CAVANI ATAMBULISHWA RASMI PSG
Mshambuliaji, Edinson Cavani (HM)
HATIMAYE Paris St Germain imekamilisha
usajili wa mchezaji ghali, mshambuliaji wa Napoli, Edinson Cavani kwa
ada ya uhamisho ya Pauni Milioni 55 kwa Mkataba wa miaka mitano.
Cavani amekuwa akiwaniwa na klabu
kadhaa kubwa Ulaya majira haya ya joto, zikiwemo Manchester City,
Chelsea na Real Madrid nazo zilihusishwa na kugombea saini ya
mshambuliaji huyo wa Uruguay.
Pamoja na hayo, mabingwa wa Ufaransa
walipiga kasi wiki iliyopita na jana mchana wametangaza rasmi kwenye
tovuti yao kwamba wamemsajili mchezaji huyo.
Cavani amekuwa tishio tangu ajiunge na
Napoli akitokea timu nyingine ya Italia, Palermo Julai 2010, akifunga
mabao 104 katika mechi 138 alizocheza Partenopei.
Aliisaidia mno Napoli kushika nafasi ya pili katika Ligi Kuu Italia, Serie A akiibuka mfungaji bora kwa mabao yake 29.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka
26 anayesajiliwa kwa bei mbaya zaidi majira haya ya joto, anaungana na
wachezaji wengine bora waliosajiliwa awali na timu hiyo, Zlatan
Ibrahimovic, Marco Verratti, Ezequiel Lavezzi, Lucas Moura, Javier
Pastore na Thiago Silva.
Cavani anatarajiwa kutengeneza pacha
kali ya ushambuliaji kwa pamoja na Ibrahimovic, ambaye alishinda tuzo ya
Mchezaji Bora wa Mwaka wa Ligue 1 baada ya kufunga mabao 30 msimu
uliopita.
Kocha mpya wa PSG, Laurent Blanc pia
atatumai Cavani na mchezeshaji Lavezzi wataendeleza ushirkkiano wao
mzuri waliokuwa nao Napoli. Chanzo: binzubeiry
No comments:
Post a Comment