Wananchi waomba Kituo cha Afya Simambwe kufanya kazi saa 24

WANANCHI 
wa Kata ya Tembela Wilaya ya Mbeya Vijijini wameiomba Serikali kusaidia 
kukiwezesha Kituo cha Afya Simambwe ili kifanye kazi saa 24 ili 
kuwasaidia muda wote wananchi wanaohudumiwa na kituo hicho hasa 
wajawazito.
Kauli
 za ombi hilo zimetolewa hivi karibuni kwa nyakati tofauti na wananchi 
hao walipokuwa wakizungumza na mwandishi wa habari hizi katika vijiji 
vyao alipowatembelea kuangalia changamoto anuai za huduma za kijamii 
vijijini Kata ya Tembela.
Mwenyekiti
 wa Kijiji cha Ilembo Usafwa, Richard Ngomela alisema licha ya kijiji 
hicho kuwa takribani umbali wa kilometa tatu na nusu kukifikia kituo cha
 afya Simambwe wanakitegemea hivyo kuomba wahudumu kufanya kazi saa 24 
ili wapate huduma muda wote.
Alisema
 kitendo cha kituo hicho kufanya kazi mchana pekee kimekuwa kikishindwa 
kuwasaidia wagonjwa wa usiku na hasa wajawazito jambo ambao limewafanya 
baadhi yao kuangaika nyakati za husiku kihuduma na wengine kujifungulia 
nyumbani.
“Kituo 
hiki kinafanya kazi mchana tu ukienda usiku inakuwa tatizo,” alisema 
Ngomela. Aliongeza kuwa nyakati za mchana wanapopata mgonjwa kijijini 
hapo hulazimika kumbeba kwenye sanduku na kutembea naye kwa miguu umbali
 wa kilometa tatu na nusu kumpeleka kituo cha Simambwe.
Mkazi wa 
Kata ya Tembela, Jestina Ndele alisema kutokana na Kituo cha Afya 
Simambwe kutoa huduma zake mchana tu imewapa shida baadhi ya wagonjwa 
hasa akinamama wajawazito ambao huitaji huduma ya uzazi/kujifungua 
nyakati za usiku hivyo wengine kulazimika kujifungulia nyumbani.
“…Unajua 
kujifungua huwezi jua utajifungua muda gani, yaweza kuwa mchana au 
wakati mwingine kuangukia usiku, sasa inapotokea hali kama hii usiku 
inatupa shida sana maana tunategemea kituo hicho tu ambacho kwa sasa 
kinafungwa saa kumi jioni hii imekuwa tatizo kwa wahitaji huduma za afya
 usiku,” alisema Bi. Ndele.
Mkazi wa 
Kijiji cha Usoha Njiapanda, Sikujua Jakobo alisema anashangaa kuona kuwa
 wamefanikiwa kuwa na kituo cha afya jirani lakini viongozi wanashindwa 
kuweka utaratibu wa kituo hicho kuweza kufanya kazi usiku kwa utaratibu 
maalumu ili kuwasaidia wanavijiji wanaokitegemea.
Akitolea 
ufafanuzi ombi hilo la wananchi, Ofisa Mtendaji wa Kata ya Tembela, 
Elias Kalinga alisema kituo hicho kinashindwa kufanya kazi usiku kwa 
kuwa mganga na wasaidizi wake wanakaa mbali na kituo hivyo kushindwa 
kutoa huduma baada ya saa za kazi za kawaida kumalizika.
Alisema 
licha ya kituo hicho kuwa na baadhi ya nyumba kwa ajili ya makazi ya 
mganga hazikuwa na hadhi ya kukaa mganga huyo pamoja na wasaidizi wake. 
“…Zipo nyumba tatu pale za kituo lakini kwa kweli hazina hadhi ya kukaa 
mtumishi Yule, kwanza madirisha na milango ilikuwa mibovu, hazina vyoo 
na jingo linguine lilikuwa kama gofu tu, hivyo mganga anakaa mbali yaani
 Igawilo,” alisema Kalinga.
Hata 
hivyo alisema kwa sasa utaratibu unafanywa wa kuzikarabati nyumba hizo 
na tayari baadhi ya wahudumu wa kituo wamekubali kuzitumia hivyo 
unaandaliwa utaratibu ambao utawawezesha wao kutoa huduma za dharura 
hata baada ya saa za kazi (usiku) kwa wananchi.
Mganga 
Mkuu wa Kituo hicho, Salome Mwaipopo alikiri kuwa nyumba zilizopo 
hazikuwa na mazingira mazuri ya kuishi wafanyakazi kituoni pale na 
juhudu zimeanza kufanywa ili kukiwezesha kituo hicho kuwasaidia wananchi
 kimatibabu hata baada ya saa za kazi
No comments:
Post a Comment