TIFFAN ENT

TIFFAN ENT

TUKO WANGAPI

TUKO WANGAPI

GLORY FREIGHT

GLORY FREIGHT

Wednesday, May 7, 2014

Tanzania ya 9 duniani kwa uwezo mdogo wa kufikiri? 

Nimependa hii post ya makala.

 

logo31 7dafb
Kama ni kweli, haishangazi nchi kukosa mwelekeo
WIKI iliyopita niliandika kuhoji iwapo mambo kwenda shagalabagala hapa Tanzania, ni kwa sababu ya werevu wa chama tawala CCM au ni kwa sababu ya ujinga wetu Watanzania.
Nilipata mrejesho wa sms na barua pepe wa ajabu kidogo – wako waliokubaliana nami, na wako ambao si tu hawakukubaliana nami, lakini walinilaumu kwa kuwaita Watanzania 'wavivu wa kufikiri'; kana kwamba wamesahau kuwa wa kwanza kutamka hivyo alikuwa Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa!
Lakini kabla sijaenda mbali, nichukue fursa hii kusahihisha kosa nililolifanya katika makala hiyo. Nilitaja jina la Rais wa Zanzibar aliyesimamia mchakato wa mwaka 2010 kuirekebisha Katiba ya Zanzibar kwa kuingiza vifungu vilivyoudhoofisha Muungano kuwa ni Dk. Mohamed Shein wakati jina nililokusudia kuandika ni Amani Karume. Namuomba radhi sana Dk. Shein na wasomaji wangu kwa kosa hilo.
Nikirejea kwenye sms nilizotumiwa, kuna moja ilinisisimua kidogo; nayo inatoka kwa msomaji wangu mwenye simu namba 0754532797 ambaye aliandika hivi:

