MSHINDI WA TAJI LA MISS NCHINI DENMARK MWAKA 2006 KUSAKA VIPAJI VYA WANAMITINDO YOSO NDANI YA BONGO
Mwanamitindo Victoria Myavilwa aliyewahi
kubeba taji la 'Miss Africa Denmark 2006' amepania kuanzisha kampeni
maalum ya kusaka wanamitindo chipukizi na kuwaendeleza kwa nia ya kukuza
sanaa hiyo inayotoa fursa nyingi za ajira kwa vijana. Victoria ambaye ni Mtanzania aliyeamua kuhamishia makazi yake nchini akitokea Denmark alikoishi kwa zaidi ya miaka 10, amesema kuwa atafanikisha mpango wa kuibua nyota wapya kupitia kampuni yake ya mitindo ya Zera Fashion. "Wakati nikiwa Denmark nilijifunza mambo mengi kuhusu urembo na mitindo... nia yangu ni kutumia ujuzi huo kuibua chipukizi wenye vipaji na kuwaendeleza ili nao wapate fursa ya kufika mbali na kufanikiwa kimaisha," anasema Victoria ambaye alizaliwa Iringa kabla ya kuhamia Denmark. Mwanamitindo huyo ameongeza kuwa ataanza harakati za kusaka wanamitindo wapya mwezi ujao na anaamini kwamba atafanikiwa baada ya muda mfupi kwani kuna vijana wengi wenye vipaji nchini. "Tatizo letu kubwa ni fursa za kupata mahala pa kuanzia. Hata mimi sidhani kama ningefika mbali kama nisingepata nafasi ya kwenda Denmark. Dhamira yangu ni kuwapa nafasi vijana wenye vipaji kama mimi ili mwishowe washiriki pia katika kutangaza mavazi ya Tanzania nje ya mipaka yetu," ameongeza. Mbali na kuwahi kuibuka kidedea katika shindano la kumsaka mrembo wa Waafrika waishio Denmark mwaka 2006, Victoria pia amekuwa akijihusisha na shughuli za mitindo kwa muda wote, hasa katika mji wa Randers ambako ndiko alikosomea katika chuo kiitwacho Randers Tradium kwa miaka minne. |
No comments:
Post a Comment