SERIKALI YATENGA BILLION 326 KUWAKOPESHA WANAFUNZI 95,902 WA ELIMU YA JUU NCHINI KWA MWAKA 2012/13
Na Benedict Liwenga-Maelezo, Dodoma.
SERIKALI
imetenga shilingi Bilioni 326.0 katika mwaka wa masomo 2012/2013 kwa
ajili ya kuwakopesha wanafunzi 95,902 wakiwemo wanafunzi wa mwaka wa
kwanza, ikilinganishwa na kiasi cha Shilingi Bilioni 56.1 kilichokuwa
kimetengwa mwaka wa masomo 2005/2006 kilichomudu kukopesha wanafunzi
42,729. Kauli hiyo imetolewa leo Bungeni mjini Dodoma na
Naibu
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Mhe. Philipo Mulugo wakati akijibu
swali la Mhe. Rashid Ali Abdallah Mbunge Jimbo la Tumbe alilotaka
kujua kwanini Serikali imeshindwa kuwapatia mikopo baadhi ya Wanafunzi
wenye sifa za kuendelea na masomo na Serikali ina mpango gani wa
makusudi kuhakikisha kuwa Wanafunzi hao wanapata elimu.
Alisema kuwa ongezeko hilo la fedha ni
ishara tosha kuwa Serikali ina nia ya kuhakikisha kuwa wanafunzi wote
wenye sifa za kusoma Vyuo vya Elimu ya Juu wanapata mikopo
itakayowawezesha kupata elimu yao katika mazingira mazuri.“Serikali ina nia njema ya kuhakikisha kuwa kila Mtanzania mwenye uwezo wa kusoma Chuo cha Elimu ya Juu anapata fursa hiyo”. Naibu Waziri Mulugo alisema.
Aliongeza kuwa kwa mwaka wa masomo 2012/2013, wanafunzi wa mwaka wa kwanza waliowasilisha maombi ya kupata mkopo walikuwa 37,315, baada ya uchambuzi kufanyika wanafunzi waliobainika kuwa na sifa ya kukopeshwa walikuwa 34,140 lakini kati ya hao ni wanafunzi 30,319 sawa na asilimia 88.9 walipata mikopo.
“Kwa mantiki hii wanafunzi waliokosa mikopo ni 3,821 sawa na asilimia 11.1 ya wanafunzi wote walioomba mkopo, wanafunzi hawa wachache walikosa mikopo hiyo kutokana na ukomo wa kibajeti pamoja na vipaumbele vilivyowekwa na Serikali”. Mhe. Mulugo alisema
No comments:
Post a Comment