TAMKO RASMI LA CHADEMA UK KUHUSU JANGA LA BOMU ARUSHA
Ndugu zangu waTanzania wenzangu,
Sisi
watanzania wapigania maendeleo - CHADEMA UK tumelazimika kuwasilisha
majonzi yetu kwenu kwa njia hii, ikiwa ni katika kuonyesha mshikamano wa
kitaifa kwa kujifariji na pia kuwafariji ninyi waTanzania wenzetu
kutokana na tukio kubwa la kuhuzunisha sana ambalo limetokea hivi majuzi
nchini mwetu huko mkoani Arusha.
Pamoja na
kwamba pamekuwa na matukio kadhaa yaliyoikabili nchi yetu hili la
Arusha tumeonelea tulisemee kwa njia ya kipekee,kwa sababu licha ya
kwamba ni tukio la kigaidi, lisilokuwa na mantiki yeyote ile zaidi ya
umwagaji damu wa raia wasio kuwa na hatia,bali pia utekelezwaji wake
unaweza kutuachia athari kubwa sana kisaikolojia na kimahusiano kama
tusipojaribu kulitathmini na kulitafakari kwa upekee wake.
Wakati
ambapo sala na maombi yetu kwa sasa yawaeendee wafiwa na wale ambao
wamedhurika moja kwa moja kimwili ama kisaikolojia kutokana na tukio
hili, tunapenda pia kupongeza juhudi zilizofanywa na kila mmoja wetu
aliyeweza kuwafikia na kutoa msaada wa aina moja ama nyingine kwa
wahanga wa janga hili bila kujali tofauti ya vyama, itikadi, kabila,
dini ama falsafa. Hiyo ndiyo Tanzania tunayoijua sisi. Pamoja na tofauti
zetu nyingi ki hali,afya ama kipato, lakini kamwe hatubaguani katika
misingi ya rangi, kabila ama dini. Na hili ndio haswa linalotusukuma
sisi kuwasilisha huu waraka wa rambirambi kwenu ninyi wenzetu leo hii.
Tuna
imani kwamba vyombo vyetu vya usalama vitafanya utafiti wa kina
kuchimbua na kutujuza chanzo cha ufedhuli huu, ni lazima sisi wenyewe
pia tufarijiane kwa maombi, michango na tafakuri mbalimbali zenye
kutiana moyo katika kipindi hiki kigumu kwetu sote. Tuna imani kwamba
yeyote aliyehusika katika mkakati huu atapatikana na kupewa adhabu
inayostahili.
Kwetu
sote watanzania, huu ni wakati muafaka kuonyesha mshikamano wetu
kuwatumia ujumbe hao wachache wenye nia mbaya kwamba waTanzania
tumeundwa kutoka jumuiya ya makabila zaidi ya mia moja, wenye asili,
rangi, dini na madhehebu mbalimbali na wasioamini. Na kati yetu wote
sisi ni marafiki na ndugu, wengine ni ndugu wa damu kabisa, kupitia
ndoa, wazazi n.k. Hivyo sisi hatuwezi kubaguana wala kuwa na chuki
miongoni mwetu kwani hiyo si asili yetu. Na yeyote yule atakayejaribu
kupandikiza mbegu hii chafu miongoni mwetu tumkatae na kumchukilia hatua
stahiki kumtokomeza yeye na kundi lake.
Ujumbe wetu kwa watanzania ni huu:
HII NI VITA DHIDI YA UMOJA WETU WA KITAIFA NA SIYO KUNDI AU IMANI FULANI.
Asanteni sana, Mungu awabariki nyote. Mungu alibariki taifa letu Tanzania.
Kwa niaba ya CHADEMA UK
G Mboya
Secretary
G Mboya
Secretary
No comments:
Post a Comment