TIFFAN ENT

TIFFAN ENT

TUKO WANGAPI

TUKO WANGAPI

GLORY FREIGHT

GLORY FREIGHT

Sunday, May 18, 2014

‘KUNA DALILI BUNGE LA KATIBA LITAPORA MAMLAKA YA WANANCHI

bu_2adac.jpg
Bunge la Katiba limesitishwa kwa muda baada ya kukutana kwa takribani miezi miwili na nusu na kufanya mijadala muhimu inayolenga kuboresha rasimu ya katiba.
Mjadala wa Rasimu ya Katiba hiyo yenye ibara 271 na viambatanisho vinane limetawaliwa na changamoto nyingi, ikiwemo baadhi ya wajumbe kutoka Kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kujitoa.
Kujitoa kwa Ukawa kumedaiwa kutokana na kupinga mwenendo wa bunge hilo, kutawaliwa na matusi, vitisho, kashfa, ubaguzi na pia kuwekwa pembeni Rasimu ya Pili ya Katiba iliyowasilishwa katika bunge hilo na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Mwenendo wa bunge hilo, sasa umeziamsha Asasi za Kiraia (Azaki) zaidi ya 1,000 na kuamua kutoa tathmini ya mwenendo wa bunge hilo.
Mwenyekiti wa Azaki katika masuala ya Katiba, Irinei Kiria na katibu wake, Onesmo Ole Ngurumwa katika tathmini ya umoja huo, wanaeleza kutoridhishwa na mwenendo wa Bunge la Katiba.
Ole Ngurumwa ambaye ni Mkurugenzi wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za binadamu (THRDC) kwa niaba ya Azaki anazungumza na gazeti hili na kufafanua msimamo wa Azaki unaotokana tathmini ya Mchakato wa Katiba na kuangalia tulikotoka, tulipofikia na tunakoenda.
"Tathmini ya Azaki imejikita katika kuangalia zaidi Mwenendo wa Mchakato wa Katiba hasa hatua ya sasa ya mjadala katika Bunge la Katiba na pia hatua inayofuata ya kupitisha katiba pendekezwa kwa njia ya kura ya maoni," anasema Ole Ngurumwa.
Anafafanua kuwa, mwenendo wa sasa wa Bunge la Katiba umelenga kutoa msimamo wa Azaki katika Mchakato wa Katiba, kushauri na kukemea yale ambayo yanayoweza kuwakosesha Watanzania fursa ya kupata katiba waitakayo na kwa muda mwafaka.
"Tunafahamu kabisa katiba yoyote ile ni lazima ipate uhalali kwa makundi yote katika taifa ili iweze kutekelezeka na njia nzuri ya kupata katiba itakayokuwa na sura ya kitaifa ni kuandaa sheria na taratibu shirikishi na kuziheshimu"anasema Ole Ngurumwa.
Anaeleza kuwa ni muhimu sana, wajumbe wa Bunge la Katiba. kuheshimu ngazi zote za kisheria katika mchakato pamoja na kuzingatia suala la maridhiano ni njia nzuri ya kupata katiba yenye ridhaa ya wananchi wote.
Msimamo wa Azaki
Ole Ngurumwa anasema kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo ndiyo inatumika sasa Ibara ya 8(1) (a) wananchi ndio msingi wa mamlaka yote na serikali itapata madaraka na mamlaka yake yote kutoka kwa wananchi
Anaeleza kuwa tofauti na michakato yote ya kupata katiba iliyokwishafanyika miaka ya nyuma, mchakato wa sasa ni wa kwanza na wa kipekee ambao umetambua na kuyatafuta maoni ya wananchi katika kupata katiba ya nchi yao.
"Kimsingi mchakato huu ambao ni mwitikio wa madai ya wananchi kwa miaka mingi na kuanzishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano Jakaya Kikwete unakidhi matakwa ya Hati ya Makubaliano ya Muungano kama inavyojieleza katika ibara yake ya saba," anasema Ole Ngurumwa.