"Tatizo letu kubwa hapa Tanzania na mkuu wa maadui wetu kama taifa ni COLLOSAL MASS IGNORANCE. Ukweli ndugu yangu Mbwambo, hatutoki hapa tulipokwama labda miaka 50 ijayo."
Kilichonisisimua kwenye ujumbe wake huo ni mambo mawili. Kwanza, ameliita tatizo letu hilo kuwa ni ujinga wa kihalaiki, lakini pili; amesema kwamba hatutoki hapa tulipokwama labda miaka 50 ijayo? Mambo hayo mawili yanatafakarisha. Je, ni kweli wetu ni ugonjwa unaoitwa COLLOSAL MASS IGNORANCE? Na kama ndiyo, je, ni kweli hatuna namna tunaweza kutoka hapo labda mpaka baada ya miaka 50? Tafakari!
Hilo pembeni, kuna msomaji wangu mwingine alikubaliana na nilichokiandika, na hasa kile kilichosemwa na Profesa Kabudi kuhusu ujinga wa kizazi hiki cha sasa cha Watanzania, na kauli ya Rais Mstaafu Benjamin Mkapa kwamba Watanzania tu wavivu wa kufikiri.
Msomaji huyo alikwenda mbali na kunifahamisha ya kwamba Tanzania tunashika nafasi ya tisa duniani katika orodha ya mataifa yenye wananchi wenye bongo zenye viwango vya chini vya kufikiri – wenyewe huita IQ - yaani Intelligence Quotient. IQ hupimwa kwa kuangalia uwezo wa ubongo wa kupembua aina mbalimbali za taarifa.
Msomaji wangu huyo alinipa changamoto niitafute kwenye tovuti nijisomee mwenyewe jinsi Tanzania tunavyofahamika duniani kuwa tu taifa lenye wananchi wenye IQ za viwango vya chini.
Kwa shauku kubwa niliifungua linki hiyo na nyingine ya http/www.statisticbrain.com, na ndipo nilipokutana na ripoti yenye kichwa kinachosomeka: The Top 10 Countries With the Lowest Population IQ. Katika orodha hiyo sisi Tanzania tunashika nafasi ya tisa tukiwa na wastani wa kiwango cha IQ 72. Nafasi ya 10 inashikiliwa na Sudan ambayo pia kiwango chake ni 72.
Kwa mujibu wa orodha hiyo, Ghana inashika nafasi ya 8 kwa wananchi wake kuwa na kiwango cha chini cha IQ yaani 71. Nafasi ya saba ni Nigeria (67), nafasi ya sita ni Guinea (66), nafasi ya tano ni Zimbabwe (66), nafasi ya nne ni DR Congo (65), nafasi ya tatu ni Sierra Leone (64), nafasi ya pili ni Ethiopia (63) na nafasi ya kwanza ni Equatorial Guinea (59).
Mpenzi msomaji, sina hakika na ukweli wa utafiti uliofanywa ulioibuka na orodha hii, na wala sina sababu ya kuuamini kwa asilimia 100, lakini ninachotaka kusema ni kwamba tuna kila sababu Watanzania na Waafrika kwa ujumla kujadili suala hili na kujiuliza kulikoni? Ni kweli IQ zetu Watanzania (na Waafrika kwa ujumla) ni za viwango vya chini?
Kitu muhimu cha kufahamu ni kwamba upimaji IQ hauzingatii namna mtu anavyojibu maswali ya ujumla (yawe ya siasa, jiografia, sayansi nk); bali huzingatia upembuaji wa ubongo wa aina mbalimbali za taarifa na ujengaji hoja. Waingereza wanaita abstract reasoning.
Kama ni hivyo, je; ni kweli ukimchanganya Mtanzania na Mnyarwanda, Mkenya, na Mganda, na kisha kuwafanyia vipimo vya kisasa vya IQ kama vile Raven's Progressive Matrices au kile cha Wechester Adult Intelligence Scale, Mtanzania atashika nafasi ya mwisho kwa kuwa na kiwango cha chini?
Nauliza hivyo; maana nchi hizo tatu majirani zetu – Kenya, Uganda, Rwanda, na hata Zambia na Burundi hazimo kwenye orodha hiyo ya nchi 10 duniani ambazo watu wake wanaongoza kwa kuwa na viwango vya chini vya IQ. Na hiyo maana yake ni kuwa, tunazidiwa na nchi hizo kwa viwango vya kufikiri. Hicho ni kitu cha kutafakari. Natukitafakari basi ili kupata maelezo yenye mashiko.
