TANZANIA NI SALAMA
Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania
imesema itahakikisha inaendelea kuimarisha hali ya ulinzi na usalama kwa
Watanzania na raia wa kigeni waliopo na wanaoendelea kutembelea hapa
nchini kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za binafsi na
kimaendeleo ili watu wote waweze kutekeleza majukumu yao na kuishi kwa
amani na usalama nchini.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk
Emmanuel Nchimbi alisema hayo jana wakati akizungumza katika kikao baina
yake na Ujumbe wa Wawakilishi wa nchi za Umoja wa Ulaya na mabalozi wa
nchi hizo hapa nchini kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa wizara
hiyo.
Taarifa ya wizara ilisema Nchimbi
alisema kwa sasa Serikali kupitia polisi imejiwekea mikakati mbalimbali
ya kukabiliana na vitendo vya uhalifu katika Jiji la Dar es Salaam na
Tanzania kwa ujumla.
‘‘ Polisi tayari imeanzisha dawati
maalumu litakalowahudumia raia wa kigeni ili kuwawezesha kufungua kesi
zao kwa urahisi, kuwapo kwa wepesi wa majadiliano na ziweze
kushughulikiwa kwa haraka na hatimaye kupatiwa ufumbuzi”, alifafanua
Waziri Nchimbi.
Waziri Nchimbi alisema pia katika
kusimamia suala la ulinzi na usalama wa raia na mali zao kwa sasa wizara
yake itafanya ukaguzi wa kampuni binafsi za ulinzi ili kuangalia na
kujiridhisha kama zinakidhi viwango vya ubora vinavyotakiwa.
Kwa upande wake Kiongozi wa Ujumbe wa
Wawakilishi wa Nchi za Umoja wa Ulaya hapa nchini, Balozi Filberto
Cerani Sebregondi alisema umoja huo utaendelea kushirikiana na Wizara ya
Mambo ya Ndani ya Nchi ambapo pia aliishukuru kwa jitihada inayoendelea
kuchukua kuhakikisha ulinzi na usalama kwa wageni na raia wa Tanzania
unaimarika.
Kwa upande wao mabalozi waliohudhuria
kikao hicho waliitaka Serikali na Watanzania kuhakikisha usalama
unadumishwa ili kutoathiri taswira ya Tanzania kimataifa na hivyo
kuhatarisha uwezekaji na utalii.
Walisema Umoja huo una imani na
Serikali kwamba itaimarisha zaidi masuala ya ulinzi na kuhakikisha raia
wote wanalindwa kwa haki. CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment