume na utaratibu
uliozoeleka wa Bunge kutambua na kushiriki katika majanga na misiba ya
aina hii.
Kamati Kuu inautaka uongozi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano uwaeleze
Watanzania kama maafa ya shambulio la Arusha yalikuwa na tofauti yoyote
na maafa ya shambulio la bomu la Olasiti, au na maafa ya mabomu ya Gongo
la Mboto, ajali ya MV Skargit au maafa mengine yaliyosababisha Bunge la
Jamhuri kuahirisha shughuli zake, kutoa michango kwa waathirika pamoja
na kupeleka ujumbe wa Bunge kuwafariji wafiwa na wahanga wa matukio
hayo;
Kutokana na maelezo hayo hapo juu Kamati kuu imeazimia kuwa:
• Iwapo Rais ataendeleza msimamo wa kutokuunda tume huru ya kimahakama,
Ushahidi uliopo juu ya tukio la kurushwa Bomu Arusha utawekwa wazi muda
utakapofika kwa wananchi wa Tanzania; vyama na mashirika ya kiraia ya
haki za binadamu hapa nchini na ya nje ya nchi; ofisi za kibalozi za
mataifa rafiki na Tanzania pamoja na jumuiya ya kimataifa ili
yaishinikize Serikali kuunda Tume huru ya Kimahakama kuchunguza
shambulio hilo na matukio mengine ya mauaji yenye sura ya kisiasa ambayo
yamehusishwa na Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya usalama vya
Serikali au vya Chama cha Mapinduzi;
2:0. Hali ya Wananchi wa Mtwara.
Kamati kuu imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa juu ya unyanyasaji,
utesaji, ubakaji na uonevu wanaofanyiwa wananchi wa Mtwara hivi sasa na
vyombo vya dola huku serikali ikikaa kimya juu ya jambo hili bila
kukemea. Kamati kuu imejadili kwa kina namna wananchi wa Mtwara
wanavyofanyiwa na vyombo vya dola na kufikia maazimio yafuatayo;
Vyombo vya dola vitimize wajibu wake wa kulinda amani na mali ya raia
na siyo kuwatesa na kuwapiga wananchi kwa kuwasababishia vifo kinyume
na Haki za Binadamu.
Serikali iwasikilize wananchi wa Mtwara na siyo kutumia ubabe,
unyanyasaji, uonevu na mateso kama mbinu za kuhalalisha kukubalika kwake
kwa wananchi.
Rais Kikwete alitangazie taifa “hali ya hatari” kwa mkoa wa Mtwara
kama anaona kuwa Mtwara ni hatari kwa kiasi hicho cha kulitumia JWTZ
kuzunguka mitaani na silaha za kijeshi ili taifa liweze kujua,Aidha kama
jeshi la polisi limeshindwa kutimiza majukumu yake kwa mujibu wa sheria
atangaze kulivunja jeshi hilo mara moja.
Serikali iunde tume huru ya kuchunguza matukio ya
mauaji,ubakaji,utesaji na ukiukwaji wa haki za binadamu yaliyofanywa na
vyombo vya dola na waathirika wote waweze kufidiwa kwa mujibu wa sheria.
3:0. Kauli ya Waziri Mkuu.
Kamati Kuu imejadili kwa kina kauli ya Waziri Mkuu Bungeni kwamba ni
sahihi kwa Jeshi la Polisi nchini kuwapiga Wananchi wote wanaotumia haki
zao za Kikatiba kupinga sera au maamuzi ya Serikali. Kamati Kuu
imeazimia kuwa:
Kauli ya Waziri Mkuu imekiuka Katiba na sheria za nchi yetu
zinazokataza Jeshi la Polisi kutumia nguvu dhidi ya raia wasiokuwa na
silaha na ambao wanatumia haki zao za kikatiba kufanya maandamano;
Kamati Kuu inaamini kwamba kauli ya Waziri Mkuu inatoa Baraka kwa
Jeshi la Polisi kuendeleza vitendo vya ukatili na mauaji dhidi ya
wananchi ambayo yamelifanya Jeshi la Polisi la Tanzania kutangazwa kuwa
moja ya majeshi katili ya polisi katika Afrika Mashariki;
Kamati Kuu inaungana na wananchi, taasisi na mashirika ya kitaifa na
kimataifa ambayo yamelaani vikali kauli hiyo ya Waziri Mkuu na inawataka
wananchi, taasisi na mashirika hayo kuendelea kumlaani vikali Waziri
Mkuu kwa kauli hiyo;
Kamati Kuu inaamini kwamba Waziri Mkuu amepoteza sifa za kuendelea
kuwa Waziri Mkuu na inaungana na wananchi na taasisi ambazo zimedai
Waziri Mkuu awajibike au awajibishwe kutokana na kauli yake hiyo. Aidha,
Kamati Kuu inawaelekeza Wabunge wote wa CHADEMA washirikiane na Wabunge
wengine wote wenye mapenzi mema na nchi hii na ambao wanaamini katika
utawala wa sheria waanzishe mchakato wa kumpigia kura ya kutokuwa na
Imani Waziri Mkuu kupitia Bunge;
Kamati Kuu imewataka Jeshi la Polisi kama sehemu ya jamii ya
watanzania kupuuza kauli ya Waziri Mkuu katika utekelezaji wa kazi zao
kwa kuwa kauli hiyo ni ya uvunjifu wa Katiba na Sheria na inachochea
uvunjifu wa amani.