Mwaka 2007 niliandika katika safu hii kulijadili suala hili baada ya mtafiti na mwanasayansi maarufu wa Marekani, Dk. James Watson, kutoa kauli inayoonyesha kuwa bongo zetu sisi watu weusi ni za viwango vya chini ikilinganishwa na bongo za Wazungu – kauli ambayo alikujashutumiwa nayo dunia nzima kwa kuitwa mbaguzi wa rangi.
Dk. Watson alisema hivi: Bara la Afrika halitoi matumaini ya kusonga mbele kimaendeleo kwa sababu sera zetu zote za kijamii zimewekwa katika msingi wa imani kwamba bongo zao (Waafrika) ni kama zetu Wazungu; ilhali vipimo vyote vya vinasaba vinaonyesha kuwa si sawa, hazifanani na zetu."
Hivyo ndivyo alivyosema mtafiti na mwanasayansi huyo. Kwa ufupi, anachosema ni kwamba bongo zetu sisi weusi ni dhaifu ukilinganisha na za Wazungu. Sasa, maneno hayo yangesemwa na Mzungu tu wa kawaida, tungeyapuuza moja kwa moja na kumwita mbaguzi wa rangi.
Lakini huyu Dk. Watson si Mzungu wa kawaida. Yeye ndiye aliyevumbua muundo wa chembechembe za nasaba (DNA) za binadamu, na pia ni mshindi wa tuzo inayoheshimika mno duniani ya Nobel, na kwa hiyo huwezi kumpuuza moja kwa moja bila kwanza kuwa na hoja nzito za kisayansi za kumpinga. Huo ndiyo ukweli mchungu kwetu sisi weusi.
Vyovyote vile, hicho alichokisema Dk. Watson miaka saba iliyopita sasa kimeungwa mkono na ripoti hiyo ya nchi 10 zinazoongoza duniani kwa wananchi wake kuwa na viwango vya chini vya IQ ambayo Tanzania tumo. Katika orodha hiyo, nchi zote 10 ni kutoka bara la Afrika.
Labda niijadili kidogo ripoti hiyo. Kwanza, ripoti hiyo inasema ya kwamba ni makosa kuhusisha viwango vidogo vya IQ moja kwa moja na suala la rangi ya mtu (mweusi au mweupe, Mzungu au Mwafrika nk).
Pili, ripoti hiyo inasema pia kwamba ni makosa kuhusisha moja kwa moja viwango vidogo vya IQ na suala la elimu tu, kwa sababu, mbali ya uduni wa elimu, IQ ndogo pia huchangiwa na mambo mengine kadhaa yakiwemo genes za wazazi, tamaduni, viwango vya lishe na afya za wahusika.
Kama hivyo ndivyo, swali la kujiuliza ni hili: Kama kiwango kidogo cha IQ hakihusiani na suala la rangi ya mtu, ni kwa nini Waafrika ndiyo tunaoongoza kwa kuwa na viwango vya chini vya IQ duniani?
Nadhani jibu lipo katika mseto wa mambo hayo mengine yaliyotajwa yanayochangia bongo zetu kuwa na IQ ndogo – yaani genes za mababu zetu, elimu duni, tamaduni zenye mila hovyo, viwango vidogo vya lishe, afya duni nk.
Kama mambo hayo ndiyo yalikuwa sehemu ya maisha ya babu zetu karne na karne zilizopita, haishangazi, basi, vizazi vya leo kuwa bado na IQ ndogo; maana si tu kwamba tuna genes zao katika miili yetu; lakini bado tumeendelea kuwa na elimu duni, afya duni na lishe duni ikilinganishwa na wenzetu Wazungu.
Kwa maneno mengine, ili isituchukue miaka mingine 50 kuondoka hapa tulikokwama kwa sababu ya uvivu wetu wa kufikiri na ujinga wetu, kama alivyoeleza msomaji wangu yule katika sms yake, ni muhimu kizazi cha sasa kupambana na mambo hayo yanayofanya sisi na wanetu na wajukuu na vitukuu vyetu kuwa na IQ ndogo – yaani tupambane na elimu duni, afya duni, lishe duni, mila duni nk!
Kwa mtazamo wangu, tusipofanya hivyo, tutaendelea kurithisha wanetu, vijukuu na vitukuu vyetu bongo zetu zenye IQ hafifu. Na tutaendelea kukasirika kila tafiti za Wazungu zitakapoibuka na "mapya" kuhusu uwezo wetu sisi Waafrika wa kufikiri.
Kwa bahati mbaya sana, tunawakasirikia watafiti wa kizungu wanapoibuka na tafiti hizo zinazotilia shaka uwezo wetu sisi weusi wa kufikiri, lakini kwa upande mwingine, ni hulka, matendo na mienendo yetu sisi wenyewe, na ya watawala wetu inayowajengea Wazungu (kina Dk. Watson) hoja kwamba uwezo wetu wa kufikiri una mushkeli!
