UKAWA WAMPONZA ASKOFU KAKOBE

USHIRIKA
 wa wachungaji wa Kipentekoste nchini (PPFT) umemtaka Kiongozi Mkuu wa 
Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF), Askofu Zakaria Kakobe, 
kuacha tabia ya kutumia mwavuli wa dini kuhubiri chuki na uchochezi kwa 
wananchi.
Akizungumza
 juzi wakati wa kufunga semina ya viongozi wa dini wa Mkoa wa 
Kilimanjaro iliyofanyika katika ukumbi wa Umoja Hostel, Mwenyekiti wa 
Ushirika wa Wachungaji nchini, Askofu Ikongo alisema kauli za Askofu 
Kakobe zimekuwa za hatari na zinaweza kuliingiza Taifa kwenye machafuko 
ya kidini.
"Nchi 
yetu imekuwa na dalili za viashiria vya kutoweka kwa amani na utulivu, 
kutokana na baadhi ya viongozi wa dini kujiingiza kwenye siasa na kuanza
 kutoa kauli za kuashiria uchochezi na kupandikiza chuki kwa 
waumini…sasa umefika wakati sisi viongozi wa dini hatuwezi kunyamaza 
kwani tutaonekana na matamko yanayotolewa kiholela kwa kutumia mwamvuli 
wa upentekoste," alisema Askofu Ikongo.
Alisema 
Askofu Kakobe amekiuka uadilifu wake, kwani Aprili 20 mwaka huu katika 
kanisa lake la Mwenge, alitoa kauli kuwa atapambana hadi Tanganyika 
irudi hata kwa kukatwa kichwa, kauli ambayo inadhihirisha ugaidi.
Askofu 
Ikongo alisema kauli kama hiyo haistahili kutolewa na mtumishi yeyote wa
 Mungu, kwani mtu mwenye uwezo wa kusema hata akatwe kichwa sio wa 
kawaida bali ni mtu aliye na mafunzo ya kujitoa mhanga kama gaidi.
"Tunasikitishwa
 na kauli za Askofu Kakobe ambazo zinaweza kuliletea Taifa machafuko ya 
kidini…siku ya Pasaka Aprili 20 mwaka huu aligeuza mimbari kuwa jukwaa 
la siasa, kwa kuhubiri uchochezi kwa kudai; kila mtu anayepigania kurudi
 kwa Tanganyika, ana Mungu ndani yake,” alisema.
Kwa 
mujibu wa Askofu Ikongo, kauli hizo za Kakobe ni za kigaidi na zina nia 
ya kuvuruga amani ya Watanzania na kuliingiza taifa kwenye machafuko, 
ambayo yataharibu tunu iliyoachwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius 
Nyerere.
Alisema 
ni vyema viongozi wa dini wajikumbushe wajibu wao wa kuliombea Taifa, na
 kuwaongoza waumini wao kufuata yaliyo mema badala ya kugeuka sehemu ya 
kutumiwa na wanasiasa.(Martha Magessa)
        
Akifunga 
semina hiyo Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Grace 
Makiluli aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa huo Leonidas Gama, alisema 
inasikitisha kuona viongozi wa dini kutumiwa na wanasiasa, kwa kutoa 
kauli zinazowafanya wananchi kuhoji kama viongozi hao hawatumii dini 
kutekeleza malengo ambayo sio mema.
Alisema 
Serikali bado ina imani na viongozi wa dini, kwa wale wanaozingatia 
maadili na utume wao wa kuhakikisha amani iliyodumu kwa miaka mingi 
inadumishwa.
Aliwataka
 waumini kutowaunga mkono wanaotumia mimbari kuwa jukwaa la siasa kwa 
kutoa maneno makali yanayohatarisha amani na kupandikiza chuki miongoni 
mwa waumini na wananchi.
CHANZO:HABARILEO
No comments:
Post a Comment