MAPINDUZI MAKUBWA YA VIWANDA
WIZARA ya Viwanda na Biashara imewasilisha bungeni bajeti yake inayoonesha mapinduzi makubwa katika viwanda, ikiwamo kuanza kwa miradi ya chuma ya Liganga na Mchuchuma na kiwanda cha kuua viluwiluwi vya mbu waenezao malaria.
Pia
kiwanda cha matairi cha General Tyre kinatarajiwa kuanza tena uzalishaji
katika mwaka ujao wa fedha. Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Abdallah
Kigoda aliwasilisha bajeti yake hiyo bungeni jana.(Martha Magessa)
Dk Kigoda
alisema ukuaji wa sekta ya viwanda ni mzuri kwani umeongezeka kutoka
asilimia 5.5 mwaka 1998 hadi asilimia 7.7 mwaka 2013, ingawa ukuaji huo
uko chini kidogo ukilinganisha na mwaka 2012.
“Ukuaji
huu umechangiwa kwa kiasi kikubwa na kuimarika kwa uzalishaji viwandani,
hususani viwanda vya vinywaji, saruji, bidhaa za chuma, na usindikaji
wa mazao ya kilimo,” alisema Dk Kigoda.
Kuhusu
Liganga na Mchuchuma, alisema katika mwaka 2013/14, utafiti uliofanywa
na Serikali kupitia Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) umethibitisha
kuwapo kwa mashapo ya makaa ya mawe ya tani milioni 370 katika eeno la
kilometa za mraba 30.
Alisema
utafiti huo, pia umethibitisha kuwapo kwa mashapo ya madini ya chuma ya
tani milioni 219 katika eneo la kilometa za mraba 10.
“Mpango
wa awali ni kuzalisha tani milioni moja za chuma na megawati 600 za
umeme. Kiasi hicho cha uzalishaji wa chuma kitaifanya Tanzania kuwa ya
tatu barani Afrika katika uzalishaji chuma.
“Aidha, kukamilika kwa miradi hiyo kutawezesha ajira zipatazo 32,000 na mapato ya takriban Sh trilioni 2.8,” alisema Dk Kigoda.
Alieleza
kuwa jambo la kutia moyo ni kwamba tayari dola za Marekani bilioni tatu
(Sh trilioni tano) zimepatikana na wabia wa miradi hiyo, NDC na Tanzania
China International Mineral Resources Ltd (TCIMRL) na kuwezesha ujenzi
wa viwanda vya chuma kuanza mwaka 2014/15.
Kuhusu
ujenzi wa kiwanda cha kuzalisha viuadudu vya kuua viluwiluwi vya mbu
waenezao malaria mjini Kibaha, kwa kutumia teknolojia kutoka Cuba,
alisema ujenzi wa majengo umekamilika kwa asilimia 90.
“Mitambo
imekwishanunuliwa na kufikishwa katika eneo la ujenzi na hivi sasa
inawekwa tayari kwa uzalishaji mwanzoni mwa mwaka 2014/205 yaani mwezi
Julai 2014,” alisema Waziri.
Alisema
kukamilika kwa mradi huo ni ukombozi mkubwa kwa Taifa katika kupambana
na malaria kwa kuwa viuadudu vitakavyozalishwa, kazi yake ni kuua mbu
kuzaliana na hivyo kupunguza wagonjwa wa malaria, gharama za kununua
vyandarua na dawa za kuulia mbu.
Akizungumzia
kiwanda cha General Tyre Ltd (GTEA), alisema NDC imekamilisha
kukarabati majengo na ukarabati wa mfumo wa umeme unaendelea na kisha
utafuatiwa na kujaribu mitambo.Kuhusu uzalishaji wa magadi soda Ziwa
Natron na Engaruka, alisema utafiti umekamilika kuhusu wingi na ubora wa
rasilimali za magadi.
Alisema
kiasi cha meta za ujazo bilioni 4.68 za magadi ambazo huongezeka kwa
kiasi cha mita za ujazo milioni 1,8675 zimegundulika katika Bonde la
Engaruka. Kwa sasa, anatafutwa mtaalamu mshauri na makadirio ya ujenzi
wa yatajulikana baada ya usanifu wa mradi huo ambao unatarajiwa kuanza
uzalishaji mwaka 2016/17.
Utaingiza
dola za Marekani milioni 320 kwa mwaka na utatoa fursa za ajira 3,900.
Dk Kigoda akizungumzia saruji alisema kumeanzishwa viwanda katika mikoa
ya Mtwara, Lindi na Pwani, na miradi hiyo itakapokamilika pamoja na
viwanda vilivyopo, vitakuwa na uwezo wa kuzalisha tani milioni sita kwa
mwaka na kutoa ajira zaidi ya 5,000.
“Kiasi
hicho cha saruji kitakuwa mara mbili ya mahitaji ya saruji nchini, na
hivyo kuwezesha kujitosheleza kabisa,” alisema waziri.
Kuhusu
fidia katika maeneo yaliyochukuliwa kwa ajili ya uwekezaji, Dk Kigoda
alisema kimsingi Serikali inawajibika kuwalipa fidia wananchi katika
maeneo hayo, itajaribu kukamilisha fidia hiyo mwaka 2014/15.
Aliyataja maeneo yenye kuhitaji fidia kuwa ni Kurasini Dar es Salaam, Bagamoyo, Ruvuma, Mtwara na Tanga.
Aliyataja
baadhi ya malengo ya mwaka 2014/15 ni kukamilisha Sheria ya Kusimamia
Biashara ya Chuma Chakavu na kuandaa kanuni zake, kuandaa Sera ya Taifa
ya Kumlinda mlaji na kuendeleza utekelezaji wa utaratibu wa kupima ubora
wa bidhaa zote mahali zinapotoka kabla ya kuingia nchini.
Katika mwaka wa fedha 2014/15, Wizara ya Viwanda na Biashara imeomba kutengewa jumla ya Sh 112,497,801,000.
CHANZO:HABARILEO
No comments:
Post a Comment