GARI LA POLISI LANASWA NA BANGI
Gari aina
ya Toyota Landcruiser linalotumiwa na Mkuu wa Kikosi cha Kutuliza
Ghasia (FFU), Mkoa wa Arusha, lilikamatwa juzi mjini Moshi likiwa
limesheheni magunia 18 ya bangi.
Habari za
awali zilieleza kuwa gari hilo lilikamatwa juzi saa 4:00 usiku katika
Mji mdogo wa Himo, Moshi Vijijini likisafirisha bangi hiyo kwenda
Tarakea, Rombo.
Polisi wawili akiwamo dereva wa gari hilo wanashikiliwa katika Kituo cha Polisi cha Himo na gari lipo Makao Makuu ya FFU, Moshi.
Kamanda
wa Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz alithibitisha kukamatwa
kwa askari hao: "Mchakato wa kuwafikisha mahakama ya kijeshi
unaandaliwa. Bangi hiyo ilikuwa inapelekwa kwa mfanyabiashara mmoja huko
Rombo na ndiye aliyewakodi."
Hata hivyo, Kamanda Boaz alisema atatoa taarifa zaidi leo kwani uchunguzi bado unaendelea.
Bangi ilivyonaswa
Habari
zimeeleza kuwa polisi waliokuwa doria waliliona gari hilo likitengenezwa
na waliamua kuwauliza wenzao kulikoni? Wakajibiwa kuwa kuna kitu
walikuwa wakirekebisha na lilikuwa ni tatizo dogo tu.
"Walipoulizwa
kwani mnaelekea wapi wakasema wanapeleka mzigo wa bosi huko Tarakea
mpakani na kwa taratibu zetu za kijeshi huwezi kuuliza ni bosi gani,"
kilidokeza chanzo kimoja ndani ya polisi.
Hata
hivyo, polisi hao wa doria walirudi katika gari yao ili waendelee na
doria lakini baadhi ya polisi wakamweleza ofisa aliyekuwapo katika gari
hilo kwamba wanashuku gari lile limebeba bangi.
"Lilikuwa
na harufu kali ya bangi na hilo ndilo lililowafanya wale polisi kurudi
tena kwa wenzao na kuwaambia wanataka waone wamebeba nini ndipo
wakakutana na magunia 18 ya bangi," kilieleza chanzo chetu.
Inadaiwa
kuwa baada ya kukuta bangi hiyo, polisi hao waliwasiliana na Mkuu wa
Upelelezi (RCO), Mkoa wa Kilimanjaro, Ramadhan Ng'anzi ambaye naye
alimjulisha Kamanda Boaz.
Ilielezwa kuwa Kamanda Boaz aliagiza kuwekwa mahabusu kwa polisi hao katika Kituo cha Himo na gari hilo lipelekwe FFU, Moshi.
No comments:
Post a Comment