HOFU YA MABOMU YATAWALA MEI MOSI ARUSHA
Na Mwandishi Wetu, Arusha
MATUKIO matatu ya milipuko ya mabomu yaliyotokea katika Jiji la Arusha ndiyo yaliyotawala Sherehe za Mei Mosi jijini hapa ambapo wafanyakazi wamesema yanawatia hofu hata katika uwajibikaji.
Wakizungumza katika risala yao, wafanyakazi hao walisema kwa kuwa matukio hayo yanatokea bila kutarajia, wakazi wengi wa jiji hilo hawana amani na kwamba wafanyakazi nao wanashindwa kutimiza wajibu wao.
"Ndugu zetu, wafanyakazi wenzetu wamepoteza maisha na wengine wamejeruhi kwa milipuko hii, tunashindwa kufanya kazi kwa amani kwa sababu hatujui ni wapi yatakapotokea tena," walisema.
Mbali ya kuiomba serikali ifanye jitihada kuzuia matukio hayo, wafanyakazi hao wamehoji ni wapi vijana wa Jeshi la Mgambo wanapelekwa baada ya kuhitimu mafunzo yao, kwani jeshi hilo ni muhimu katika ulinzi wa taifa.
Walisema ingawa vijana wengi wanahitimu mafunzo, lakini hakuna mahali popote ambako wanapelekwa kufanya kazi, jambo ambalo linadidimiza uchumi wa nchi na kuwanyifa vijana hao fursa za ajira.
"Tunaihoji serikali, ni wapi hata vijana hawa wanapaswa kuripoti, maana hakuna hata ofisi ambayo inashughulika na mgambo hawa," walisema.
Mgeni rasmi katika sherehe hizo, Mkuu wa Mkoa wa Arusha Magesa Mulongo, alisema kwamba mabomu yaliyolipuliwa siyo ya kigaidi bali yametengenezwa kienyeji.
Alisema vyombo vya usalama kwa kushirikiana na vile vya kimataifa vimebaini kwamba bomu lililolipuliwa kwenye baa ya Arusha Night Club halikuwa la kigaidi, bali limetengenezwa kienyeji na kwamba yawezekana miongoni mwa Watanzania wapo wenye nia mbaya ya kuua wenzao.
"Interpol wametuambia wazi kwamba, wamechunguza na kuona bomu hilo siyo la kigaidi, ni la kienyeji, hivyo wametuambia tuulizane wenyewe ni akina nani wenye mchezo huo mchafu," alisema.
Hata hivyo, sherehe hizo zilipambwa na matukio mbalimbali yakiwemo maonyesho ya mbwa wanaofunzwa kukamata wahalifu pamoja na dawa za kulevya.
No comments:
Post a Comment