Tiketi za ndege ziliwekewa ‘cha juu’ mara 16 serikalini
Tuhuma
nzito za ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka zimezidi kuibuliwa
katika ofisi nyeti za Serikali, ikiwamo ya tiketi za ndege kuuzwa kwa
bei kubwa mara 16 zaidi ya nauli halisi.
Hayo yamo
katika Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG),
iliyotokana na ukaguzi maalumu wa hesabu za Serikali kwa kipindi
kinachoishia Machi 31, 2014 iliyowasilishwa bungeni juzi.
Katika
ukaguzi wake, sampuli 72 za tiketi za safari za nje zilichukuliwa katika
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Wizara ya Maliasili
na Utalii na zilipofanyiwa uchunguzi, ilibainika kuwa 56 sawa na
asilimia 72 zililipiwa zaidi na hivyo kupoteza Sh273.6 milioni za
walipakodi.
Badala ya Serikali kulipa Sh700.9 milioni kwa mawakala wa usafiri wa anga, ililipa Sh974.5 milioni.
Kwa
mujibu wa ripoti hiyo ya CAG, mawakala walitakiwa kutoza gharama ya
huduma kama ilivyo katika mikataba ya Wakala wa Huduma za Ununuzi
(GPSA), lakini walitoza viwango ambavyo ni zaidi ya vile vilivyoko
kwenye mikataba na hivyo Serikali kulipa zaidi.(P.T)
Sampuli
ya tiketi 22 zilizochukuliwa kati ya safari 239 za maofisa wa Wizara ya
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa zilionyesha pia kuwa, zilitozwa
zaidi ya kiwango kilichokubaliwa.
Matokeo
yake, taasisi za ununuzi zililipa Sh44 milioni badala ya Sh23.5 milioni
na hivyo kusababisha malipo ya ziada ya Sh20.5 milioni ambayo ni karibu
mara mbili ya gharama zilizotakiwa.
Ripoti
hiyo inasema uchunguzi wa sampuli ya safari 229 kutoka kwa wakala
mwingine kwenye wizara hiyo, unaonyesha kuwa pia zilitozwa zaidi ya
kiwango kilichokubaliwa. "Baadhi ya tiketi zilitozwa zaidi ya mara 16
ikilinganishwa na bei iliyowekwa kwenye mkataba na GPSA... Nusu ya
tiketi zilitozwa zaidi ya mara tatu ya bei iliyokubaliwa," inasomeka
sehemu ya taarifa hiyo.
Matokeo
yake, wizara hiyo ililipa Sh70.8 milioni badala ya Sh18.8 milioni ikiwa
ni ongezeko la Sh52.3 milioni, ambazo ni mara tatu zaidi ya kiwango
kilichokuwa kwenye mikataba.
Ripoti
hiyo ya CAG imebainisha kuwa kwenye sampuli ya tiketi 45 za safari za
nje, kulikuwapo fursa ambayo ingemwezesha wakala kuchagua bei kati ya
Sh488,250 hadi Sh46.3 milioni.
Hata
hivyo, bei iliyochukuliwa na mawakala ilikuwa ya kati ya Sh919,150 hadi
Sh40.3 milioni na kusababisha wizara kulipa kiasi cha Sh611.9 milioni
ingawa ingeweza kulipa Sh366.6 milioni.
"Serikali
ingeweza kuokoa Sh162.3 milioni... Kwa wastani nusu ya tiketi
zilizonunuliwa kwa safari za nje ziligharimu Sh2 milioni kila moja zaidi
ya kiwango cha chini kilichokuwapo," inasema taarifa hiyo.
Kutokana
na hali hiyo, CAG Ludovick Utouh katika taarifa yake alisema Mamlaka ya
Usafiri wa Anga (TCAA), haikuwa ikitimiza wajibu wake wa kisheria wa
kusimamia viwango vya nauli za usafiri wa anga.
"TCAA
hawakutambua majukumu yao ya kusimamia viwango vya nauli za ndege na
hivyo kusababisha mawakala kukosa msimamizi na hivyo kutoza nauli kadri
wanavyoona inafaa," alisema.
CAG
amependekeza Serikali kuimarisha uwezo wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana
na Rushwa (Takukuru) ili iweze kufanya uchunguzi na kubaini vitendo vya
rushwa katika ununuzi wa umma.
Chanzo:Mwananchi
No comments:
Post a Comment