WAZIRI AKWEPA HOJA ,AMSHAMBULIA LISSU
Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Samia Suluhu Hassan alikataa
kueleza walipo waasisi sita wa Muungano ambao kambi ya upinzani ilidai
kuwa waliuawa na kuzikwa handaki moja, badala yake akatumia nafasi hiyo
kumshambulia mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu akidai hizo ni
propaganda na upotoshaji.
Juzi
wakati akiwasilisha hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani, Lissu aliitaka
Serikali kutoa maelezo bungeni kuhusu sababu za kuuawa kwa waasisi sita
wa Muungano wa Tangayika na Zanzibar na kuzikwa katika handaki moja
visiwani Zanzibar.
Lissu
aliwataja waasisi hao kuwa ni Abdalah Kassim Hanga, aliyekuwa waziri
mkuu, Abdul Aziz Twalam aliyekuwa Waziri wa Fedha na Abdulaziz na Saleh
Akida aliyekuwa mjumbe wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar.(P.T)
Pia
aliwataja Othman Shariff, Mdungi Ussi na Jaha Ubwa ambao alisema nao
waliuawa na kuzikwa katika handaki moja eneo la Kama nje kidogo ya
Zanzibar.
"Tunataka
kujua ukweli kama walifanya makosa, walishtakiwa katika mahakama gani
iliyowahukumu adhabu ya kifo... tunataka kuambiwa ukweli kwanini mchango
wao kuhusu Muungano umefichwa," alisema Lissu juzi.
Lakini
alipoulizwa kuhusu madai hayo, Waziri Hassan alionekana kuzigeuza hoja
hizo kuwa ni za Lissu pekee badala ya kambi ya upinzani na kumshambulia
mbunge huyo akidai kuwa ni mpotoshaji, anayepiga propaganda na
mchochezi.
Waziri
huyo, ambaye ni Mzanzibari, alisema alipuuza maswali yote kuhusu waasisi
hao akisema mbunge huyo wa Chadema alipotoka katika hotuba yake na ndio
maana hakutaka kuzungumzia katika majumuisho ya bajeti ya ofisi yake
bungeni.
"Yule Lissu sio mkweli na ndio maana sisi tulimpuuza," alisema waziri huyo.
"Hakuna
kitu kama hicho na endapo kingekuwepo sisi Serikali tungeshatoa
ufafanuzi ili watu wapate kujua ukweli wake," aliongeza Waziri Samia
bila kutoa ufafanuzi wa nini kiliwatokea watu hao walioshika nafasi za
juu serikalini mara baada ya Mapinduzi na Muungano wa Zanzibar na
Tanganyika.
Pamoja na
kudai kuwa aliona hoja hizo ni upotoshaji, Waziri huyo, ambaye pia ni
makamu mwenyekiti wa Bunge la Katiba, aliwasihi wabunge wa upinzani
kupeleka hoja zao katika Bunge Maalumu la Katiba linalojadili uundwaji
wa Katiba Mpya, ambalo pia limetawaliwa na suala la muundo wa Muungano
na kero zake.
Waziri
Samia alisema hoja hizo zinalenga kuwaaminisha Watanzania mambo ambayo
hayapo ili kuwajaza chuki dhidi ya Serikali yao na pia alidai zina
uchochezi ndani yake.
Waziri
Samia aliwashauri wabunge pamoja na Watanzania kupuuza kauli hizo akidai
mbunge huyo hautakii mema Muungano na ndio maana anaibua mambo aliyodai
kuwa ni ya uongo na ya uchochezi.
No comments:
Post a Comment