Ole Ngurumwa anasema Azaki zinaamini kuwa, katika mchakato huu, Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilikusanya na kuchambua maoni ya wananchi ambayo yametoa taswira ya kile ambacho wananchi wamesema wanakitaka.
Kwa nini wanatetea Rasimu ya Pili
Ole Ngurumwa anasema Azaki zinatetea Rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, kwani hadi sasa hakuna maoni yoyote ambayo kisheria yanapaswa kufanyiwa kazi na Bunge la Katiba zaidi ya yale yaliyomo kwenye Rasimu ya Pili ya Katiba.
"Kwa kuwa wananchi waliotoa maoni ndio msingi na chimbuko la madaraka yote na mamlaka ya nchi na ni kwa kupitia rasimu hii wananchi wametamka Muundo wa Uongozi namna ya kuwapata na kuwawajibisha viongozi na wamegawanya madaraka kwa viongozi wao," anasema Ole Ngurumwa.
Haturidhishwi na mwenendo wa Bunge
Ole Ngurumwa anasema Azaki, zinaamini kuwa majadiliamo bungeni yamekosa utashi wa utaifa kutokana na baadhi ya wajumbe kupoteza moyo wa maridhiano na kuheshiminiana. Ole Ngurumwa anasema Mwenendo mzima wa Bunge Maalumu la Katiba kuchukua sura ya ubinafsi na yenye maslahi ya kivyama zaidi na kusahau masilahi ya Watanzania na mustakabali wa Taifa.
Anasema mwenendo wa kusuasua unaotia shaka unaonesha kuwa wapo Watanzania wenzetu wasio na nia njema ya kufanikisha katiba mpya kwa muda muafaka na hivyo ucheleweshaji wa makusudi unalenga kufanikisha malengo hayo.
Katibu huyu anafafanua kuwa, wamebaini uwepo wa mazingira na kila dalili ya kutaka kulipa Bunge la Katiba madaraka makubwa yasiyostahili ya kutupilia mbali rasimu hii ya wananchi na kuja na rasimu inayopendekezwa na watawala.
Anasema Azaki haziridhishwi na lugha ya vitisho na ubaguzi kwa wananchi na hata kwa wajumbe wa Bunge la Katiba wenye misimamo huru na hasa kwa wale wanaosimama na kutetea maoni ya wananchi.
"Vitisho hivi ni pamoja na kauli ya Rais Jakaya Kikwete na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera na Uratibu, William Lukuvi kuwa muundo wa serikali tatu, unaweza kutoa mwanya kwa jeshi litapindua nchi, "anasema
Wito
Anasema kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Sura ya 83 Toleo la 2014, kifungu cha 27(2), Bunge la Katiba na wajumbe wake wanapaswa kuwa huru katika kujadili na kupendekeza katiba mpya.
"Ni muhimu tutambue kuwa kati ya wananchi milioni 45, wenye itikadi za vyama hawafiki milioni saba, hivyo ni kosa kubwa kugeuza mjadala wa Bunge la Katiba kuwa Uaja wa siasa za vyama badala ya kujadili Katiba," anasema.
Anasema bunge halina mamlaka ya kubadili mambo ya msingi ya katika Rasimu ya Katiba. "Bunge linakosa uhalali huo kwanza kutokana na muundo wa mchakato wa uandaaji wa Katiba hapa nchini. Muundo wetu umekuwa shirikishi na kuundwa kwa tume kwa ajili ya kukusanya maoni ya wananchi tayari kumelipunguzia Bunge madaraka makubwa," anasema.
Anasema kwa maana hiyo Bunge hili halina mamlaka ya kubadili rasimu hii zaidi ya kujadili, kuboresha na kuongeza masharti ya mpito. Pili, Kifungu cha 25 cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83 imeweka bayana kuwa Bunge lina madaraka tu ya kujadili na kupitisha masharti ya katiba, .(E.L)

No comments:

Post a Comment