Chukua mfano wa hapa Tanzania. Kwa miaka karibu 50 tumekuwa tukipokea misaada ya maendeleo ya mabilioni ya fedha kutoka kwa nchi za Scandnavia, lakini mpaka leo tumeshindwa kuzitumia fedha hizo kujiendeleza. Bado tunawaomba misaada hata ya kujenga choo!
Na hii inanikumbusha kauli iliyopata kutolewa na mama mmoja mwanaharakati wa Sweden. Mama huyo alisema kwamba alipokuwa akinyonyesha mwanawe wa kwanza, Serikali ya Sweden ilikuwa ikiipa Tanzania sehemu ya mapesa ya walipakodi ili iyatumie kujiendeleza.
Mama huyo akaendelea kusema ya kwamba, sasa mwanawe huyo amekuwa mkubwa - naye amezaa mtoto wake, lakini bado Serikali ya Sweden inaendelea kuipa Tanzania misaada ya maendeleo ya mabilioni ya fedha za walipokodi, na akahitimisha kauli yake kwa kuhoji: Ni nchi gani hii Tanzania isiyoweza kusimama yenyewe na kutembea yenyewe hata baada ya miaka 50 ya kusaidiwa?
Jibu la mama huyo liko katika aina ya watawala tulionao, na pia limo katika aina ya bongo tulizonazo watawaliwa. Unapokuwa na Rais anayefurahia kusafiri kila mara kwenda Ulaya kuomba misaada (tena daraja la kwanza) huku akiwa na msafara mkubwa, unatarajia nini kutoka kwake kuhusu dhana ya kujitegemea?
Unapokuwa na watawala wanaoigeuza nchi kuwa "shamba la bibi" kwa wawekezaji wa kigeni, na huku mikataba wakiifanya siri, na wakati huo huo wananchi wakiona ni sawa tu, na kwenye uchaguzi wanakichagua chama chake kwa sababu tu wanapewa pilau, kofia kanga, na vijisenti kidogo, kwa nini Wazungu wasiibuke na tafiti zinazotilia shaka uwezo wetu wa kufikiri?
Tunapokuwa na maliasili za kila aina – maji, madini, misitu, gesi asilia nk, lakini bado wanetu wanakalia mawe shuleni na wajawazito hospitalini wanajifungulia chini, kwa nini tusiamini tunapowekwa katika orodha ya nchi 10 duniani ambazo wananchi wake wana viwango vya chini vya IQ?
Tunapopiga makofi na kushangilia bila kutafakari (abstract reasoning) kila watawala wanapopanda majukwaani na kupiga blah blah za kisiasa; licha ya kufahamu kwamba walijiuzia kwa bei poa nyumba za serikali na mashirika ya umma, kwa nini kina Dk. Watson wasihoji uwezo wetu wa kufikiri?
Babu wa Loliondo anapoibuka na tiba yake ya 'kuoteshwa ya kikombe' na kudai inatibu ukimwi na kisukari, na sisi tunakimbilia kwake kwa mamilioni tukiongozwa na mawaziri wetu, kwa nini tushangae tafiti za kisayansi za kina Dk. Watson zikihoji ubora wa bongo zetu?
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anapokaa kimya wakati Katiba ya Zanzibar inarekebishwa kwa kuweka vifungu vinavyokiuka Katiba ya Muungano, na kisha Rais huyo huyo katika hotuba zake ajinadi kuwa ni 'mpenda Muungano' na ataulinda kwa uwezo wake wote, vipimo vya IQ zetu vitaonyeshaje kama sisi wananchi tunamshangilia katika hilo bila abstract reasoning?
Ndugu zangu, nihitimishe tena kama nilivyohitimisha wiki iliyopita kwa kusema kwamba; Profesa Palamagamba Kabudi alikuwa sahihi kabisa alipowatahadharisha hivi watawala wetu kuhusu mfumo wa Muungano unaotakiwa na wananchi katika Katiba mpya:
"Ujinga wa kizazi hiki tusidhani utakuwa ujinga wa kizazi cha kesho. Vizazi vijavyo vya Tanzania vitakuwa na ujinga wake. Ni vyema kuwawekea misingi lakini waje kuishi na ujinga wao kuliko kulazimisha ujinga wetu, kwa sababu ujinga wetu ndiyo amali yetu lakini kwa wengine siyo amali."
Tafakari.
Chanzo: Johnson Mbwambo, http://www.raiamwema.co.tz (HM)

No comments:

Post a Comment