4:0. Uchaguzi wa Madiwani.
Kamati Kuu imepokea taarifa kuhusu ushiriki wa CHADEMA katika Uchaguzi
wa Madiwani uliofanyika tarehe 16/06/2013 katika kata 22.
Kamati Kuu imeipongeza Sekretarieti na uongozi wa Kanda mbalimbali za
CHADEMA kwa maandalizi mazuri katika Uchagzuzi huo uliosababisha CHADEMA
kuwapokonya CCM ushindi katika kata 4 ilizokuwa imeshinda katika
Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010. Kamati Kuu imewapongeza wananchi kwa
kuipatia CHADEMA kura asilimia (47.7%) dhidi ya CCM (49%) na (3.3%) za
CUF.
Kamati kuu imesikitishwa na vitendo vya fujo walivyofanyiwa viongozi,
wagombea pamoja na Wanachama mbalimbali katika sehemu mbalimbali palipo
fanyika Uchaguzi. Kamati Kuu imesikitshwa na kulaani vitendo hivyo
vikiwemo vya watu kukatwa mapanga , kuchomwa visu na kubakwa kwa akina
Mama na vijana wahuni walioandaliwa na Chama cha Mapinduzi.
Kamati Kuu imelaani vitendo hivyo vya kinyama vilivyofanywa mbele ya jeshi la polisi na Wakuu wa Wilaya.
Ili kukabiliana na vitendo vya fujo vinavyofanywa na vijana wa CCM
dhidi ya wagombea, Wanachama na viongozi wa CHADEMA, Kamati Kuu imeagiza
kwamba kitengo cha ulinzi cha Chama “Red Brigade” kiimarishwe zaidi kwa
kuhakikisha kuwa vijana wote wa Red Brigade Nchi nzima wanapewa mafunzo
maalum ya UKAKAMAVU yatakayoandaliwa katika Makambi maalum katika mikoa
yote.
Kamati Kuu imejadili maandalizi ya Uchaguzi wa madiwani katika kata
nne (4) katika Jiji la Arusha. Kamati Kuu imepokea kwa masikitiko
taarifa juu mipango inayofanywa na jeshi la polisi kwa kushirikiana na
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Magesa Mulongo na viongozi wengine wa CCM mkoani
Arusha katika kuhujumu zoezi la Uchaguzi kwa kuwatisha wapiga kura kwa
kutumia polisi na vijana wa Green Guard siku ya uchaguzi.
Kamati Kuu inamtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) kuchukua hatua
stahiki kuzuia harakati za polisi na CCM za kuvuruga Uchaguzi na kutaka
kujipatia ushindi kwa njia za hila. Aidha Kamati kuu imelitaka jeshi la
polisi kuheshimu maadili ya uchaguzi yaliyosainiwa na Serikali, Tume ya
uchaguzi na vyama vya siasa.
Kamati Kuu imesikitishwa na Tume ya Uchaguzi kushindwa kuwazuia CCM
kuendelea na kampeni za Uchaguzi huku wakiwa wamezuia kampeni hizo kwa
vyama vingine.
Kamati Kuu imeendelea kuwapa pole wananchi wa Arusha kwa matukio
mabaya wanaofanyiwa na serikali ya CCM mkoani humo, na imewapongeza kwa
kusimama kidete katika kulinda haki na ukweli.
Kamati Kuu imewaomba wananchi wa Arusha wajitokeze kwa wingi siku ya
kupiga kura tarehe 14 Julai 2013, na imewataka wabunge wote washiriki
katika kusimamia zoezi la upigaji kura na uhesabuji kura siku ya
Uchaguzi na wananchi wajitokeze kwa wingi kulinda kura bila hofu.
5:0. Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Kamati Kuu imejadili kwa kina sana maudhui yaliyomo katika Rasimu ya
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliyotolewa na Tume ya
Mabadiliko ya Katiba;
• Kamati Kuu imetambua kazi kubwa iliyofanywa na Tume ya Mabadiliko ya
Katiba katika kukusanya na kuchambua maoni ya wananchi na kuandaa Rasimu
ya Katiba Mpya;
• Hata hivyo, Kamati Kuu imetambua na kuainisha mapendekezo mengine ya
msingi ambayo yanastahili kuboreshwa zaidi katika Rasimu hiyo;
• Msimamo na maazimio ya Kamati Kuu juu ya Rasimu ya Katiba Mpya
yameainishwa na kuchapishwa katika kijitabu maalumu ambacho
kitazinduliwa katika Mkutano wa hadhara utakaofanyika siku, tarehe na
mahali patakapo tangazwa hapo baadaye.
Imetolewa na:
……………………….
Freeman A. Mbowe, (MP)
Mwenyekiti Taifa
No comments:
Post a Comment