DKT. MGIMWA : UCHUMI WA TANZANIA UNAKUA
Waziri wa Fedha Mhe. Dr. Augustao Wiliam Mgimwa amewaeleza Benki ya
Dunia pamoja na Shirika la Fedha la Kimataifa vipimo vya ukuaji wa nchi
yetu kiuchumi ambapo unakuwa kwa asilimia 6.9. Ukuaji huu wa uchumi ni
mkubwa ukilinganisha na ilivyokuwa mwaka uliopita 2011 ambapo ilikuwa
ni asilimia 6.3.
Akizungumzia mfumuko wa bei, Mgimwa alisema kuwa, mfumuko wa bei
umepungua kutoka asilimia 19.8 kwa Desemba mwaka 2011 na kufikia
asilimia 9.8 kwa mwezi Machi mwaka huu 2013. Aidha aliendelea kuongeza
kuwa viwango vya ubadilishaji fedha umeendelea kuimarika na upatikanaji
wa vyakula nao unakwenda vizuri.
Akiendelea kufafanua Mhe. Dkt Mgimwa alisema katika “Mikutano hii ya
majira ya kipupwe inayoendelea hapa Washington inatupatia fursa ya
kueleza hali tuliyofikia katika kuendesha uchumi wetu, nafasi tuliyonayo
kiuchumi, na tunapata nafasi ya kujieleza ni namna gani Tanzania
inavyoweza kukidhi mahitaji ya wananchi wake pamoja na utendaji wa
uchumi wetu. Aidha alisema kuwa Tanzania inapata nafasi ya kuishawishi
dunia ili iweze kutuunga mkono katika maeneo tunayowekeza.
“Katika mikutano hii ya Majira ya kipupwe tunapata nafasi ya kuwa
katika muda mzuri wa kupata uwezekano wa kuyatatua matatizo yetu ya
kiuchumi kwa kuwekeza zaidi ili vyanzo vyetu tunavyowekeza viweze
kutuletea maendeleo ya haraka”. Aidha Mgimwa aliendelea kueleza kuwa
hivi sasa Serikali inawekeza katika gesi iliyoko Mtwara ili itumike
kutoa umeme kwani bei yake ni ndogo ukilinganisha na bei ya mafuta
ambayo yanatumika. Aidha alisema kuwa Gesi hii itasaidia viwanda kupata
umeme na kuongeza ajira pamoja na mapato ya Taifa yatakuwa kwa haraka
zaidi.
“Serikali ina mpango wa kupanua Reli, Bandari ya Dar es Salaam,
Mtwara, Tanga na Bagamoyo ili kurahisisha uingizaji wa mizigo na kukuza
biashara kwa nchi zinazotuzunguka pamoja na kurahisisha usafiri kwa
wananchi kwa njia ya reli.” Aliongeza Mgimwa.
“Tumezungumzia namna ya kuunganisha reli za nchi zinazotuzunguka kama
vile Zambia, Burundi, Rwanda na Uganda hivyo tunavyowaeleza hivi
tunapata wawekezaji wengi wanaotuunga mkono kwa kupitia Benki ya Dunia
na Shirika la Fedha la Kimataifa. Mpaka sasa hivi wameonyasha kwamba
utendaji wa uchumi wa nchi yetu unakwenda vizuri kwa hivyo wana imani
kubwa na nchi yetu. Kwa kuwaeleza hivyo wao wanaweka ushawishi kwa
wawekezaji wakubwa walioko katika nchi zingine”. Alisema Mhe.Dkt Mgimwa.
Mgimwa alimalizia kwa kuwaomba wananchi kuwa, waunge mkono sera
zinazowekwa mbele yao ambazo zinaboresha uchumi, tunaomba wawekezaji
binafsi katika sekta binafsi nao watuunge mkono kwa kuwekeza katika
miradi ambayo tunaiweka mbele yao ili washirikiane kuiboresha na
kuijenga Tanzania. Kila mtu atuunge mkono kwa sababu tunataka Tanzania
ibadilike na kuongeza kasi ya maendeleo ili kila mtu apate nafasi ya
kuboreka kiuchumi. Chanzo: Ingiahedi Mduma, Msemaji- Wizara ya Fedha.
No comments:
Post a Comment