Waziri ajiua kwa kushindwa uchaguzi
Kabla ya kujiua, aliacha ujumbe kwamba amechukua hatua hiyo baada ya kutokea migongano ya kisiasa.
Wakati
Rais wa Malawi, Joyce Banda akizidi kuelemewa kwenye uchaguzi
uliofanyika Jumanne wiki hii, Naibu Waziri wa Serikali za Mitaa, Godfrey
Kamanya amejiua baada ya kubaini ameshindwa kutetea kiti chake cha
ubunge.
Kamanya alijipiga risasi nyumbani kwake mjini Lilongwe saa 9:30 asubuhi baada ya kupewa taarifa hizo kwa ujumbe mfupi wa simu.
Kabla ya kujiua, aliacha ujumbe kwamba amechukua hatua hiyo baada ya kutokea migongano ya kisiasa.
Kamanya
aligombea ubunge katika Jimbo la Nzonzi Kusini kupitia People's Party
(PP) na mwili wake ulikutwa chumbani kwake na ulipelekewa kuhifadhiwa
kwenye Hospitali Kuu ya Kamuzu.(P.T)
Taarifa nyingine zinaeleza kwamba waziri huyo alijiua kutokana na vitisho kutoka kwa mtu asiyefahamika.
Katika
matokeo yasiyo rasmi kutoka kituo cha kuhesabia kura cha Lilongwe
yaliyotolewa Jumatano asubuhi, mgombea huyo alikuwa ameshika nafasi ya
tano kati ya wagombea saba waliowania ubunge kwenye jimbo hilo.
Katika
matokeo hayo ya awali, Kamanya alipata kura 1,738 huku mgombea wa Malawi
Congress Party (MCP), Higton Jiya akiongoza kwa kura 4,625.
Wakati
tukio hilo likitokea, mke wa Kamanya alimpigia simu waziri wa zamani wa
usafirishaji, Ulemu Chilapondwa ambaye alikuwa rafiki ya mumewe na
kumweleza kuwa amesikia mlio chumbani wakati mlango umefungwa.
Kutokana
na taarifa hiyo, Chilapondwa alipofika nyumbani kwa marehemu akiwa na
watu wengine wawili walivunja mlango na kukuta mwanasiasa huyo ameshaaga
dunia baada ya kujipiga risasi kifuani.
Tukio
hilo limekuja wakati mgombea urais kupitia chama chake, Rais Joyce Banda
akiwa katika nafasi ya pili akiwa na asilimia 22 ya kura akigongana na
Lazarous Chakwera wa Malawi Congress Party (MCP). Anayeongoza ni mgombea
urais kupitia Democratic Progressive (DPP), Peter Mutharika kwa zaidi
ya asimilia 30.
Chanzo:Mwananchi
No comments:
Post a Comment