Waathirika wa mafuriko Kilosa watangaza vita
Waathirika
wa mafuriko wilayani Kilosa mkoani Morogoro wamejipanga kupambana
kishujaa, endapo mkuu wa wilaya hiyo, atatumia nguvu kuvunja makazi yao
ya muda.
Wananchi hao wamesema wako tayari kupambana ili kulinda haki yao baada ya Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Elias Tarimo, kuagiza waondoke kwenye makazi ya muda ili yavunjwe na bati zake zitumike kuezekea shule na kanisa.
Tangazo hilo limezua mgogoro baina ya waathirika hao zaidi ya 10,000 wanaoishi kwenye makambi ya muda yaliyoko Kilosa, Mazulia, Kondoa na Kimamba ambao nyumba na mali zao zilizolewa na mvua kwenye mafuriko ya mwaka 2010.
Waathirika hao walisema hawajapewa viwanja licha ya Rais Jakaya Kikwete, kuwatembelea na kuagiza wapatiwe viwanja na mabati ili kujenga makao ya kudumu.
MALALAMIKO
Wakazi hao waliiambia NIPASHE Jumapili kuwa, Tarimo, alitoa maamuzi ya kuvunja nyumba zilizojengwa kwa mabati baada ya kuafikiana na madiwani na wakuu wa vitengo wilayani hapo waliotaka mabati ya waathirika yatumike kuezeka Shule ya Msingi Mkondoa.
Kadhalika mabati mengine iliamuliwa yapelekwe kuezeka Kanisa la Anglikana la Magomeni ambalo litapatiwa mabati 20 kwa gharama ya Sh 80,000 sawa na Sh 4,000 kwa kila moja.
Walidai kuwa baada ya kufikia maamuzi hayo waamini wametangaziwa makanisani kuwa kila mmoja atachanga Sh. 1,000 ili kupata Sh 80,000 za kuyanunua mabati hayo.
Baadhi ya wakazi hao walidai kuwa mkuu wa wilaya hiyo aliagiza pia makazi hayo yavunjwe ili kupata mabati ya kuzungushia
uzio wa kiwanja kitakachotumiwa wakati wa mbio za Mwenge za mwaka huu.
MIKAKATI YA KUWAONDOA
Baadhi ya waathirika walidai maamuzi hayo yalifanyika wakati wa kikao cha viongozi wa wilaya, mwenyekiti wa madiwani wa wilaya ya Kilosa Amiri Mwarabu, aliwatangazia wananchi hao kuondoka akikaririwa na Redio ya Jamii.
Alisema watu 10,000 wanaoishi kwenye kaya 1,500 watatakiwa kuondolewa kwenye makao ya muda ili wajanja wafaidi mabati.
Alieleza kuwa mabati hayo yalitolewa na wahisani walioahidi pia kuwajengea nyumba waathirika hao.
WATANGAZA VITA
Baada ya kusikia tangazo hilo wananchi walicharuka na kukaa kikao cha dharura na kuandaa silaha za jadi zikiwamo rungu, mapanga na matairi kwa ajili ya kushambulia na kuchoma watu watakaowavamia ili kubomoa mabanda yao.
Mwarabu alidaiwa kuwa alitangaza kuwa baada ya siku ya Mei Mosi askari watapita kubomoa nyumba za waathirika hao na kuwataka kuondoka mara wasikiapo tangazo hili na hakuna muda mwingine wa kisheria wa kuendelea kukaa.
Baada ya kutoa notisi hiyo Mwenyekiti wa Waathirika wa mafuriko Matthew Gervas , alisema walifanya kikao na kuamua kuipeleka serikali hiyo mahakamani kwa kuchoshwa na vitisho vya kila wakati kutoka kwa viongozi wa wilaya.
Alisema wakati wanapata matatizo ya mafuriko hayo Mkuu wa Wilaya alikuwa Halima Dendegu,aliyewatia moyo ikiwa ni pamoja na kuwafariji na kuwasisitiza wasirudi mabondeni kwani serikali itakuwa na kazi ngumu ya kuwaokoa.
MKUU WA WILAYA AFUNGUKA
Akiongea na NIPASHE Tarimo alisema mabanda yatakayobomolewa ni yale yasiyokuwa na watu ili kuondoa wahalifu hasa wavuta bangi, machangudoa na vibaka wanaojificha mabandani humo.
Alipoulizwa sababu za kuchelewa kuwapatia waathirika hao viwanja kama ilivyoagizwa na Rais alisema mchakato haujakamilika lakini huenda wakavipata mwishoni mwa mwezi ujao.
MKUU WA MKOA
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Joel Bendera akizungumzia sakata hilo alisema hana taarifa za kimaandishi kuwa wahanga hao watabomolewa makazi yao.
Alisema serikali inafanya kazi kwa mujibu wa sheria na kwamba hajaelezwa sababu za kuwafukuza watu wasio na makazi kwenye maeneo walikohifadhiwa kisheria.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
No comments:
Post a Comment