"WANAOPINGA KODI YA LINE ZA SIMU NI WANAFIKI WASIOPENDA MAENDELEO "....MIZENGO PINDA
WAKATI Serikali ikiahidi kutazama upya 
tozo ya Sh 1,000 kwa laini za simu ili kupunguza mzigo kwa wananchi, 
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, amesema tozo hiyo si ya kuwaumiza wananchi 
bali mapato yake yatakwenda moja kwa moja kusaidia kueneza umeme 
vijijini.
Alisema hayo alipozungumza kwenye 
mkutano wa hadhara mjini Songea juzi, katika ziara yake ya wiki moja 
mkoani Ruvuma, baada ya kuutembelea mkoa mpya wa Njombe.
“Ni kama vile tozo iliyoongezwa kwenye 
mafuta ya petroli, ambayo imetupa fedha nyingi kwenye Mfuko wa Barabara,
 za kuunganisha miji na mikoa na nyingi zimejengwa na zinaendelea 
kujengwa.
“Nani asiyetaka vijiji vipate umeme 
kama miji, ili usaidie kuondoa giza, uendeshe viwanda vidogo vidogo na 
usaidie kukuza uchumi? Wanaopinga tozo hii, hawatutakii mema,” alisema Pinda.
Bunge la bajeti lililomalizika mwezi 
uliopita, lilipitisha tozo ya Sh 1,000 kwa matumizi ya simu za mikononi,
 ili fedha zitakazopatikana zisaidie katika mpango mkubwa wa kueneza 
umeme vijijini unaoendeshwa na Wakala wa Umeme Vijijini, (REA). Kwa mkoa
 wa Ruvuma peke yake, vijiji vipatavyo 150 vitapatiwa umeme chini ya 
mpango huo.
Katika mikoa yote nchini kuna idadi 
inayotofautiana ya vijiji vingi vitakavyonufaika katika mpango huo. 
Umeme umo katika sekta ya nishati ambayo ni moja ya sekta sita 
zilizoteuliwa kutekelezwa chini ya mpango wa kuhakikisha matokeo makubwa
 yanapatikana sasa, wenye upeo wa miaka mitatu, kuanzia mwaka huu wa 
fedha wa 2013/14. Sekta nyingine ni Kilimo, Uchukuzi, Maji, Elimu na 
Mapato.
Kabla ya mkutano wa hadhara, Waziri Mkuu
 alizindua Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi cha Songea, kinachodahili 
zaidi ya wanafunzi 500 na kutoa mafunzo ya muda mfupi kwa mfundi stadi 
mbalimbali.
Awali Waziri Mkuu Pinda alisema bei ya mahindi kutoka kwa mkulima katika mkoa wa Ruvuma, itakuwa ni Sh 500 kwa kilo badala ya Sh 450, ili wakulima wahamasike kuuza mahindi kwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA).
Mkoa wa Ruvuma ni moja ya mikoa 
inayozalisha mahindi, chakula kikuu nchini kwa wingi na NFRA inatarajia 
kununua tani 50,000 kutoka katika mkoa huo.
NRFA imepangiwa kununua zaidi ya tani 
200,000 nchini kote kwa ajili ya hifadhi ya chakula, kiwango kikubwa 
kuliko mwaka uliopita.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Pinda pia aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa soko la kimataifa katika kijiji cha Mkenda kwenye mpaka na Msumbiji, ikiwa ni moja ya masoko 48 yatakayojengwa mipakani kurahisisha biashara na kukabiliana na magendo. Leo Waziri Mkuu ataondoka Songea kurejea Dar es Salaam baada ya kumaliza ziara yake mkoani humo.

No comments:
Post a Comment