TIFFAN ENT

TIFFAN ENT

TUKO WANGAPI

TUKO WANGAPI

GLORY FREIGHT

GLORY FREIGHT

Wednesday, May 14, 2014

UNDP KUIWEZESHA TUME YA UCHAGUZI 


Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Maendeleo (UNDP), Hellen Clark akikabidhi moja ya kompyuta mpakato kati ya 60 kwa mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Mstaafu Damiani Luvuva, alipokutana na wakuu wa NEC, Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) pamoja na mabalozi wa nchi mbali mbali za Ulaya, Dar es Salaam jana. Kulia ni Mkurugenzi wa Uchaguzi kutoka NEC, Julius Malaba. Picha na Emmanuel Herman. (J M)
Dar es Salaam. Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) limeeleza nia ya kuisaidia Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ili ifanikishe matumizi ya mashine za kisasa za Biometric Voters Register (BVR) wakati wa uchaguzi mkuu ujao.
Mkurugenzi wa shirika hilo, Hellen Clark alitoa ahadi hiyo jana na kuongeza kuwa hata hivyo, matumizi ya mashine hizo yamechelewa kwani zilitakiwa zitumike tangu uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, muda uliobaki unahitaji utekelezaji ili zitumike mwakani.
Clark ambaye pia ni waziri mkuu wa zamani wa New Zealand, alisema hayo wakati akizungumza na wanahabari kuhusu ziara yake ya siku nne nchini.
Alisema alipokuja nchini mwaka 2010 alitembelea NEC na kuziona kompyuta zilizokuwa zikitumika kusajili wapigakura kuwa zilikuwa zinatumia mfumo uliopitwa na wakati.
“Natambua kuwa kuna mpango wa kuwenda kwenye mashine za BVR ambazo zitahusisha uchukuaji wa alama za vidole na mambo mengine, natambua kuwa uamuzi umeshachukuliwa kuhusu mfumo huo, umechelewa, lakini sasa utekelezaji unatakiwa,” alisema.
Kauli hiyo imetolewa siku chache baada ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kulitaarifu Bunge mjini Dodoma kuwa NEC inaendelea na maandalizi ya kupata vifaa vya kisasa kwa ajili ya zoezi la kuboresha daftari la kudumu la wapigakura.
Pinda alitoa kauli hiyo wakati alipokuwa akisoma hotuba kuhusu mapitio na mwelekeo wa kazi za serikali na makadirio ya matumizi ya fedha ya ofisi yake na ofisi ya bunge kwa mwaka 2014/15.
Katika hotuba yake, Pinda alieleza kuwa mfumo wa BVR utakaotumika ni tofauti na mfumo wa awali wa Optical Mark Recognition (OMR) ambao ulikabiliwa na changamoto nyingi za utendaji.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa NEC, Jaji Mstaafu Damian Lubuva akizungumza na gazeti hili hivi karibuni, alisema kuwa mashine za BVR zitatumika wakati wa uandikishaji wapigakura pekee yake.
Akizungumza kwa kujiamini, Hellen alisema Tanzania imeshafanya uchaguzi mara nne kwa mafanikio makubwa.
Alisisitiza kuwa UNDP ipo tayari kutoa msaada wowote wa kiufundi ingawa mpango huo ni wa kitaifa, lakini mradi wa wa shirika hilo unatoa nafasi kuisaidia NEC.
Clark ambaye ameshafanya ziara nne nchini, alisema kuwa wadau mbalimbali wanaoshirikiana na shirika lake wameshatoa dola 22 milioni sawa na Sh35.2 bilioni kusaidia mchakato wa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwakani.
“Hali kadhalika, tutashirikiana nanyi katika kuhakikisha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu wanashiriki kwenye uchaguzi huo,” aliongeza.
Hata hivyo, Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe wakati akiwasilisha taarifa ya kambi yake bungeni kwenye Bunge la bajeti mwaka jana, alimtaka Waziri Mkuu Pinda kuiamuru NEC kusimamisha maandalizi ya mfumo wa uchaguzi wa elektroniki hadi hapo itakapowashirikisha wadau.
Mbowe alisema tayari NEC imekiri kuanza maandalizi huku wadau wa uchaguzi vikiwamo vyama vya siasa hawajashirikishwa.
Ujangili Tanzania
Akieleza masuala aliyozungumza na Rais Jakaya Kikwete, Clark alisema kuwa alimwelezea changamoto za ujangili na umaskini aliouona alipotembelea Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, kwamba kuna umaskini mkubwa, njaa, watoto hawapati elimu ya kutosha na kinamama wajawazito wanakufa kwa sababu zinazoweza kuzuilika.
CHANZO, MWANANCHI

No comments:

Post a Comment