GHASIA KUBWA ZAZUKA MTWARA
Vurugu
hizo zilitokana na hatua ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa
Sospeter Muhongo kusisitiza kuwa bomba la gesi kutoka Mtwara na kuja Dar
es Salaam litajengwa, jambo lingine linalodaiwa kusababisha
ghasia hizo ni hatua ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC)
kutokurusha moja kwa moja matangazo ya Bunge hivyo kuwakosesha wananchi
fursa ya kusikiliza bajeti hiyo.
Hali
ya usalama mkoani Mtwara ni tete. Mtu mmoja anaaminika kufariki dunia
na wengine kadhaa kujeruhiwa kutokana na vurugu kubwa zilizozuka jana
huko Mtwara baada ya kusomwa hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Madini na
Nishati bungeni Dodoma jana.
Aidha,
askari wanne wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), wamefariki dunia
katika ajali wakitokea Nachingwea kwenda Mtwara ili kusaidia kutuliza
vurugu hizo. Katika ajali hiyo, askari 20 walijeruhiwa, wengi wao vibaya
na saba walinusurika.
Kaimu
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Ligula, Dk Mohamed Kodi
alithibitisha kupokea maiti moja na kuomba apewe muda kutaja idadi ya
majeruhi.
Hata
hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Linus Sinzumwa alidai kwamba
hakuna mtu aliyefariki dunia wala majeruhi. Alisema watu 45 wamekamatwa.
Milio ya
risasi za moto na mabomu ya machozi vilisikika kila kona na hasa Mitaa
ya Mdenga, Magomeni na Shengena Mjini Mtwara ambako hali ilikuwa mbaya
kutokana na kuwapo kwa mapambano kati ya polisi na vijana.
Vurugu
hizo zilitokana na hatua ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa
Sospeter Muhongo kusisitiza kuwa bomba la gesi kutoka Mtwara na kuja Dar
es Salaam litajengwa, jambo lingine linalodaiwa kusababisha ghasia hizo
ni hatua ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kutokurusha moja kwa
moja matangazo ya Bunge hivyo kuwakosesha wananchi fursa ya kusikiliza
bajeti hiyo.
Akizungumzia
kukosekana kwa matangazo hayo ya televisheni, Mkurugenzi Mkuu wa TBC,
Clement Mshana alisema kukatika kwa matangazo hayo kulitokana na tatizo
la satelaiti katika mji huo na Musoma.
Hata hivyo, wakazi wa Mtwara waliokuwa na ving'amuzi walipata fursa ya kuangalia matangazo hayo.
Pia
vurugu hizo zilichangiwa na vipeperushi vilivyosambazwa na watu
wasiojulikana wakitaka watu kuacha kufanya shughuli zozote na kukaa
nyumbani ili kufahamu hatima ya mradi wa usafirishaji wa gesi kutoka
Msimbati hadi Dar es Salaam kwa njia ya bomba.
Katika
vurugu hizo zilizozagaa zaidi maeneo ya Mikindani na Magomeni, wananchi
pia waliharibu Daraja la Mikindani linalounganisha Mikoa ya Dar es
Salaam, Lindi na Mtwara.
Tangu
asubuhi kama ilivyokuwa Mei, 17 mwaka huu, Mji wa Mtwara ulikuwa kimya
na huduma nyingi za kijamii zilisimama ikiwamo usafiri wa pikipiki,
daladala, mabasi maduka na masoko.
Katika
Mtaa wa Magomeni, nyumba ya Mwandishi wa TBC, Kassim Mikongolo
iliteketezwa kabisa kwa moto na kundi hilo la vijana. Pia nyumba za
Mbunge wa Mtwara Mjini (CCM), Hasnein Murji na Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Waziri Mkuu, Tamisemi) ambaye pia ni Mbunge wa Mtwara Vijijini, Hawa
Ghasia zilichomwa moto.
Mikongolo
alisema nyumba yake ilichomwa moto saa nne asubuhi... "Walipania
kuchoma nyumba yangu kwa kuwa mke wangu ni Koplo wa Jeshi la Polisi."
Katika
Mtaa wa Majengo, kundi la vijana lilivamia Ofisi ya CCM Kata na Ofisi ya
Serikali ya Kata na kuanza kuzibomoa. Pia nyumba ya Mwenyekiti wa CCM
Wilaya ya Mtwara-Mikindani, Ali Chinkawene ilirushiwa mawe.
Ofisi ya
Mtendaji Mtaa wa Msikitini, Kata ya Reli na Ofisi ya CCM Chikongola nazo
zimeteketezwa kwa moto. Wanafunzi wa Shule za Msingi Shangani na
Majengo walirejeshwa nyumbani baada ya mabomu ya machozi kurindima
kuanzia asubuhi hadi mchana.
"Ni kweli
Ofisi ya CCM na Ofisi ya Serikali ya Kata zimebomolewa, nyumba yangu
imerushiwa mawe," alisema Chinkawene kwa sauti ya chini na kukata simu.
Msimbati shwari
Wakati
Mtwara Mjini hali ikiwa tete, katika Kijiji cha Msimbati ambako gesi
asilia inachimbwa, hali ni shwari na wananchi walikuwa wanaendelea na
kazi zao kama kawaida.
"Maduka
na soko vimefunguliwa, huku hali ikiwa shwari kabisa ingawa msimamo wetu
upo palpale, hatutaki gesi iende Dar es Salaam kwa njia ya bomba,"
alisema mkazi wa kijiji hicho, Juma Ayoub.
JWTZ wafariki ajalini
Kamanda
wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Mtwara, Edward Gontako
alithibitisha kutokea ajali hiyo ya askari wa JWTZ, 41KJ Nachingwea na
kusema wamelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Nachingwea.
Mganga
Mfawidhi wa Hospitali hiyo ya Wilaya, Dk John Sijaona alithibitisha
kupokea maiti za askari hao na kusema hali za majeruhi ni mbaya na
kwamba mipango ilikuwa inafanywa kuwapeleka katika Hospitali ya Ndanda,
Mtwara.
No comments:
Post a Comment