BOSI WA UDA KUJIELEZA BUNGENI
Mgogoro
wa uwekezaji katika Shirika la Usafirishaji Dar es Salama (Uda)
umechukua sura mpya baada ya Bunge kuamua Mkurugenzi wa Simon Group
inayoendesha shirika hilo, Robert Kisena ahojiwe na Kamati ya Kinga,
Haki na Madaraka ya Bunge kutokana na kuingilia kati madaraka hayo.
Agizo
hilo lilitolewa na Spika wa Bunge, Anne Makinda alipokuwa akijibu hoja
iliyotolewa na Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika ambaye alitaka
tuhuma zilizotolewa na Kisena dhidi ya Bunge na wabunge zijadiliwe kwa
sababu ameingilia uhuru na kinga za Bunge kwa kuzungumza nje ya Bunge
masuala ambayo yametolewa maelezo na Serikali bungeni.
Hoja ya
Mnyika ilitokana na taarifa za baadhi ya magazeti yaliyotolewa Mei 19,
mwaka huu yakimnukuu Kisena akisema kuwa wabunge wa Dar es Salaam
wamehongwa na mfanyabiashara mmoja na kwamba kampuni yake inamiliki hisa
nyingi tofauti na majibu ya Serikali bungeni.
Akinukuu
majibu ya Serikali katika swali lililoulizwa na Mbunge wa Kawe (Chadema)
Halima Mdee, Mnyika alisema kuwa Serikali ililieleza Bunge kuwa
mgawanyo halali wa hisa za Uda upo kama ulivyosajiliwa kwa msajili wa
mashirika ya umma, kwamba shirika hilo linamilikiwa na Serikali na
Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.
Katika
kujenga hoja yake Mnyika alisema majibu hayo yalionyesha kuwa Uda ni
Shirika la Umma, jambo ambalo lilipingwa na Kisena kupitia mkutano wake
na waandishi wa habari, akisema Uda inamilikiwa na kampuni yake kwa
asilimia 76.
Alisema
kuwa mwekezaji huyo ameingilia haki, kinga na madaraka ya Bunge kinyume
na utaratibu na kuanza kuwatuhumu wabunge ambao walisema ukweli ndani ya
Bunge.
Mnyika
alisema uhuru wa Bunge wa mawazo umehojiwa nje ya Bunge kinyume cha
kanuni, kinga na haki za Bunge jambo ambalo ni hatari kwa mustakabali wa
Bunge.
"Mheshimiwa
Spika, naomba kutoa hoja na wabunge wenzangu naomba waniunge mkono ili
jambo hili liweze kujadiliwa ili Kamati ya Kinga, Haki na Madaraka ya
Bunge imuite na ahojiwe kikamilifu," alisema Mnyika.
Baada ya
hoja hiyo, wabunge wengi walisimama kwa pande zote bila ya kujali
itikadi zao za vyama wakiongozwa na wabunge wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Hata
hivyo, Spika Makinda alisimama na kuwataka waketi, ndipo akatangaza kuwa
suala hilo haliwezi kujadiliwa bungeni, bali kamati husika itamuita
Kisena na kumhoji.
Kisena
hakupatikana jana kuzungumzia suala hilo na hata alipopigiwa, simu yake
iliita bila ya kupokewa na alipotumiwa ujumbe wa maandishi hakujibu
CHANZO MWANANCHI.
CHANZO MWANANCHI.
No comments:
Post a Comment