UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA WATENGEWA SH.5 BILLIONI

Waziri 
Mkuu, Mizengo Pinda jana aliwasilisha bungeni, bajeti ya ofisi yake na 
mfuko wa Bunge inayofikia Sh5.21 trilioni. Kati ya hizo, Sh5 bilioni 
zimetengwa kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliopangwa 
kufanyika baadaye mwaka huu.
Hayo 
yalielezwa bungeni jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu 
(Tamisemi), Hawa Ghasia wakati wa maelezo kuhusu kazi zilizotekelezwa 
mwaka 2013/2014 na mwelekeo wa kazi zitakazotekelezwa 2014/2015.
Ghasia 
alisema shughuli zitakazogharimiwa na fedha hizo ni pamoja na maandalizi
 ya masanduku ya kupigia kura, kupitia kanuni za uchaguzi na kuandaa 
fomu na nyaraka mbalimbali za uchaguzi.
Shughuli nyingine ni uhakiki wa majimbo ya uchaguzi huo ambayo ni vijiji, mitaa na vitongoji.
Malipo ya wabunge
Katika 
bajeti hiyo ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Sh132.6 bilioni zimetengwa kwa 
ajili ya Mfuko wa Bunge la Muungano, kati yake posho na mishahara kwa 
ajili ya Bunge (wabunge na watumishi wa Bunge) ikiwa ni Sh123.94 
bilioni.(P.T)
        
Kwa 
mujibu wa nyaraka za bajeti hiyo, wabunge peke yao wametengewa Sh102.317
 bilioni kwa ajili ya mishahara, posho za vikao na kujikimu na posho za 
safari ndani na nje ya nchi.
Kwa mwaka
 wa fedha unaomalizika Juni 30 mwaka huu, mishahara na posho za wabunge 
zilitengwa Sh93.37 bilioni, kati ya hizo posho zilikuwa Sh48.74 bilioni 
ikilinganishwa na Sh49.526 bilioni zilizotengwa katika bajeti 2014/2015,
 sawa na ongezeko la Sh800 milioni.
Usimamizi
 wa rasilimali watu na utawala ambayo ndiyo inayohusika na mishahara na 
posho kwa watumishi wa Bunge kwa mwaka wa fedha wa 2014/2015, umetengewa
 Sh21.6 bilioni.
Takwimu hizo zinaonyesha kuwa mishahara ya wabunge imetengewa Sh12.769 bilioni.
Safari za ndani
Posho za safari ndani ya nchi zimetengewa Sh11.192 bilioni wakati zile za safari za nje kwa wabunge zimetengewa Sh9.08 bilioni.
Posho 
hizo ambazo hazikatwi kodi ni karibu mara nne ya kiwango kilichotengwa 
kwa ajili ya mishahara yao ambayo ndiyo pekee hukatwa kodi.
Fedha za Maendeleo
Kati ya 
Sh8.7 bilioni zilizotengwa kwa ajili ya maendeleo, Sh2.9 bilioni ni kwa 
ajili ya ukarabati wa majengo ya Ofisi za Bunge, Sh5.9 bilioni ni kwa 
ajili ya programu ya kujenga miundombinu ya Bunge na programu ya 
kuimarisha Bunge imetengewa Sh755 milioni.
Chanzo:Mwananchi
No comments:
Post a Comment