TIFFAN ENT

TIFFAN ENT

TUKO WANGAPI

TUKO WANGAPI

GLORY FREIGHT

GLORY FREIGHT

Wednesday, May 21, 2014

"MADENI YA WALIMU KULIPWA KABLA YA JULAI" 

bunge-dom_467c7.png
SERIKALI imesisisitiza kuwa italipa madeni ya malimbikizo ya mishahara ya walimu kabla ya kumalizika kwa mwaka huu wa fedha, 2013/14. Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Kassim Majaliwa, alieleza hayo bungeni juzi jioni wakati akichangia mjadala wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
Bunge lilipitisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2014/15 ya Sh bilioni 799 zikiwamo Sh bilioni 344.2 za matumizi ya kawaida na Sh bilioni 454.8 kwa ajili ya maendeleo.(Martha Magessa)
Majaliwa alisema madeni ya walimu yalielezwa kufikia Sh bilioni 61 na kwamba kumekuwa kukifanyika uhakiki, na kwa baada ya uhakiki, Februari mwaka huu, walilipa Sh bilioni 19.
“Lakini pia Machi na Aprili tayari kuna fedha nyingine zimelipwa, kwa bahati mbaya sikuja na takwimu hapa, lakini Serikali itahakikisha kuwa madeni yote yanalipwa katika mwaka huu wa fedha kabla haujamalizika,” alisema Majaliwa.
Aidha, alisema fedha nyingine za malimbikizo yakiwamo ya likizo, matibabu, usafiri na masomo zinalipwa kwa kupitia katika halmashauri husika.
Kuhusu ujenzi wa nyumba za walimu, alisema tayari nyumba 1,200 zinajengwa ambapo kati yake 268 zimekamilika na zimetengwa Sh bilioni 200.
Kuhusu fedha za chenji za rada, Naibu Waziri alisema hadi sasa zimeshanunulia madawati 93,988 ambayo yatagawanywa 600 kwa kila halmashauri katika awamu ya kwanza na awamu ya pili madawati 400.
Akizungumzia walimu kuwa na waajiri tofauti, alisema mwajiriwa wa walimu ni Katibu Mkuu Tamisemi, na katika ngazi ya mikoa wako chini ya Katibu Tawala wa Mkoa (RAS) na katika Halmashauri, kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya (DED).
Akichangia hoja hiyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia alisema walimu wanaona unafuu zaidi tangu wawe chini ya Tamisemi, huku akiwataka wabunge kuacha kupotosha dhana ya kuchangia maendeleo.
Naye Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa, alitetea uamuzi wa kubadili madaraja ya ufaulu, akisema si kitu kigeni duniani. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Celina Kombani, aliahidi kukutana na wadau ili kujadili kuundwa kwa chombo kimoja cha kushughulikia masuala ya walimu.
CHANZO:HABARILEO

No comments:

Post a Comment