"KILA MTU ANAHAKI YA KUCHINJA NA KULA CHOCHOTE HATA CHURA"...HII NI KAULI MPYA YA RAIS MWINYI
RAIS
mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi amerejea kauli yake kuhusu
mgogoro wa udini akisema kila mtu ana haki ya kuchinja kutokana na imani
yake ilimradi tu asivunje sheria za nchi.
Mwinyi alisema
anashangaa kuona watu wakigombania kitu kidogo kama kuchinja ilihali
Tanzania ina utamaduni wa amani siku zote na kwamba kila mtu ana imani
yake ya dini anayoiamini.
Kiongozi huyo mstaafu alitoa msimamo
huo jana jijini Dar es Salaam katika kongamano juu ya utamaduni wa
Kiislamu Afrika Mashariki ambapo Tanzania imechaguliwa kuwa mwenyeji.
“Imani
ni nafsi ya mtu na haitakiwi kumlazimisha kula nyama iliyochinjwa na
mwenzie. Na kama unaona aliyochinja mwenzio ni kibudu basi usile chinja
yako, kula hata ukitaka kula chura, mjusi, konokono, kula utakacho ruksa
ilimradi tu usiingie katika jinai,” alisema.
Mwinyi alikumbusha
kuwa hata wakati wa utawala wake majaribu kama hayo yaliwahi kumtokea,
lakini alijitahidi kuweka sawa kwa kumwambia kila mtu ale kile
anachofikiri ni chakula bila kumlazimisha mwenzake.
Alisema
Watanzania wamezaliwa ardhi moja na kwamba kinachotakiwa ni kuwa na
misingi ya kuvumiliana, na kwamba sifa ya Uislamu ni pamoja na kuwa na
uvumilivu.
Aliongeza kuwa Uislamu si kufanya vurugu kama
inayotafsiriwa na makundi ya wanaotaka kuvunja amani ya nchi kwa kutumia
jina la dini ya Kiislamu.
Pia alimshukuru Katibu Mkuu wa
Shirikisho la Ulimwengu wa Kiislamu Duniani (Rabita), Dk. Abdullah
Mohsin Al-Turki kwa kuichagua Tanzania katika kuhubiri amani.
Waziri
wa Maji, Prof. Jumanne Maghembe ambaye alimuwakilisha Makamu wa Rais
Dk. Gharib Bilal katika kongamano hilo, alisema kuwa utamaduni wa
Kiislamu Afrika Mashariki na duniani kwa ujumla ni kuvumiliana katika
dini.
Pia aliwataka Waislamu kujiendeleza katika elimu, akisema
kuwa hata Mtume alihamasisha hayo, lakini Waislamu wameshindwa
kuyafuata.
Prof. Maghembe alitoa mfano kuwa Waislamu wana Chuo
Kikuu kimoja wakati dhehebu moja la Lutherani lina vyuo vikuu 11,
akisema ni vyema wakaungana na kujenga vyuo kwa ajili ya kusaidia
kuongeza wasomi katika taaluma mbalimbali.
“Suala la elimu ya
dunia pia ni muhimu, lakini mfano mzuri wa elimu kushuka ni katika mikoa
ya Pwani ambako ndiko ilipoanzia. Mathalani mwaka 1995 wanafunzi
walioanza darasa la kwanza walikuwa 35,000 lakini waliomaliza darasa la
saba ni 9,000. Hapa inaonesha Waislamu tunarudi nyuma,” alisema.
Akizungumza
katika kongamano hilo, Dk. Abdullah Mohsin Al-Turki alisema katika nchi
ya Saudia wanaishi watu tofauti, lakini wakiwa katika upendo huku
akisisitiza kikubwa ni kuheshimiana.
Alisema Rabita imekuwa
ikifanya kazi katika nchi mbalimbali za Nigeria, Gabon, Jamhuri ya Kongo
na baada ya ziara yake nchini hapa atahitimisha kwa kuitembelea Sudan.
Kongamano
hilo limeandaliwa na Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu
Tanzania likiwa na lengo la kusisitiza amani nchini.
Chanzo: Tanzania Daima 11 Aprili 2013
No comments:
Post a Comment