Maombi ya mikopo elimu ya juu 2014/2015 yafunguliwa
Mkurugenzi wa Habari,Elimu na Mawasiliano wa HESLB,Cosmas Mwaisobwa
Bodi ya
Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), imefungua maombi ya mikopo
kwa wanafunzi wanaotarajiwa kujiunga na Taasisi za Elimu ya Juu
zinazotambulika kwa masomo ya shahada mbalimbali kwa mwaka wa masomo
2014/2015.
Akizungumza
na waandishi wa habari katika ofisi za HESLB jijini Dar es Salaam jana,
Mkurugenzi wa Habari, Elimu na Mawasiliano wa HESLB, Cosmas Mwaisobwa,
alisema maombi ya mikopo ambayo yanafanyika kwa njia ya mtandao (Olas)
yamefunguliwa kuanzia Aprili 23 na yatafungwa rasmi Juni 30, mwaka huu.
Mwaisobwa
alisema kuwa Bodi inatarajia kupokea maombi ya mikopo kutoka kwa
waombaji wenye sifa zilizoainishwa kwenye mwongozo na vigezo vya utoaji
mikopo kwa mwaka wa masomo 2014/2015 ambao ulitolewa na Bodi na
kutangazwa kupitia magazeti na tovuti yake mwanzoni mwa Aprili, 2014.
Mwongozo
huo unataja sifa za msingi za waombaji mikopo kuwa wawe ni wahitimu wa
kidato cha sita, Stashahda na cheti cha elimu ya ufundi ((Tvet) hatua ya
sita, waliohitimu masomo yao kati ya mwaka 2012 na mwaka 2014
wanaotarajia kujiunga na elimu ya juu na wanaotarajia kuomba mikopo toka
Bodi ya Mikopo wanafahamishwa kuwa wanapaswa kutuma maombi yao ndani ya
kipindi kilichotajwa hapo juu.
Bodi
inatarajia kutoa mikopo kwa wanafunzi takriban 35,000 wa mwaka wa kwanza
watakaodahiliwa kujiunga na masomo katika vyuo mbalimbali vya elimu ya
juu.
"Pamoja
na kupewa fursa ya kuomba mikopo, waombaji wa mikopo wanapaswa
kuzingatia masuala ya msingi yanayoambatana na mchakato mzima ikiwa ni
pamoja na kusoma kwa umakini mwongozo na vigezo vya utoaji mikopo kwa
mwaka wa masomo 2014/2015 kabla ya kulipa ada ya maombi na kujaza fomu,
kusoma kwa umakini na kujaza vipengele vyote vya fomu kulingana na
maelekezo ili kuiwezesha Bodi kupata taarifa sahihi za mwombaji,"
alifafanua Mwaisobwa.
Aliongeza
kuwa ni muhimu kwa mwombaji mkopo kuambatanisha nyaraka zinazohitajika
kama vile cheti cha kuzaliwa, vyeti vya taaluma, vielelezo vya mdhamini
na uthibitisho wa nyaraka kutoka kwa mamlaka husika na mwisho kutuma
fomu kamili na viambatanisho kwenye Bodi ya Mikopo ili ziweze kupitia
kwenye mchakato wa uchambuzi na upangaji wa mikopo kwa wakati.
Aidha,
Mwaisobwa alieleza kuwa kuna mabadiliko machache yamefanyika ambapo
wanufaika wa mikopo wanaoendelea na masomo hawatakiwi kujaza tena fomu
kuthibitisha uhitaji wao wa mikopo kwa mwaka unaofuatia. CHANZO: NIPASHE (FS)
No comments:
Post a Comment