Askari
wa Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI), tayari wapo Arusha
kushirikiana na polisi ili kuchunguza tukio la mlipuko wa bomu la kutupa
kwa mkono kwenye mkutano wa kampeni za Chadema.
Katika
tukio hilo lililotokea Juni 15, mwaka huu Viwanja vya Soweto, eneo la
Kaloleni, Arusha, watu wanne walipoteza maisha huku zaidi ya 60
wakijeruhiwa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Lebaratus Sabas, alithibitisha ushiriki wa FBI katika upelelezi huo.
Licha
ya FBI, polisi wanashirikiana na wenzao kutoka nchi jirani ya Kenya,
ambao wana uzoefu na matukio ya milipuko ya mabomu yanayotokea nchini
mwao mara kwa mara, hasa baada ya nchi hiyo kupeleka wanajeshi nchini
Somalia kukabiliana na Kundi la Al-Shabaab.
“Tunaendelea
na uchunguzi wa kina mlipuko wa bomu Soweto, tayari wenzetu wa FBI na
polisi wa Kenya wamefika kushirikiana nasi, nachukua fursa hii kuwaomba
wenye ushahidi utakaosaidia upelelezi kujitokeza,” alisema Sabas.
Serikali
imetangaza zawadi ya Sh100 milioni kwa yeyote atakayetoa taarifa
itakayosaidia kumpata aliyehusika, au wanaohusika na mlipuko huo.
Sabas alisema watu watatu waliokuwa wakishikilia na polisi kwa mahojiano kuhusu bomu hilo, tayari wameachiwa kwa dhamana.
Hii ni mara ya pili maofisa wa FBI na polisi kutoka Kenya kushiriki uchunguzi wa mlipuko wa bomu Arusha.
Mara
ya kwanza walishiriki kuchunguza mlipuko uliotokea kwenye Kanisa la
Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, eneo la Olasiti iliyotokea Mei 5, mwaka
huu.
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, bomu lililolipuka Soweto ni la kijeshi na limetengenezwa nchini China.
Uchaguzi
wa madiwani kata nne za Elerai, Kimandolu, Themi na Kaloleni,
uliahirishwa hadi Juni 30, mwaka huu kabla ya kusogezwa mbele tena hadi
Julai 14, kwa kile kilichoelezwa na Mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian
Lubuva, kuwa sababu za usalama.
Wakati
huohuo, Serikali imetangaza kugundua mtandao wa milipuko ya mabomu
yaliyotokea Kanisa la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, eneo la Olasiti na
Viwanja vya Soweto, Arusha.Pia, iliahidi kuwachukulia hatua stahiki
wahusika wote bila kujali cheo, umaarufu wala nafasi yake kisiasa.
Tamko hilo lilitolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Arusha,
Magessa Mulongo, alipozungumza kwenye kikao cha Baraza la Ushauri Mkoa
(RCC).
Mulongo alisema uchunguzi umegundua kuwa mipango ya milipuko ya mabomu yote mawili ya Olasiti na Soweto, ilifanyika Arusha.
Hata hivyo, Mulongo hakutoa ufafanuzi na kwamba, Serikali
imefanikiwa kujua mtandao unaohusika na milipuko hiyo baada ya kupata
maelezo kutoka kwa raia wema waliojitokeza kutoa taarifa baada ya
matukio hayo.
Mwananchi:
No comments:
Post a Comment