Wagonjwa wa dengue wafikia 376
Na Hudugu Ng'amilo
Homa ya
dengue inaendelea kushika kasi nchini baada ya takwimu za Januari hadi
juzi kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, kuonyesha kuwa watu 376
wamekwishagundulika kuugua ugonjwa huo.
Mtaalamu
wa Ufuatiliaji wa Magonjwa wa wizara hiyo, Dk Janeth Mugamba alisema
hadi jana watu wawili walikuwa wamepoteza maisha, idadi ambayo alisema
inaweza kuwa kubwa zaidi endapo upimaji utafanyika katika kila wilaya.
"Pengine idadi inaweza kuwa kubwa zaidi kwa sababu wengi hawapimwi,
Ijumaa (kesho) tutatoa, taarifa zaidi," alisema.
Alisema
Wilaya ya Kinondoni ina wagonjwa wengi zaidi, ikifuatiwa na Ilala na
Temeke. Hata hivyo, alisema huenda wilaya zenye idadi ndogo ya wagonjwa
hazijaweza kupima na kubaini watu wenye maradhi hayo ikilinganishwa na
Kinondoni.
Juzi,
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid alisema hali ni mbaya
na wananchi wanatakiwa kuchukua hadhari wasipate maambukizi ya ugonjwa
huo.
Mtafiti
wa malaria, tabia za mbu na mazingira, wa Taasisi ya Afya ya Ifakara, Dk
Nicholas Govela alisema tayari wameshatuma maombi ya kufanya utafiti wa
kina kuwajua mbu wanaoeneza homa ya dengue nchini. "Utafiti huu
utasaidia kujua ni mbu kiasi gani wameathirika na virusi hivyo.
Tukifanya hivyo tutajua ukubwa wa tatizo, tutajua wanapatikana wapi
zaidi na virusi vyao vimetokea wapi," alisema.
Dk Govela
alisema ni lazima utafiti huo ufanyike ili kudhibiti maambukizi zaidi
ya homa hiyo akisema zipo sababu kadhaa zinazohisiwa kusababisha maradhi
hayo, ikiwamo ya wahamiaji kuleta virusi hivyo vinavyosababisha homa
hiyo na kuambukizwa kwa njia ya kuumwa na mbu.
"Ugonjwa
huu umeenea zaidi nchi za Amerika ya Kusini na Kusini mwa Bara la Asia.
Hapa kwetu mbu hawa walikuwapo lakini ugonjwa wa dengue haukuwapo kwa
kiasi hiki, ndiyo maana sababu zinazohisiwa zaweza kuwa ni wahamiaji,"
alisema.
Alisema
maambukizi ya homa ya dengue hutokea baada ya mtu mwenye ugonjwa huo
kuumwa na mbu hao aina ya Aedes Egyptiae na mbu hao wakichukua virusi,
huvisambaza kwa watu wengine. "Inawezekana tatizo ni kubwa zaidi ya hivi
inavyofikiriwa kwa sababu wanaokuja hospitali kupimwa na kugundulika ni
wachache, wengi wasiofika hawawezi kujulikana," alisema.
Makazi duni hatarini zaidi
Daktari
Kiongozi na Mtaalamu wa homa ya dengue, Mrisho Rupinda alisema watu
wanaoishi katika makazi duni wapo hatarini kuathiriwa zaidi kwa sababu
ya kuwapo kwa taka nyingi na madimbwi.
Alitoa
mfano wa wagonjwa wa kwanza wilayani Kinondoni, akisema walitokea maeneo
ya Kambangwa, Mwananyamala Komakoma ambako kulikuwa na madimbwi na
bwawa la maji.
"Wagonjwa
wengi huonekana zaidi kwenye makazi duni kwa sababu ya mpangilio mbovu
na kuzagaa kwa taka. Lakini pia maeneo mengine ambayo watu huhifadhi
maji kwenye matenki au ndoo kwa muda mrefu bila kuyafunika," alisema.
CHANZO MWANANCHI
CHANZO MWANANCHI
No comments:
Post a Comment