SERIKALI KUFUTA MISAMAHA YA VAT
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi. Picha na Maktaba
Dar es Salaam. Serikali itawasilisha bungeni rasimu ya maboresho ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ambayo itafuta misamaha ya kodi hiyo.
Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi
alisema jana kwamba mpango huo unafanyiwa uchambuzi na Serikali na
kwamba utawasilishwa katika Bunge la Bajeti wiki mbili zijazo.
Kwa
nyakati tofauti, mwenyekiti wa CUF ambaye pia ni mtaalamu wa uchumi,
Profesa Ibrahim Lipumba alikuwa akipigia kelele juu ya wingi wa misamaha
ya kodi akisema imekuwa ikipoteza kiasi kikubwa cha mapato ya Serikali.
Profesa
Lipumba alisema hivi karibuni kuwa ili kuondoa kasi ya ukuaji wa nakisi,
Serikali inatakiwa kufuta kabisa misamaha holela ya kodi inayofikia
Sh1.8 trilioni ambayo ni sawa na asilimia tano ya pato la taifa.
Siku tano
zilizopita, Waziri wa Fedha, Saada Mkuya, wakati akiwasilisha mpango wa
Bajeti ya mwaka 2014/15 kwa wabunge, alisema Serikali imepanga
kukamilisha utungwaji mpya wa Sheria ya VAT.
Alisema
hatua hiyo itakwenda sambamba na kuongeza wigo wa kodi kwa kuimarisha
vyanzo vilivyopo na kuanzisha vyanzo vipya pamoja na kurasimisha sekta
isiyo rasmi ili iingie kwenye mfumo rasmi wa kodi.
Katika bajeti ya mwaka 2013/14, Serikali iliondoa msamaha wa VAT kwa viwanda vya nguo vinavyotumia pamba ya ndani.
Kwa
mujibu wa ripoti ya utafiti ya taasisi ya CRC Sogema ambayo inaishauri
Wizara ya Fedha, misamaha chini ya Kodi ya VAT ilifikia Sh802 bilioni
kwa mwaka 2012, wakati jumla ya misamaha yote ilikuwa Sh1.8 trilioni.
Ripoti
hiyo ya mwaka 2013 inasema: “Matokeo ya utafiti huu muhimu yanapendekeza
kuwa kuna ufanisi zaidi kwa nchi zinazoendelea kujikita zaidi katika
kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji kuliko kutoa misamaha ya kodi kwa
mashirika.”
Jana,
Lukuvi alisema: “Serikali ina mpango huo na hivi sasa rasimu ya VAT bado
inaandaliwa na jambo hilo lipo mikononi mwa Mwanasheria Mkuu wa
Serikali.”
Hata
hivyo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema hakupatikana
jana kuzungumzia hatua iliyofikiwa katika maandalizi ya rasimu hiyo.
Wasomi watofautiana
Hatua
hiyo imepokewa kwa mitizamo tofauti na baadhi ya wachumi, wengine
wakisema itaongeza mapato ya Serikali tofauti na ilivyokuwa awali na
wengine wakisema itawaumiza zaidi wananchi.
Profesa
wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Humphrey Moshi alisema ni
hatua nzuri ambayo itaongeza mapato kwa Serikali kwa sababu taasisi
nyingi zilikuwa zikitumia vibaya misamaha hiyo.
“Fedha
zitakazopatikana zitumike vizuri kwa kugharimia miundombinu, kutoa
huduma bora za elimu na afya na si posho na vikao visivyo na tija,”
alisema.
Alisema
hata kama Serikali itaondoa misamaha hiyo, bado ina wajibu wa kufanya
uchambuzi wa kina na kuujulisha umma kuwa ni taasisi gani zilitumia
vibaya misamaha hiyo.
Hata
hivyo, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (Sua),
Dk Damian Gabagambi alisema hatua hiyo ikifanikiwa itaathiri jamii kwa
kuwa baadhi ya taasisi zilizokuwa zinasamehewa kodi zilikuwa zikisaidia
kwa kiasi kikubwa.
Alisema
Serikali na baadhi ya watu wanaopinga misamaha ya kodi wamekuwa
wakiangalia upande wa gharama au hasara inayotokana na misamaha hiyo
bila kuangalia faida zake.
“Nipo
tofauti kabisa na wanaounga mkono hatua hiyo; kwa sababu taasisi nyingi
kama mashirika ya dini yamekuwa yakitoa huduma nzuri kwa wananchi.
Wasikurupuke kuondoa misamaha kwa kuwafurahisha watu,” alionya Dk
Gabagambi.
Alisema
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilishindwa kufanya uchunguzi wa kina
kugundua ni kina nani waliokuwa wakitumia vibaya misamaha hiyo kutokana
na usimamizi mbovu.
“Unapokuwa
umetoa misamaha ni lazima uweke mifumo mizuri ya ufuatiliaji kubaini
watu watakayoitumia vibaya, lakini TRA hawatumii mfumo huo,” alisema.
Alisema
iwapo Serikali itafuta misamaha hiyo kuna uwezekano mkubwa wa kuwepo
madhara makubwa katika uwekezaji, ajira na huduma kwa jamii kwa kuwa
baadhi ya mashirika yanayosamehewa kodi yalikuwa yanaajiri watu wengi na
kutoa huduma nzuri.
Serikali
imekuwa ikitafuta vyanzo mbalimbali vya mapato na moja ya ha Mkakati
mwingine ni kuanzisha kodi ya kila mwezi ya matumizi ya kadi za simu
ambao haukufanikiwa kutokana na kupingwa na wadau mbalimbali. CHANZO: MWANANCHI (FS)
No comments:
Post a Comment