WAFANYAKAZI HALMASHAURI YA KILOLO WANAISHI 'PEPONI'
MWALIMU Julius Nyerere, katika kitabu chake cha Uhuru na Maendeleo cha mwaka 1973 alisema: "Tunaweza kujibagua kutoka kwa wenzetu kutokana na elimu tuliyonayo; tunaweza kujaribu kujilimbikizia wenyewe mali haramu ya umma. Lakini gharama kwetu, pamoja na kwa ndugu zetu, itakuwa kubwa mno. Itakuwa kubwa siyo tu kwa kushindwa kutimiza haja zetu, lakini pia kwa usalama wetu na ustawi wetu."
Naam. Nimeamua nianze na nukuu hii kutokana na ukweli kwamba hali ya uadilifu aliyoisimamia Mwalimu Nyerere na kuiabudu imetoweka kwa watumishi wa umma ambao, pengine kwa kujiona ‘wamesoma’ sana kuliko wengine na kupewa nyadhifa walizonazo, wameamua kujibagua na kuangalia namna ya kujilimbikizia madaraka na mali bila kujali Watanzania wenzao.
Kwa miaka zaidi ya 10 sasa Watanzania wanalia kuhusu viongozi wa umma kukosa uadilifu. Jambo baya zaidi ni kwamba, hakuna hata kiongozi mmoja wa juu anayeweza kumkemea mwenzake kutokana na kushindwa kutekeleza wajibu wake ama anapoona amekiuka kanuni za utawala.
Pale inapotokea kiongozi mmoja akachukua hatua dhidi ya wale wanaojiona ‘miungu-watu’ kwa kutumia visivyo mali za umma, kiongozi huyo anachukuliwa na watu wa kada hiyo kama dikteta, mbabe na anayekiuka ‘haki za binadamu’.
Hivi sasa kuna mazengwe yanayoendelea katika Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa. Mazengwe haya yanatokana na watendaji wa Halmashauri ‘kujisahau’ na kutenda kinyume na taratibu, hali ambayo kwa kiasi kikubwa imesababisha kuwepo kwa vitendo vingi vya ufisadi, matumizi mabaya ya madaraka na hivyo kuwa kero kubwa.
Hakuna ubishi kwamba Wilaya ya Kilolo haina ardhi kwa sababu viongozi wa halmashauri na serikali kwa ujumla walishiriki kwa namna moja ama nyingine kuwashawishi wananchi wauze ardhi kwa wawekezaji wa New Forests Company. Matokeo yake vijiji vingi kwa sasa havina hata ardhi ya ziada, hata ya kujenga zahanati.
Baadhi ya watendaji nao wamekuwa wakihusika na migogoro ya ardhi kwa sababu wanazojijua wao. Hali hii ndiyo iliyomlazimu Mkuu wa Wilaya hiyo, Gerald Guninita, kumweka mahabusu Kaimu Ofisa Mtendaji wa Kata ya Mlafu, Thomas Nyabange, kutokana na uzembe wa kushindwa kushughulikia mgogoro wa ardhi kwenye kata hiyo.
Hakuishia hapo, kwani hivi karibuni alimkamata Ofisa Usafirishaji wa wilaya hiyo, Beatus Nyato, na kumweka ndani kwa kosa la kushindwa kuidhinisha gari la kuwapeleka askari nyumbani kwake kwa shughuli za kumlinda usiku.
Ukiachana na hayo, hali halisi inaonyesha kwamba watumishi wa halmashauri hiyo wanaishi ‘peponi’ kwani wanatumia mali ya umma kadiri wanavyopenda, na hawataki waguswe wala wanyooshewe kidole. Ukiondokea tu kuwa mfuatiliaji wa masuala yao, ‘wanakushughulikia’.
Asilimia kubwa ya watumishi hao wanaishi Iringa mjini, zaidi ya kilometa 50 kutoka Kilolo. Kwa hiyo, kila siku asubuhi wanakwenda huko kufanya kazi, jioni wanarejea tena.
Afadhali wangekuwa wanatumia usafiri wao, lakini wanatumia magari ya serikali, tena mashangingi ambayo yanabugia mafuta kama hayana akili nzuri. Mafuta yanayotokana na kodi za walalahoi kama mimi.
Wamejiwekea wenyewe kautaratibu kao kwamba kila asubuhi wanakwenda pale Ipogolo mbele ya Mti Mkubwa wakisubiri magari ya STJ na STK yapite, wapande ili waende kazini. Hata kama kuna usafiri mwingine wa umma, hawako tayari kupanda kwa sababu si kuna magari ya serikali yanayotumia ‘mafuta ya bure’?
Ukiwauliza fedha za mafuta hayo wanazitoa katika fungu gani hawawezi kujibu haraka, lakini kwa vyovyote zitakuwa zinatoka katika fungu la maendeleo, hali ambayo kwa hakika itakuwa inakwamisha miradi mingi ya maendeleo kwa matumizi yasiyo ya lazima.
Kwamba watumishi hao hawana nyumba huko, ni suala la halmashauri yenyewe na Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Ilikuwaje Tamisemi waliiunda wilaya hiyo bila kujenga nyumba za watumishi? Na kwa nini miaka zaidi ya sita sasa tangu Kilolo iwe wilaya nyumba hizo hazijajengwa?
Hicho lakini hakiwezi kuwa kisingizio, kwa sababu tunatambua kwamba hata Iringa mjini watumishi wengi hawaishi katika nyumba za serikali, wamepanga. Sasa kwa nini watumishi hawa wa Kilolo wasipange huko huko? Jibu ni rahisi – wakipanga huko watakula wapi?
Hivi kama watumishi wa Wilaya ya Mufindi nao wangekuwa wanaishi Iringa mjini, halafu wawe wanakwenda na kurudi kazini, hali ingekuwaje?
Ajabu ni kwamba, pamoja na juhudi zote alizozichukua Guninita za kuwabana watumishi wanaotumia vibaya mali ya umma, hakuna anayezipongeza na badala yake amekuwa adui yao mkubwa.
Tayari amekwishatishiwa maisha na baadhi ya watendaji hao ambao wanasema anaingilia mirija yao ya unyonyaji. Inadaiwa kwamba wameapa ‘kumshughulikia’.
Kwa kweli hali hiyo inasikitisha sana na ninashangaa ikiwa Ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali itakuwa haijagundua matumizi haya ya kifisadi. Kwa matumizi haya mabaya ya fedha za umma, kweli Kilolo inastahili kupewa hati safi?
Nimpongeze tu Guninita kwa juhudi zake hizo, ambazo zinatakiwa kuungwa mkono na wapenda maendeleo, na ninamwambia kamwe asitishike na kelele za watendaji hawa ambao kimsingi wamekuwa wanyonyaji na wanatakiwa kuona aibu. Japo mara moja.
No comments:
Post a Comment